Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Sheikh Mkuu wa Jumuiya ya Shia Tanzania (TIC) Maulana Sheikh Hemedi Jalala Mwakindenge, ameshiriki katika Kongamano la Amani la kitaifa kuelekea Uchaguzi Mkuu 2025 lililofanyika jana tareh 27 /10 / 2025 katika Ukumbi wa Julius Nyerere International Convention Centre ( JNICC ).
Kongamano hilo limehudhuriwa na Viongozi mbali mbali wa Kidini na Serekali, huku wakiongozwa na Mgeni Rasmi Mhe. Prof. Kitila Alexander Mkumbo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji. Katika hotuba yake Sheikh Jalala, aligusia nukta kadhaa muhimu zinazo husiana na tabia ya Mtanzania, ambazo ndizo nguzo kuu za utulivu wa taifa, nukta hizo ni kama ifuatavyo:
1. Mila, desturi na tabia za Watanzania
Watanzania wanajulikana kwa maadili mema, heshima, na utu. Mila na desturi za taifa hili zimejengeka katika misingi ya heshima kwa wazazi, viongozi, na jamii kwa ujumla, utamaduni wa Tanzania umechangiwa na makabila mengi lakini wote wameunganishwa na dhamira moja ya kuheshimiana na kuishi kwa amani. Huu ndio msingi unaoifanya Tanzania kuwa mfano wa kuigwa katika bara la Afrika.
2. Umoja wa kitaifa
Umoja wa kitaifa ndio silaha kubwa ya Watanzania katika kuienzi na kulinda amani, tofauti zilizopo katika upande wa dini, kabila au itikadi za kisiasa hazijawahi kuwatenganisha Watanzania bali zimekuwa chachu na nguvu ya kuimarisha udugu wa kitaifa. Umoja huu ni urithi ulioachwa na waasisi wa taifa, hususan Mwalimu Julius Nyerere, ambaye alisisitiza misingi ya usawa na undugu. Watanzania tunashirikiana katika furaha na huzuni, na hili ndilo linaonyesha uhalisia wa umoja wetu.
3. Mshikamano wa Watanzania
Mshikamano wa kijamii ni sehemu muhimu ya utambulisho wa Mtanzania, mshikamano huo unaonekana wazi katika namna ya Watanzania wanavyosaidiana bila kujali tofauti zao — iwe ni katika majanga ya asili, shughuli za kijamii, au hata katika harakati za maendeleo. Mshikamano huu ni kielelezo cha moyo wa utu na ubinadamu ambao umejengeka katika jamii yetu kwa muda mrefu.
4. Asili ya kuvumiliana
Katika kipengele kingine, Sheikh Mkuu alizungumzia kuhusu uvumilivu, akisema kuwa ni moja ya nguzo zinazotunza amani nchini. Alisema Watanzania wanafahamika kwa uwezo wao wa kusikiliza, kuelewana, na kuheshimu maoni ya wengine.
Kuvumiliana ni tabia ya asili kwa Watanzania. Ndiyo maana dini tofauti zinaishi kwa amani, bila uhasama wala ubaguzi, alisema Sheikh Mkuu, uvumilivu huu ndio unaolifanya taifa hili kuwa kimbilio la amani kwa watu wengi kutoka mataifa mengine.
5. Asili ya upendo na kupendana
Upendo ni roho ya taifa la Tanzania, Watanzania wanaishi kwa moyo wa kusaidiana, kupendana na kuheshimiana. Upendo huo unajidhihirisha kwenye uhusiano wa kijamii, majirani, familia na hata katika siasa za nchi. Upendo ndiyo msingi wa amani. Pale penye upendo hakuna vita, hakuna chuki, hakuna ubaguzi.
6. Tanzania haina desturi ya kubaguana wala kuvunja amani
Tanzania ni taifa lisilo na historia ya migogoro ya ndani inayotokana na ubaguzi. Watanzania wamelelewa katika utamaduni wa kuheshimiana na kuthamini utu wa kila mmoja. Tumelelewa katika kisiwa cha amani, na ni wajibu wetu kuhakikisha kisiwa hiki hakigeuki kuwa uwanja wa chuki, amani ni urithi ambao lazima ulindwe kwa busara, umoja, na maombi ya pamoja.
7. Dua – Silaha ya muumini
Akiwa anakamilisha hotuba yake, Sheikh Mkuu aliwataka Watanzania wote kumtegemea Mwenyezi Mungu katika jitihada za kudumisha amani. Alikumbusha maneno ya Mtume (s.a.w.w) kwamba “Dua ni silaha ya muumini”, akimaanisha kuwa kila changamoto, hofu au tishio la kuvuruga amani linaweza kushindwa kutokana na kumuomba Mwenyezi Mungu kwa ikhlasi. Alisema: “Tuendelee kumuomba Mwenyezi Mungu atupe nguvu ya kulinda amani, kwani amani ni zawadi kubwa zaidi kwa taifa lolote duniani.”

Hitimisho
Kwa ujumla, hotuba ya Sheikh Mkuu wa Jumuiya ya Shia Ithnaasharia Tanzania (TIC) katika kongamano hilo ilikuwa wito wa kipekee kwa Watanzania wote — waendelee kuenzi maadili ya taifa, kudumisha umoja, kuvumiliana, na kuimarisha upendo. Ilisisitiza kuwa Tanzania imejengeka katika misingi ya amani, na ni jukumu la kila raia kuhakikisha urithi huo unalindwa kwa matendo mema na dua za dhati.



Maoni yako