Alhamisi 16 Oktoba 2025 - 09:45
Kuanza kwa sura mpya ya ushirikiano wa kitamaduni kati ya Iran na India baada kutiwa saini kwa mikataba miwili muhimu mjini Mumbai

Hawza/ Tukiwa tunakaribia maadhimisho ya miaka 70 tangia kuanzishwa kwa Nyumba ya Utamaduni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mjini Mumbai, mikataba miwili muhimu ya ushirikiano wa kielimu na kiutamaduni imetiwa saini na kuhuishwa kati ya kituo hicho na jumuiya ya Hamiat ya Wairani Ithnaashari wanaoishi Pune pamoja na Chuo Kikuu cha Deccan.

Kwa mujibu wa taarifa ya Idara ya tarjama ya Shirika la Habari la Hawza, katika hafla iliyofanyika kwa heshima ya kumbukumbu ya miaka 70 ya Nyumba ya Utamaduni ya Iran mjini Mumbai, mkataba wa ushirikiano wa kielimu na kitamaduni ulitiwa saini kati ya kituo hicho na jumuiya ya Hamiat ya Wairani Ithnaashari walioko Pune.

Katika hafla hiyo, Mohammad Khwaja Nouri, mwenyekiti wa jumuiya hiyo, aliwasilisha ripoti kuhusu shughuli za kielimu na kitamaduni za jumuiya hiyo, huku akibainisha historia ya uendeshaji wa madarasa ya kufundisha lugha na fasihi ya Kifarsi kwa Wairani wanaoishi Pune.

Baadaye, Mohammad Reza Fazel, afisa wa masuala ya kitamaduni na msimamizi wa Nyumba ya Utamaduni ya Iran mjini Mumbai, akirejelea ushirikiano wa mafanikio uliokuwapo katika miaka iliyopita, alieleza kuwa kutiwa saini kwa mkataba huo ni hatua muhimu katika kuendeleza shughuli za pamoja za kielimu na kitamaduni.

Kwa upande wake, Hassan Mohseni-Fard, kaimu mkuu wa ubalozi mdogo wa Iran mjini Mumbai, alisisitiza umuhimu wa kujifunza lugha ya mama, na kuwataka Wairani wanaoishi India kuwa mstari wa mbele katika kuhifadhi na kueneza lugha ya Kifarsi.

Kwa mujibu wa masharti ya mkataba huo, pande zote mbili zitashirikiana katika maeneo kama vile kuandaa tamasha za kitamaduni, kuanzisha madarasa ya lugha ya Kifarsi katika ofisi za jumuiya hiyo, na pia kuendesha warsha za elimu kuhusu utamaduni na historia ya Iran.

Katika kikao kingine, mkataba wa ushirikiano wa kitamaduni kati ya Nyumba ya Utamaduni ya Iran mjini Mumbai na Chuo Kikuu cha Uzamili cha Deccan Pune umesainiwa tena kwa mwaka wa kumi mfululizo.

Waliohudhuria kikao hicho ni pamoja na Hassan Mohseni-Fard, kaimu mkuu wa ubalozi mdogo wa Iran mjini Mumbai; Mohammad Reza Fazel, afisa wa utamaduni; Profesa Joshi, mkuu wa Chuo Kikuu cha Deccan; na Dkt. Sonal Kulkarni.

Mkuu wa Chuo Kikuu cha Deccan, akipokea kwa furaha uamuzi wa ushirikiano huo, alisisitiza umuhimu wa kuendeleza kozi fupi za lugha na fasihi ya Kifarsi, na akapendekeza kuanzishwa kiti maalumu cha lugha na fasihi ya Kifarsi na lugha za kale za Kiajemi.

Kwa upande wake, Hassan Mohseni-Fard, akielezea furaha yake juu ya kusainiwa mkataba huo, alisema kuwa lugha na fasihi ya Kifarsi ni urithi wa pamoja wa mataifa mawili – Iran na India – na akasisitiza umuhimu wa kuendeleza programu za kielimu.

Aidha, Mohammad Reza Fazel, afisa wa kitamaduni wa Iran, alitaja kusainiwa kwa mkataba huo kuwa ni hatua muhimu katika kuimarisha uhusiano wa kitamaduni baina ya nchi hizo mbili, akisema: “Umuhimu wa kuzingatia utofauti wa shughuli na mipango ya baadaye unaonyesha dhamira ya pamoja ya Iran na India katika kukuza ushirikiano wa kitamaduni.”

Mwisho wa kikao hicho, mkuu wa idara ya akiolojia katika Chuo Kikuu cha Deccan alionyesha hamu ya kutiwa saini mkataba maalumu wa ushirikiano kati ya idara yake na Nyumba ya Utamaduni ya Iran – hatua itakayoweka msingi wa utekelezaji wa miradi ya pamoja ya utafiti na uchimbaji wa kihistoria kati ya nchi hizo mbili.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha