Kwa mujibu wa idara ya tarajama ya Shirika la Habari la Hawza, ikinukuu vyanzo vya Iraq ikiwemo Sumeriyeh News, uchaguzi wa Iraq, ambao upo ukingoni mwa kufanyika, sasa umeingia katika hatua mpya isiyokuwa na mfano wake kwa miaka mingi. Mabadiliko haya yametokea kufuatia mauaji ya mmoja wa wagombea wa uchaguzi ambaye pia alikuwa mwanachama wa Baraza la Mkoa wa Baghdad, tukio ambalo linatajwa kuwa mauaji ya kwanza ya kisiasa yanayohusiana na kampeni za uchaguzi tangu mwaka 2013.
Habari ya kuuawa kwa Safaa al-Mashhadani, mwanachama wa Baraza la Mkoa wa Baghdad na mgombea wa muungano wa Uongozi (al-Siyada), iliripotiwa saa chache baada ya saa nane za usiku wa leo. Kwa mujibu wa watu wa karibu naye, al-Mashhadani alikuwa ameenda katika eneo la Tarmiyah, kaskazini mwa Baghdad, kwa ajili ya shughuli za kampeni zake za uchaguzi, alipouawa baada ya mlipuko wa bomu lililokuwa limepandikizwa kwenye gari lake.
Ofisi yake ya habari ilitoa taarifa ya video kuhusu tukio hilo, ikitoa maelezo ya awali. Katika taarifa hiyo, mkurugenzi wa ofisi yake, bila kutaja majina ya watu au taasisi fulani, alishutumu baadhi ya mitandao ya kisiasa kwa kupanga shambulio hilo. Aliongeza kuwa hii haikuwa mara ya kwanza kwa al-Mashhadani kulengwa katika jaribio la mauaji, lakini safari hii jaribio hilo limefanikiwa.
Mustafa al-Hayali, mkurugenzi wa ofisi ya al-Mashhadani, alifichua juu ya kile alichokiita “njama kamili ya mauaji”. Kwa mujibu wake, bomu hilo liliwekwa kwenye gari wakati mgombea huyo akiwa nje ya eneo la Tarmiyah, kisha likaripuliwa mara tu alipoingia ndani ya eneo hilo. Alisema mpango huo ulilenga malengo mawili kwa wakati mmoja — kumuua Safaa al-Mashhadani na wakati huo huo kueneza taswira kwamba eneo la Tarmiyah ni hatarishi na lisilo salama.
Mauaji ya mgombea wa uchaguzi ambaye pia ni mwanachama wa baraza la mkoa ni tukio lisilo la kawaida na lenye kutikisa mchakato wa uchaguzi wa sasa wa Iraq. Kampeni za “uchaguzi wa damu” ni jambo ambalo Wairaqi hawajalikumbana nalo tangu mwaka 2013.
Kwa mujibu wa Sumeriyeh News, wachambuzi wanakadiria kuwa tukio hili linaweza kusababisha hali ya hofu na vitisho vya kisiasa. Kuna uwezekano mkubwa kwamba raia wengi wa Iraq, kwa kuogopa kulengwa au kushambuliwa, wataepuka kwenda kupiga kura. Vilevile, wagombea wengi watalazimika kuimarisha ulinzi na kuchukua tahadhari kali zaidi, huku baadhi wakionekana kuepuka kuingia katika ulingo wa siasa kwa kuhofia maisha yao.
Kwa mujibu wa wachambuzi hao, hali hii inaweza kusababisha mchakato wa kisiasa na wa kugombea nafasi za uongozi kuwa finyu zaidi, tofauti na miaka iliyopita ambapo ushiriki ulikuwa mpana, jambo ambalo linaashiria kuingia kwa Iraq katika hatua hatarishi ya kisiasa kabla ya uchaguzi wake mkuu
Maoni yako