Kwa mujibu wa mwandishi wa Shirika la Habari la Hawza, Ayatullah Mahmoud Rajabi alieleza kuhusu mapambano dhidi ya ubeberu na ukamilifu wa kijamii katika programu ya Semina ya Misbah al-Huda, iliyofanyika jana usiku mbele ya wananchi waliohamasishwa wa Qum.
Alisema: “Suala la ukamilifu wa kijamii ni miongoni mwa mijadala ya kifalsafa kuhusu jamii. Shahidi Murtadha Mutahhari na Ayatullah Misbah Yazdi walijadili suala hili, na pia limejadiliwa katika taaluma ya sosholojia.”
Jihadi Kubwa ya Kujijenga Kiroho ni Sharti la Ushindi katika Mapambano ya Nje
Ayatullah Rajabi alifafanua kuwa; jihadi kubwa yaani kujijenga na kujisafisha nafsi, ni sharti la awali la kupata ushindi katika mapambano ya nje. Hii ni kwa sababu mapambano dhidi ya ubeberu yanawezekana pale tu mtu anapokuwa amepambana na shetani aliye ndani yake na kumshinda.
Alisema: “Mtu anayeweza kuvuka waya wenye miiba wa adui ni yule ambaye tayari amevuka waya wenye miiba wa nafsi yake. Tunapokuwa bado tunahangaika na waya wenye miiba wa nafsi zetu, hatuwezi kuvuka vikwazo vya adui wala kumshinda.”
Mkuu huyo wa Taasisi ya Elimu na Utafiti ya Imam Khomeini (ra) alieleza kuwa; kujijenga kiroho kulianza tangu mwanzo wa uumbaji wa mwanadamu. Alitolea mfano wa kisa cha Habil na Qabil, ambapo sadaka ya mmoja wao haikukubaliwa, jambo lililomfanya Qabil kutishia kumuua ndugu yake.
Habil alimwambia:
«لَئِنْ بَسَطْتَ إِلَيَّ يَدَكَ لِتَقْتُلَنِي مَا أَنَا بِبَاسِطٍ يَدِيَ إِلَيْكَ لِأَقْتُلَكَ»
“Ukininyoshea mkono wako ili kuniua, mimi sitakunyooshea mkono wangu ili nikuue.”
Vilevile, Habil alisema kuwa kutokukubaliwa kwa sadaka ya ndugu yake kulitokana na kukosekana kwa uchamungu, akasema:
«إِنَّمَا يَتَقَبَّلُ اللَّهُ مِنَ الْمُتَّقِينَ»
“Hakika Mwenyezi Mungu hukubali kutoka kwa wachamungu tu.”
Kumtii Walii Faqihi ni Mwendelezo wa Kumtii Mwenyezi Mungu na Mtume Wake (s.a.w.w.)
Mjumbe huyo wa Jumuiya ya Walimu wa Hawza ya Qum aliongeza kuwa; uchamungu unamaanisha kujijenga kiroho na mtu kuwa mwangalifu ili asije akaasi amri za Mwenyezi Mungu. Kadiri nafasi ya mtu inavyokuwa ya juu zaidi, ndivyo anavyohitaji kuwa na kiwango kikubwa zaidi cha uchamungu.
Alieleza kuwa utiifu una mnyororo wa kimamlaka. Kama ambavyo ni wajibu kumtii Mwenyezi Mungu, vivyo hivyo ni wajibu kumtii Mtume (s.a.w.w.), Imam Maasumu (as), na katika kipindi cha ghaiba, kumtii Walii Faqihi.
Ayatullah Rajabi aliendelea kusema kuwa uchamungu unamaanisha mtu kuwa mwangalifu ili asikiuke maagizo ya Walii Faqihi na Kiongozi. Mtu anapaswa kuhakikisha kuwa hapingani na yale ambayo uongozi wa haki umeelekeza. Alisema kuwa mtu anapokiuka maagizo hayo, anakuwa miongoni mwa wale wanaolaaniwa katika sehemu ya Ziyarat Ashura inayosema:
«وَلَعَنَ اللهُ أُمَّةً دَفَعَتْكُمْ عَنْ مَقامِكُمْ، وَأَزالَتْكُمْ عَنْ مَراتِبِكُمُ الَّتِي رَتَّبَكُمُ اللهُ فِيهَا»
“Na Mwenyezi Mungu aulaani umma uliowasogeza mbali na nafasi zenu na kuwaondoa katika daraja zenu ambazo Mwenyezi Mungu alikuwa amewaweka humo.”
