Alhamisi 8 Oktoba 2026 - 14:33
Wanafunzi wa Tanzania Qum Wakutana na Hujjatul Islam Mahdawipur/ Mazungumzo ya Kuimarisha Harakati za Kiislamu Afrika Yajadiliwa + Picha

Hawza/ Qum, Iran – Kikao maalumu cha kubadilishana fikra na uzoefu kati ya wanafunzi wa Tanzania wanaosoma nchini Iran na Hujjatul Islam Mahdawipur kimefanyika leo, Jumatano, Oktoba 7, 2026, katika mji mtakatifu wa Qum, kikilenga kujadili uzoefu wa shughuli za kidini nchini Tanzania pamoja na njia za kuimarisha harakati za kielimu, kitamaduni na tablighi barani Afrika.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, kikao hicho kilichofanyika leo asubuhi kilihudhuriwa na wanafunzi wa Tanzania wanaoendelea na masomo yao ya Hawza nchini Iran, pamoja na kamati ya Hujjatul Islam Mahdawipur. Kikao kilianza kwa kisomo cha Qur’ani Tukufu, kabla ya Hujjatul Islam Mahdawipur kueleza kwa kina uzoefu na tajriba alizozipata wakati wa safari yake ya hivi karibuni nchini Tanzania, katika maelezo yake, aligusia hali ya shughuli za kidini, kielimu na tablighi, pamoja na fursa na changamoto zinazowakabili Waislamu na taasisi za Kiislamu nchini humo.

Akielezea ziara yake nchini Tanzania, Hujjatul Islam Mahdawipur alisema kuwa: Alifanikiwa kutembelea taasisi mbalimbali za kidini na kielimu, akiwemo Hawza ya Imam Swadiq chini ya usimamizi wa Maulana Sheikh Hemed Jalala, Taasisi ya Bilal Muslim inayosimamiwa na Makhoja, pamoja na taasisi ya Jamiatul Mustafa chini ya usimamizi wa Dkt. Taqawi. Aidha, alitembelea baadhi ya taasisi nyingine za kidini katika mikoa mbalimbali ya Tanzania, ikiwemo Kigoma na maeneo mengine, huku akibainisha umuhimu wa kuimarisha taasisi hizo na kuongeza ushirikiano wa kielimu na tablighi.

Katika muendelezo wa mazungumzo hayo, Hujjatul Islam Mahdawipur alisisitiza pia umuhimu wa kuwepo harakati madhubuti za kielimu na tablighi barani Afrika, miongoni mwa mambo aliyoyaelezea, ni haja ya kuanzishwa Hawza yenye uwezo wa kutoa elimu ya kiwango cha juu barani Afrika, jambo ambalo litawapa nafasi wanafunzi wanaohitimu masomo yao ya juu katika Hawza za Iran kurejea Afrika na kushiriki katika kufundisha, kufanya tablighi na kuwahudumia wananchi. Kwa mtazamo huo, kuandaliwa wataalamu na wanazuoni wenye uelewa mpana wa mazingira ya Kiafrika inaweza ikawa ni hatua muhimu katika kuendeleza elimu ya Kiislamu na kuimarisha kazi za kitablighi katika bara hilo.

Baada ya Hujjatul Islam Mahdawipur kukamilisha maelezo yake, wajumbe mbalimbali walipata fursa ya kushiriki katika majadiliano na kutoa mawazo yao kuhusu namna ya kuimarisha harakati za kitablighi na kumkuza zaidi muballigh wa Kiafrika, hususan kutoka Tanzania. Miongoni mwa walioshiriki katika mjadala huo ni Sheikh Hadari Mshele, Sheikh Athumani Suya, Sheikh Saalim Ra'jih, Sheikh Ha'shir Zakaria, Sheikh Rajabu Hanafi pamoja na wanafunzi na wageni wengine waliohudhuria. Wajumbe hao walitoa mapendekezo na kuainisha nukta mbalimbali zinazohusiana na tablighi, malezi ya wanazuoni na muballighina, pamoja na umuhimu wa kuandaa kizazi cha wataalamu wa dini wenye uwezo wa kukabiliana na mahitaji halisi ya jamii za Afrika.

Kikao hicho kilihitimishwa kwa kusoma kwa pamoja Dua ya Faraji, ambapo washiriki walimuomba Mwenyezi Mungu (swt) aharakishe kudhihiri Imam wa Zama (aj), na pia wakamuomba Mola awape mafanikio katika kuendeleza elimu, tablighi na huduma za kidini kwa jamii ya Tanzania na Afrika kwa ujumla.

Wanafunzi wa Tanzania Qum Wakutana na Hujjatul Islam Mahdawipur/ Mazungumzo ya Kuimarisha Harakati za Kiislamu Afrika Yajadiliwa + Picha

Wanafunzi wa Tanzania Qum Wakutana na Hujjatul Islam Mahdawipur/ Mazungumzo ya Kuimarisha Harakati za Kiislamu Afrika Yajadiliwa + Picha

Wanafunzi wa Tanzania Qum Wakutana na Hujjatul Islam Mahdawipur/ Mazungumzo ya Kuimarisha Harakati za Kiislamu Afrika Yajadiliwa + Picha

Wanafunzi wa Tanzania Qum Wakutana na Hujjatul Islam Mahdawipur/ Mazungumzo ya Kuimarisha Harakati za Kiislamu Afrika Yajadiliwa + Picha

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha