Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Ayatullah Khamenei, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, leo asubuhi katika kikao na mamia ya mabingwa wa michezo mbalimbali na washindi wa medali za Olimpiki za kielimu duniani, aliwaita watu hawa wanaoleta fahari kuwa ni taswira ya ukuaji na uoneshaji wa nguvu ya kitaifa, na akasisitiza:
“Nyinyi mmeonesha kwamba vijana wa Iran wenye matumaini, kama nembo ya taifa, wana uwezo wa kusimama kileleni na kuzielekeza akili na macho ya dunia kwenye anga yenye mwanga ya Iran.”
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, pia kwa kurejelea ubabe na maneno ya upuuzi ya hivi karibuni ya Rais wa Marekani, alisema: “Mtu huyu alijaribu kwa tabia yake ya kujinga na uongo mwingi kuhusu Iran na taifa la Iran, kuwapa moyo Wazayuni na kuonekana mwenye uwezo, lakini kama ana uwezo, aende akawatulize mamilioni ya watu wanaompinga katika majimbo yote ya Marekani.”
Yeye, akieleza furaha yake kutokana na uwepo katika mkutano wa vijana wenye nguvu ambao kwa bidii, juhudi na ushindi katika nyanja za michezo na elimu wamelifurahisha taifa na kuwapa hamasa vijana, alisema: “Medali zenu zina thamani ya juu zaidi kuliko medali za nyakati nyingine, kwani mmezipata katika kipindi ambacho adui katika vita laini anajaribu kufanya taifa liwe na huzuni na lisahau au likate tamaa na uwezo wake, lakini nyinyi kwa kuonesha uwezo na nguvu ya taifa katika uwanja wa vitendo, mmetoa majibu madhubuti.”
Kiongozi wa Mapinduzi alitaja baadhi ya vishawishi kuhusu kukata tamaa kwa vijana kuwa ni maneno yasiyo na msingi, na akasisitiza: “Iran yetu pendwa na vijana wake ni mfano wa matumaini, na ni lazima tuelewe ukweli huu muhimu kwamba kijana wa Kiirani, akijitahidi na kujihimu, ana uwezo na ustadi wa kufika kileleni, kama mlivyo fanya nyinyi katika michezo na elimu.”
Ayatullah Khamenei, kwa kurejelea maendeleo makubwa katika baadhi ya sekta baada ya Mapinduzi, aliongeza: “Mfano mmoja ni haya mafanikio yenu mwaka huu, ambayo huenda hayajawahi kutokea katika historia ya michezo nchini.”
Yeye, akiheshimu kupanda kwa vijana wenye vipaji vya nchini kwenye vilele vya elimu duniani, alisema: “Kazi hizi zenu zinahesabiwa kwa niaba ya taifa la Iran na zinavutia macho kuielekea Iran.”
Kiongozi wa Mapinduzi alieleza “kuiheshimu bendera, kusujudu na dua za wanamichezo waliopata ushindi” kuwa ni alama ya taifa la Iran, na akasema: “Vijana wapendwa wa Olimpiki za kielimu kwa sasa ni nyota ang’avu, lakini baada ya miaka kumi, kwa kuendelea kujitahidi, watakuwa jua ang’avu, jambo ambalo linaweka jukumu muhimu kwa viongozi.”
Ayatullah Khamenei alitaja mchango wa vijana baada ya ushindi wa Mapinduzi kuwa ni mfululizo wa kudumu, akisema: “Katika vita vya kulazimishwa vya miaka 8, kizazi cha vijana kilikuwa ndicho kilichoonyesha ubunifu wa kijeshi licha ya upungufu mwingi na hali ya kuwa mikono mitupu, kiasi kwamba Iran, mbele ya adui aliyekuwa na vifaa vingi na kuungwa mkono kutoka pande zote, ilipata ushindi.”
Yeye alitaja uwanja wa maarifa kuwa ni moja ya nyanja zenye fahari ya wazi kwa vijana wa nchini, na kwa kurejelea uwepo wa Iran katika nafasi kumi za juu duniani katika utafiti na elimu, katika taaluma mbalimbali ikiwemo “nano”, “leza”, “nyuklia”, “viwanda vya kijeshi” na “maendeleo ya tiba”, alisema: “Siku chache zilizopita nilisikia habari muhimu sana kwamba moja ya vituo vya utafiti nchini kimefanikiwa kupata njia ya matibabu kwa ugonjwa ambao haukuwa na tiba.”
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, katika sehemu nyingine ya hotuba yake, kwa kurejelea maneno ya kipuuzi ya hivi karibuni ya Rais wa Marekani kuhusu eneo na Iran pendwa, alisema: “Rais wa Marekani, kwa kusafiri kwenda Palestina iliyokaliwa kwa mabavu na kutoa maneno matupu yaliyojaa upuuzi, alijaribu kuwapa matumaini Wazayuni waliovunjika moyo na kuwapa nguvu ya kisaikolojia.”
Yeye alitaja kipigo cha ajabu cha Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa utawala wa Kizayuni katika vita vya siku 12 kuwa ndicho kilichowakatisha tamaa Wazayuni, na akaongeza: “Wazayuni hawakutarajia kwamba kombora la Kiirani lingeweza kupenya hadi kwenye sehemu zao nyeti na muhimu, na kuziharibu na kuzigeuza kuwa majivu.”
Ayatullah Khamenei alisisitiza kwamba: “Iran haikununua au kukodisha makombora haya kutoka popote, bali ni utengenezaji wa mikono na matunda ya akili ya vijana wa Kiirani.”
Akaongeza: “Kijana wa Kiirani anapoingia uwanjani, kwa bidii na juhudi zake anaunda miundombinu ya kisayansi na anaweza kufanya mambo makubwa kama haya.”
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu alisisitiza: “Makombora haya yaliandaliwa na majeshi yetu na viwanda vyetu vya kijeshi, yakatumika, na bado yapo. Na kama itahitajika tena, yataendelea kutumika wakati mwingine.”
Baada ya kueleza kuwa maneno mepesi na tabia za kijinga za Trump ni kwa ajili ya kuwapa moyo Wazayuni, Ayatullah Khamenei alizungumzia mada kadhaa kuhusu madai yake, akisema: “Katika vita vya Ghaza, Marekani bila shaka ilikuwa mshirika mkuu wa uhalifu wa utawala wa Kizayuni. Kama alivyokiri mwenyewe Rais wa Marekani kwamba ‘tulikuwa tukishirikiana na utawala huo huko Ghaza.’ Hata kama asingesema, ilikuwa dhahiri, kwani silaha na vifaa vilivyokuwa vikimiminiwa juu ya vichwa vya watu wasio na hatia wa Ghaza vilikuwa vya Marekani.”
Ayatullah Khamenei alitaja dai lingine la Trump kwamba Marekani inapambana na ugaidi kuwa ni mfano mwingine wa uongo wake, akiongeza: “Zaidi ya watoto 20,000, wakiwemo vichanga, waliuawa kishahidi katika vita vya Ghaza — je, hao walikuwa magaidi? Gaidi halisi ni Marekani, ambayo ndiyo iliyounda Daesh (ISIS), ikawaleta katika eneo hili, na hadi leo imechukua baadhi ya wanachama wake na kuwahifadhi kwa manufaa yake.”
Yeye alitaja mauaji ya takriban watu 70,000 katika vita vya Ghaza, pamoja na kuuawa zaidi ya Wairani 1,000 katika vita vya siku 12, kuwa ni ushahidi wa wazi wa asili ya ugaidi wa Marekani na utawala wa Kizayuni, na akaongeza: “Mbali na mauaji holela ya watu, waliwaua pia wanasayansi wetu kama Tahranchi na Abbasi, na wakajivunia jinai hiyo. Lakini wanapaswa kujua kwamba hawawezi kuiua elimu.”
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, akirejelea tena maneno ya Rais wa Marekani ambaye alijigamba kwamba amebomoa sekta ya nyuklia ya Iran, alisema:
“Hakuna tatizo, endeleeni kuamini hivyo, lakini hasa wewe ni nani hata utoe masharti kuhusu nchi yenye sekta ya nyuklia? Inahusiana nini na Marekani kama Iran ina uwezo wa nyuklia au haina? Huu ni mwingilio usiofaa, wa makosa na wa kiunyanyasaji.”
Ayatullah Khamenei, akirejelea maandamano ya kitaifa yenye watu milioni saba dhidi ya Trump katika majimbo na miji mbalimbali ya Marekani, alisema: “Kama kweli una uwezo, basi badala ya kusambaza uongo, kuingilia mambo ya nchi nyingine na kujenga kambi za kijeshi humo, nenda ukatulize mamilioni hayo ya watu na uwarejeshe majumbani mwao.”
Ayatullah Khamenei alisisitiza kuwa “gaidi na sura halisi ya ugaidi ni Marekani,” na akataja madai ya Trump ya kuwapenda wananchi wa Iran kuwa ni uongo mtupu, akiongeza: “Vikwazo vya pili vya Marekani, ambavyo mataifa mengi yanaviunga mkono kwa kuogopa, viko dhidi ya taifa la Iran. Kwa hivyo, nyinyi ni maadui wa taifa la Iran, si marafiki zake.”
Akirejelea kauli ya Trump ya utayari wa kufanya ‘makubaliano,’ Ayatullah Khamenei alisema: “Anasema yeye ni mtu wa kufanya makubaliano, ilhali kama makubaliano hayo yanahusisha ubabe na matokeo yake yanajulikana kabla, hiyo si biashara bali ni kulazimisha. Taifa la Iran halitakubali kamwe kushinikizwa.”
Ayatullah Khamenei, akieleza jitihada zinazofanywa na adui ili kuzuia maendeleo ya kisayansi ya Iran, alisema: “Maadui wa taifa la Iran pia wanajaribu, kwa ‘kukanusha au kupuuza baadhi ya mafanikio’, ‘kuchanganya ukweli na uongo’, ‘kukuza makosa madogo’ na ‘propaganda zenye mwelekeo maalum’, kuonesha anga ya Iran kuwa giza na lenye huzuni, lakini nyinyi kwa kusimama juu ya vilele vya michezo na elimu mmeonesha anga yenye kung'ara nchini.”
Alisema; kupoteza imani katika uwezo kuwa ni moja ya mbinu nyingine za adui za kukatisha tamaa taifa na kizazi cha vijana, na akasisitiza: “Kinyume na shughuli hizi, vijana kwa kutegemea nguvu isiyo na mwisho ya ujana, waongeze juhudi zao kwa ajili ya mafanikio, kuleta matumaini na kudhihirisha nguvu ya taifa.”
Kiongozi wa Mapinduzi alitaja kujitolea kwa vijana kutumia vipaji vyao kwa ajili ya taifa la Iran kuwa ni jambo muhimu, na akasema: “Huenda baadhi wanapenda kuishi katika nchi nyingine, lakini watu hawa waelewe kwamba katika nchi nyingine, hata kama watapiga hatua, watabaki kuwa wageni; ilhali Iran ni yenu na ya kizazi chenu, na ni ‘ardhi na nyumba’ yenu.”
Akirejelea maneno mengine ya Trump kuhusu kuwepo kwa kifo na vita katika eneo la Asia ya Magharibi, alieleza: “Vita hivi ni nyinyi mnaovianzisha. Marekani ndiyo mwanzilishi wa vita; pamoja na ugaidi, pia mnaeneza vita. La sivyo, hizi kambi zote za kijeshi mlizo nazo katika eneo hili ni za nini? Mnafanya nini hapa? Eneo hili linahusiana nini na nyinyi? Eneo hili ni mali ya watu wake, na vita na vifo katika eneo hili vinatokana na uwepo wa Marekani.”
Ayatullah Khamenei, akihitimisha hotuba yake, alisema: “Misimamo ya Rais wa Marekani ni ya kimakosa, na katika mambo mengi ni ya uongo na ya dhulma. Ingawa ubabe unaweza kuziathiri baadhi ya nchi, lakini kwa msaada wa Mwenyezi Mungu, kamwe hautaathiri taifa la Iran.”
Maoni yako