Mjumbe huyo wa Kamati ya Uongozi ya Baraza la Wataalamu wa Uongozi alisisitiza kuwa; katika miaka iliyopita kabla ya vita vya hivi karibuni vilivyolazimishwa, wakati wa suala la makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, na pia katika kipindi cha vita hivyo, kama maagizo ya Kiongozi yangetiiwa kikamilifu, leo hii ubeberu usingekuwepo tena.
Kukiuka Mwongozo wa Walii Faqihi Husababisha Madhara kwa Jamii
Mwalimu wa masomo ya juu ya kifiqhi katika Hawza ya Qum alikumbusha kuwa; kila aina ya ukiukaji wa mwongozo wa Walii Faqihi, hata kama unatokana na nia njema ya kutaka kuulinda mfumo wa Kiislamu, husababisha madhara kwenye jamii.
Alieleza kuwa kukosekana uchamungu humfanya mtu kutotambua nafasi ya Walii Faqihi na kuweka maoni yake binafsi mbele ya maoni ya Walii Faqihi. Katika hali hiyo, mtu hutegemea hesabu na tathmini za mambo zinazoonekana kwa nje, huku akipuuzia kanuni na desturi za Mwenyezi Mungu. Matokeo yake ni kufanya makosa katika tathmini na kuisababishia jamii madhara.
Kwa maneno mengine, kukosekana uchamungu binafsi kwa kiongozi mmoja katika kumtii Walii Faqihi kunaweza kusababisha madhara na kushindwa jamii nzima.
Alifafanua kuwa jambo hilo halimaanishi kwamba watu hao hawana dini au wanapinga mfumo wa Kiislamu, bali tatizo linatokana na makosa katika tathmini zao na kukosekana uchamungu kunakowafanya wasizingatie mwongozo wa uongozi. Alinukuu kauli ya Kiongozi aliyeuawa kishahidi, aliyesema kuwa miongoni mwa makosa ya tathmini ni kuchambua matukio kwa kutegemea sababu za kimada zilizo dhaifu na ndogo, ilhali sababu hizo hazina thamani yoyote zinapolinganishwa na uwezo wa Mwenyezi Mungu.
Ayatullah Rajabi alisisitiza tena umuhimu wa kujijenga kiroho akisema kuwa; kwa baraka za Imam aliyeuawa kishahidi wa Mapinduzi ya Kiislamu, sehemu kubwa ya wananchi imejijenga kiroho. Alisema Kiongozi huyo aliijenga jamii na hata baada ya kuuawa kwake kishahidi, watu wengi wameendelea kubadilika na kupata mwamko mpya.
Ndoto ya Trump, Mhalifu, Haikutimia
Ayatullah Rajabi aliongeza kuwa; wananchi wanapokuwa wamejijenga kiroho, Mwenyezi Mungu huwasaidia pia. Alisema kuwa katika vita viwili vya hivi karibuni vilivyolazimishwa, mataifa mawili makubwa yenye silaha za nyuklia, kwa kushirikiana na washirika wao wa Ulaya, yaliikabili Iran, lakini yakashindwa. Alieleza kuwa Trump alitaka kueneza hofu mioyoni mwa wananchi, lakini hadi sasa wananchi hao wamekuwa wakijitokeza katika medani kwa zaidi ya miezi saba. Vilevile, Trump alikuwa amedai kwamba angeusambaratisha mfumo huo ndani ya wiki mbili, lakini kilichotokea kilikuwa kinyume na matarajio yake, kwani mfumo huo ulizidi kuwa na nguvu.
Ayatullah Rajabi alisema kuwa, kama alivyobainisha Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu, kwa mujibu wa tathmini za kawaida zinazoonekana kwa nje, Iran ni dola kuu ya nne duniani, lakini kwa mujibu wa tathmini za kiroho, ni dola kuu ya kwanza duniani. Alisisitiza kuwa mafanikio yote hayo yalipatikana chini ya kivuli cha kufuata na kutii Wilayat al-Faqihi.
Mkuu huyo wa Taasisi ya Elimu na Utafiti ya Imam Khomeini (ra) alisema kuwa; taifa linalomtegemea Mwenyezi Mungu na ambalo maagizo ya Walii wa Mwenyezi Mungu yana nafasi muhimu ndani yake, hupata msaada na kuungwa mkono kutoka kwa Mwenyezi Mungu.
Kujitenga na Wilaya Humpeleka Mtu Katika Kundi la Madhalimu
Ayatullah Rajabi alieleza kuwa kukubali uongozi wa Walii Faqihi ni miongoni mwa sababu zinazoweka mazingira ya kupata msamaha wa Mwenyezi Mungu. Alisisitiza kuwa mtu anayejitenga na Wilaya hujikuta katika kundi la Twa'ghut, yaani mamlaka na nguvu zinazompinga Mwenyezi Mungu na uongozi Wake. Alisema kuwa historia imetuonesha jinsi watu waliojitenga na Wilaya walivyoishia kujiunga na Marekani, Saddam na wengine wenye misimamo kama hiyo. Hata hivyo, alifafanua kuwa mtu anayeyaunganisha maisha yake na Wilaya, Mwenyezi Mungu humwandalia mazingira ya kujirekebisha na kuboresha hali yake.
Tuzuie Watu Wanaofuata Matamanio Yao Kutumia Fursa kwa Maslahi Binafsi
Ayatullah Rajabi alikumbusha kuwa tunapowaona watu wanaoisababishia jamii na mfumo madhara, tunapaswa kusimama dhidi yao na kuzuia watu wanaofuata matamanio yao binafsi wasitumie hali iliyopo kujinufaisha. Alisema kuwa katika kiwango kikubwa zaidi, msimamo huo unapaswa pia kuchukuliwa dhidi ya kambi ya ubeberu wa kimataifa.
Mjumbe huyo wa Kamati ya Uongozi ya Baraza la Wataalamu wa Uongozi alisema kuwa; mchamungu hawezi kukaa kimya mbele ya ubeberu huku akisubiri mpaka ashambuliwe ndipo achukue hatua. Badala yake, anapaswa kuchukua hatua za kukabiliana nao kabla shambulio halijatokea.
Maadui Hawaridhiki na Sisi Kujisalimisha
Akizungumzia msimamo dhidi ya ubeberu wa kimataifa na Uzayuni, Ayatullah Rajabi alisema kuwa kusimama na kupambana dhidi ya nguvu hizo ni sehemu ya mantiki ya Uislamu. Alisisitiza kuwa maadui hawaridhiki na sisi kulegeza msimamo au kujisalimisha, bali wanataka kutuangamiza kabisa. Alisema kuwa jambo hili limerudiwa mara nyingi katika Qur’ani Tukufu. Kwa sababu hiyo, kauli ya Imam Khomeini (ra) iliyosema “Vita, vita mpaka ushindi” imetokana na mafundisho ya Qur’ani Tukufu.
Umuhimu wa Kutangaza Kujitenga na Maadui
Mkurugenzi huyo wa Taasisi ya Elimu na Utafiti ya Imam Khomeini (ra), akizungumzia umuhimu wa kutangaza kujitenga na maadui, alisema kuwa Mwenyezi Mungu anawataja Mtume Muhammad (s.a.w.w.) na Nabii Ibrahim (as) kuwa ni mifano bora ya kuigwa. Alieleza kuwa Mwenyezi Mungu anaonesha jinsi Nabii Ibrahim (as) alivyokuwa mfano bora kwa sababu aliwaambia makafiri na maadui kwamba yeye na wafuasi wake wanajitenga nao na kwamba uadui na chuki yao dhidi yao viko wazi.
Kauli hiyo inapatikana katika Qur’ani Tukufu:
«حَتَّىٰ تُؤْمِنُوا بِاللَّهِ»
“Mpaka mumwamini Mwenyezi Mungu.”
Kulipiza Kisasi kwa Ajili ya Damu ya Kiongozi Aliyeuawa Kishahidi ni Wajibu Kwetu Sote
Ayatullah Rajabi, ambaye pia ni mjumbe wa Baraza Kuu la Hawza alisisitiza kuwa; kulipiza kisasi kwa damu ya Kiongozi aliyeuawa kishahidi ni wajibu kwa kila mtu. Alisema kuwa kila mtu mwenye uwezo anapaswa kulipiza kisasi dhidi ya wote waliohusika katika uhalifu huo, wakiwemo wale waliotoa amri, marubani na wengine waliohusika.
Uislamu Utashinda
Katika sehemu ya mwisho ya hotuba yake, Ayatullah Rajabi alisema kuwa; hatupaswi kuwa na wasiwasi kuhusu maadui, kwa sababu hata wakijitahidi kwa kiwango gani, Uislamu utashinda na ustaarabu wa Kiislamu utatekelezwa. Alieleza kuwa jambo muhimu ni kila mmoja wetu kutekeleza wajibu wake ipasavyo.
Alisema: “Tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa sababu taifa letu limechangia katika suala hili na litakuwa miongoni mwa sababu za kuandaa mazingira ya kudhihiri Imam Mahdi (aj).”
Alihitimisha kwa kusisitiza kuwa na yakini kwamba msaada wa Mwenyezi Mungu ndio utakaowezesha mfumo huu kupata ushindi.
Maoni yako