Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, ofisi ya Ayatollah Sistani, kufuatia kifo cha Papa Francis, kiongozi wa Kanisa Katoliki, imetoa ujumbe wa rambirambi ambao maandishi yake ni kama ifuatavyo:
بسم الله الرحمن الرحيم
Mheshimiwa Kardinali Pietro Parolin,
Katibu Mkuu wa Serikali ya Vatican
Amani iwe juu yako na heshima tele.
Tukiwa na huzuni kubwa, tumepokea taarifa ya kifo cha Baba Mtakatifu Papa Francis, Papa wa Vatican; mtu ambaye alikuwa na hadhi ya juu ya kiroho na kimaanawi miongoni mwa mataifa mengi duniani, na aliyekuwa akiheshimiwa sana na watu wote. Alitekeleza jukumu mashuhuri katika kuhudumia amani, kuvumiliana, na kuleta mshikamano kwa wanyonge na waliodhulumiwa duniani kote.
Kikao cha kihistoria kilicho fanyika kati ya Papa na Kiongozi Mkuu wa Kishia katika mji mtakatifu wa Najafu lilikuwa ni tukio muhimu sana, ambapo pande zote mbili zilisisitiza nafasi ya msingi ya imani kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu na ujumbe wa Mungu, sambamba na kushikamana na maadili ya juu ya kiroho katika kukabiliana na changamoto kubwa za kibinadamu katika zama hizi. Vilevile, walisisitiza umuhimu wa kuunganisha juhudi za kukuza utamaduni wa kuishi kwa amani, kuepuka vurugu na uchochezi wa chuki, pamoja na kuimarisha maadili, huruma na mshikamano kwa wanadamu, kwa misingi ya kuheshimiana na kutambua haki za kila mmoja miongoni mwa wafuasi wa dini na mitazamo mbalimbali.
Marjaa mkubwa wa dini, anatoa rambirambi na kushiriki majonzi ya pamoja na wafuasi wa Kanisa Katoliki duniani kote kutokana na msiba huu mkubwa, anawatakia subira na utulivu, na anamwomba Mwenyezi Mungu Mtukufu, Mwenye uwezo wote, kwa rehema zake pana, awajalie kheri, baraka na amani wao na wanadamu wote kwa ujumla.
(22 Shawwal 1446 Hijria) sawa sawa na 2025/4/21
Ofisi ya Hadhrat Ayatollah Al-Udhma Sistani (Mwenyezi Mungu aendelee kulilinda kivuli chake) – Najafu Ashraf
Maoni yako