Alhamisi 1 Mei 2025 - 07:49
Tamko kutoka katika Ofisi ya Ayatollah al-Udhma Shubeyri Zanjani kuhusiana na ulazima wa kubainisha na kulinda misingi ya itikadi ya maktaba tukufu ya imamiya

Ni jambo la kusikitisha sana kwamba katika nchi ambayo inajivunia kuufuata mwendo wa nuru wa Ahlul-Bayt wa ismah (amani iwashukie), na kuwa mbebaji wa bendera ya uongozi wa Amiri wa Waumini (amani iwe juu yake), mara kwa mara huchapishwa mambo ya matusi yasiyolingana na msingi wa itikadi ya madhehebu, na ukweli wa elimu ya dini hupotoshwa au kufichwa, hali ambayo huujaza huzuni moyo mtukufu wa Imamu wa Zama (Ajalallahu ta‘ala farajahu ash-sharif) na nyoyo za Mashia kwa ujumla.

Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Habari la Hawza, ofisi ya Hadhrat Ayatollah Shubeyri Zanjani, kutokana na kuzingatia umuhimu wa kubainisha misingi ya kiitikadi ya madhehebu ya haki ya Imamiya na ulazima wa kuilinda misingi hiyo mizito ya mwendo huu wa nuru, imetoa tamko ambalo maandishi yake ni kama yafuatayo:

Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema, Mwingi wa Huruma

Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu Mola wa walimwengu wote, na rehema na amani zimshukie Bwana wetu Muhammad na watu wa nyumba yake watoharifu, na laana iwe juu ya maadui zao wote hadi siku ya malipo.

Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w) amesema: "Wafuasi wa Ali ndio watakaofanikiwa siku ya kiyama."

Itikadi ya Shia wa Imamiya inajengwa juu ya misingi imara na mizizi madhubuti kama hoja za kiakili, aya thabiti za Kitabu kitukufu cha Mwenyezi Mungu, mambo yaliyo dhahiri katika dini tukufu ya Uislamu, hadithi mutawatir, na riwaya zenye ishara thabiti na zinazoungwa mkono na ukweli wa kihistoria ulio wazi. Katika kilele cha misingi hiyo ni imani ya juu ya Uimamu na usia wa moja kwa moja wa kiongozi wa waumini Ali bin Abi Talib (a.s), na baada yake uimamu na uongozi wa kizazi chake kitakatifu, ambao kwa hakika ndio nguzo ya imani na msingi wa dini ya kweli. Kama vile bibi mtukufu Fatima Zahra (amani ya Mwenyezi Mungu iwe juu yake) alivyosema katika khutba yake ndani ya Msikiti wa Mtume (s.a.w) baada ya kufariki kwake kuwa, kufuata watu wa nyumba ya ismah (amani iwashukie) ni sababu ya kudumu kwa umma wa Kiislamu, na kwamba lulu ya uimamu ni kiini cha umoja na kinga dhidi ya kila aina ya mfarakano na utengano.

Katika karne nyingi zilizopita, maulamaa wakubwa na watafiti mashuhuri kuanzia Sheikh Saduq, Sheikh Mufid, Sayyid Sharif Murtadha, Sheikh Tusi hadi Allamah Hilli, Khwaja Tusi, na hadi Mir Hamid Husayn Hindi (radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yao) walijitahidi kubainisha misingi hii ya kiitikadi na wakaandika kazi zenye thamani na adhimu.
Kwa njia ya hoja na uthibitisho, walikamilisha hoja mbele ya watu wote na wakaifanya njia ya uwongofu kuwa wazi kwa wanaotafuta ukweli; kazi ambazo zenyewe ni ushahidi wazi wa uhalali wa mwendo wa Ahlul-Bayt wa ismah na utwahara (amani iwashukie).

Kwa msingi huu, ni wajibu wa maulamaa, wanafikra na wenye kalamu kutumia vyanzo vya kuaminika na vyenye ushahidi ili kubainisha, kueneza na kutetea elimu ya haki ya Ahlul-Bayt (amani iwashukie), na kuufanya ukweli wa nuru wa mti mtukufu wa uongozi uonekane wazi kwa sura mbalimbali. Kwani Uislamu wa kweli bila ya imani juu ya uongozi wa kiongozi wa waumini Ally (amani iwe juu yake) ni mfano wa umbo lisilo na roho, lisilo na ukweli.

Maulamaa wa madhehebu, kwa kufuata uongozi wa Maimamu waongofu (amani iwashukie) na maagizo yao, daima wamehimiza kuepuka fitna na migogoro. Hata hivyo, kama ambavyo kuchochea fitna miongoni mwa waislamu si jambo linalokubalika, vivyo hivyo kudhoofisha imani za haki ni kosa kubwa na hasara isiyofidiwa.

Na ni jambo la kusikitisha sana kwamba katika nchi inayojivunia kuufuata mwendo wa nuru wa Ahlul-Bayt wa ismah (amani iwashukie) na kuwa mbebaji wa bendera ya uongozi wa Amiri wa Waumini (amani iwe juu yake), mara kwa mara huenezwa mambo ya matusi yasiyolingana na misingi ya itikadi ya madhehebu, na ukweli wa elimu ya dini hupotoshwa au kufichwa, na moyo mtukufu wa Imamu wa Zama (ajalallahu ta‘ala farajahu ash-sharif) na nyoyo za Mashia kwa ujumla hujawa na huzuni juu ya haya.

Ni lazima wale walio na dhamana ya vyombo vya habari warekebishe mtazamo wa juu juu na urahisishaji wa kueneza itikadi thabiti za Mashia Ithna‘ashariyya, na kwa kushirikiana na wataalamu wenye uelewa wa dini na watu wenye fikra, watambue wajibu wao mbele ya misingi ya kiitikadi ya kishia, na kwa njia ya elimu madhubuti, upangaji makini na ustadi unaostahiki, warekebishe upungufu uliopo.

Ni jambo lililo wazi kwamba mlango wa majadiliano ya kielimu kwa misingi na vyanzo vya Qur’ani na Sunna, kama walivyokuwa wakihimiza wakubwa kama Ayatollah al-Udhma Burujirdi (rahimahullah), uko wazi daima. Na hawza za Kishia zimekuwa tayari kila wakati kwa ajili ya mazungumzo na majadiliano kwa ajili ya kubainisha elimu ya uislamu.

Tunamuomba Mwenyezi Mungu Mtukufu atupe mafanikio na msaada katika kuilinda dini ya Mwenyezi Mungu na kueneza elimu safi ya Ahlul-Bayt (amani iwashukie), na atufanye tuwe miongoni mwa wafuasi wa kweli katika kizazi hicho kitakatifu.

Na amani iwe juu ya yule aliyeufuata uwongofu.

Ofisi ya Ayatollah al-Udhma Shubeyri Zanjani (hafidhahullah)  

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha