Shirika la Habari la Hawza- Tunaamini kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu hafanyi jambo dogo wala kubwa ila kwa msingi wa hekima na maslahi; iwe tunaelewa maslahi hayo au hatuelewi.
Na pia matukio yote madogo na makubwa yanayojiri ulimwenguni yanatekelezwa kwa mpango wa Mola na matakwa yake, ambapo moja ya matukio muhimu zaidi ni ghaiba ya Imam Mahdi (a.s). Kwa hiyo, ghaiba ya Imam huyo pia iko katika msingi wa hekima na maslahi, japokuwa hatujui falsafa yake.
Hata hivyo, huenda mwanadamu anayekiri kuwa matendo yote ya Mwenyezi Mungu yana hekima, na anajisalimisha mbele yake, akatamani kujua siri na hekima za baadhi ya matukio ya ulimwenguni, ili kwa kufahamu falsafa ya jambo fulani anaweza kupata utulivu wa nafsi na ithibati katika moyo. Kwa hiyo, tunachunguza hekima na athari za ghaiba ya Imam Mahdi (a.s), na tunarejea riwaya zinazohusiana na jambo hilo:
1. Kuwaadhibu watu
Wakati Umma unaposhindwa kumthamini Mtume na Imam, na hawatekelezi majukumu yao kwake, bali wanamuasi na kupuuza amri zake, basi ni jambo la haki kwamba Mwenyezi Mungu amuweke mbali kiongozi wao ili wajiangalie nafsi zao, na katika kipindi cha ghaiba yake, watambue thamani na baraka za kuwepo kwake. Na kwa hali hiyo, ghaiba ya Imam ni kwa maslahi ya Umma, hata kama hawajui wala kuelewa.
Imam Baqir (a.s) anasema:
«إِنَّ اَللَّهَ إِذَا کَرِهَ لَنَا جِوَارَ قَوْمٍ نَزَعَنَا مِنْ بَیْنِ أَظْهُرِهِمْ.»
Pindi Mwenyezi Mungu anapochukia kuwepo kwetu miongoni mwa watu fulani, Hututoa kutoka katikati yao. (Ilalu-sharai, juz 1, uk 244)
2. Uhuru na kutokuwa chini ya mkataba wa wengine
Wale wanaotaka kuleta mageuzi au mapinduzi, aghalabu hulazimika awali kufanya mikataba na baadhi ya wapinzani ili waweze kufanikisha malengo yao. Lakini Mahdi al-Maw'ud 1(a.s) ni mrekebishaji mkubwa ambaye hatakubali muafaka wowote na watawala madhalimu katika safari yake ya kuanzisha dola ya haki ya kimataifa. Kwa mujibu wa riwaya nyingi, yeye ameamrishwa kupambana waziwazi na kwa uthabiti na madhalimu wote. Kwa hivyo, hadi mazingira ya mapinduzi yatakapokuwa tayari, ataingia katika ghaiba ili asilazimike kufanya ahadi au mikataba na maadui wa Mungu.
Katika riwaya kutoka kwa Imam Ridha (a.s), sababu ya ghaiba imeelezwa hivi:
«لِئَلاَّ یَکُونَ لِأَحَدٍ فِی عُنُقِهِ بَیْعَةٌ إِذَا قَامَ بِالسَّیْفِ.»
Ili wakati atakaposimama kwa upanga, asiwe na ahadi ya utii kwa yeyote juu ya shingo yake. (Kamalu-d'in, juz 2, uk 480)
3. Kuwatahini watu
Kuwaweka watu katika mitihani ni miongoni mwa desturi za Mwenyezi Mungu. Huwa anawajaribu waja wake kwa sababu mbalimbali ili kiwango cha uthibiti wao katika njia ya haki kiwe dhahiri. Ingawa matokeo ya mtihani yanajulikana kwa Mwenyezi Mungu, lakini katika tanuru la majaribio, ni waja wenyewe wanaojengwa na kugundua hakika ya nafsi zao.
Imam Kadhim(a.s) anasema:
«إِذَا فُقِدَ اَلْخَامِسُ مِنْ وُلْدِ اَلسَّابِعِ فَاللَّهَ اللَّهَ فِی أَدْیَانِکُمْ لاَ یُزِیلُکُمْ عَنْهَا أَحَدٌ یَا بُنَیَّ إِنَّهُ لاَ بُدَّ لِصَاحِبِ هَذَا اَلْأَمْرِ مِنْ غَیْبَةٍ حَتَّی یَرْجِعَ عَنْ هَذَا اَلْأَمْرِ مَنْ کَانَ یَقُولُ بِهِ إِنَّمَا هِیَ مِحْنَةٌ مِنَ اَللَّهِ عَزَّ وَ جَلَّ اِمْتَحَنَ بِهَا خَلْقَهُ.»
Pale atakapopotea wa tano kati ya watoto wa wa saba, mcheni Mwenyezi Mungu kuhusu dini zenu, msiruhusu yeyote awaondoe katika dini zenu. Mwanangu! Bila shaka mwenye jambo hili atalazimika kuwa katika ghaiba mpaka wale waliokuwa wakiiamini Imama wake warejee nyuma. Hakika hilo ni jaribio kutoka kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu ambalo kwayo Huwa jaribu viumbe Wake. (Al-kafi, juz 1, uk 336)
4. Kulinda maisha ya Imam
Mojawapo ya sababu zilizowafanya Manabii wajitenge na kaumu zao ni kulinda maisha yao. Walifanya hivyo ili waweze kuendelea kutekeleza risala zao katika muda mwingine mwafaka, pale walipokuwa katika hatari. Hali hiyo hiyo ilimtokea Mtume wa Uislamu(s.a.w) alipohama kutoka Makka na kujificha pangoni,
bila shaka yote haya ni kwa amri na irada ya Mwenyezi Mungu.
Kuhusu Imam Mahdi (a.s), na sababu ya ghaiba yake, riwaya nyingi zimelieleza jambo hili.
Imam Swadiq (a.s) anasema:
«إِنَّ لِلْقَائِمِ غَیْبَةً قَبْلَ ظُهُورِهِ قُلْتُ ولِمَ؟ قَالَ: یَخَافُ اَلْقَتْلَ.»
Hakika al-Qā’im atakuwa na ghaiba kabla ya kudhihiri kwake. Nikauliza: kwa nini? Akasema: anaogopa kuuawa. (Alghaiba-Sheikh T'usi, juz 1, uk 332)
Ijapokuwa kuuawa kishahidi ni tamanio la watu wa Mungu, lakini shahada inayokubalika ni ile inayotokea katika uwanja wa utekelezaji wa jukumu la Mwenyezi Mungu na yenye manufaa kwa jamii na dini ya Mwenyezi Mungu. Ama pale kuuawa kwa mtu kunamaanisha kupotea kwa malengo na kushindwa kwa ujumbe, basi kuogopa kuuawa ni jambo la busara na lenye kukubalika. Kuuawa kwa Imam wa kumi na mbili (a.s) ambaye ni akiba ya mwisho ya Mwenyezi Mungu, kunamaanisha kuanguka kwa matumaini ya Mitume wote na Mawalii wa Mwenyezi Mungu (a.s), na kutotimia kwa ahadi ya Mola ya kuasisi serikali ya haki duniani.
Inapaswa kutambua kuwa katika riwaya nyingine pia kuna maelezo mengine kuhusiana na sababu ya ghaiba ya Imam wa kumi na mbili (a.s), lakini kwa sababu ya kuepuka kurefusha, hatutazitaja hapa. Hata hivyo, jambo muhimu ni kwamba “ghaiba” ni siri miongoni mwa siri za Mwenyezi Mungu, na sababu yake halisi itadhihirika baada ya kudhihiri kwake. Na yale yaliyotajwa hapa ni sababu zinazochangia katika ghaiba ya Imam wa zama (a.s).
Utafiti huu unaendelea…
Imenukuliwa kutoka katika kitabu “Nagīne Āfarīnish”, huku ikifanyiwa marekebisho kiasi.
Maoni yako