Kwa mujibu wa kitengo cha tarjama cha Shirika la Habari la Hawza, Bi. Booth alizungumza katika Mkutano wa 13 wa Kimataifa wa Badiuzzaman, uliofanyika kuanzia tarehe 4 hadi 6 Oktoba mjini Istanbul, wenye mada ya “Suluhisho za Qur’ani kwenye Migogoro ya Dunia”. Alikosoa mifumo ya udanganyifu wa kisiasa, ushawishi wa makampuni na utamaduni wa ulaji ambao kwa kiwango kinachoongezeka unaunda fikra, matamanio na maisha ya kila siku ya watu.
Booth alianza hotuba yake kwa kurejea Aya za 11 na 12 za Surat Al-Baqarah, ambazo zinawalaani wale wanaoeneza ufisadi huku wakijitambulisha kuwa ni watu wa kuleta amani.
Akirejea simulizi ya Qur’ani kuhusu Nabii Musa (as) na Firauni, alisema kwamba mbinu za mvuto na hofu zilizotumiwa katika zama za kale kudumisha madaraka, katika zama za kisasa zimechukua sura tata zaidi, lakini kimsingi hazijabadilika.
Akiwasilisha simulizi binafsi kuhusu safari yake kuuelekea Uislamu na kusilimu kwake, alisema alipowaambia mabinti zake wawili wadogo kwamba alikuwa akifikiria kuupokea Uislamu, walimuuliza iwapo angeendelea kuwa mama yao, angeacha kunywa pombe na angeanza kuvaa mavazi yenye stara. Alisema kwamba maswali yao yalimwathiri sana na yalidhihirisha kile alichokiita nguvu ya fitra.
Kwa mujibu wa Booth, baada ya kuwaeleza mabinti zake mabadiliko aliyokusudia kuyafanya katika maisha yake, mabinti hao waliupokea Uislamu kwa mtazamo chanya. Booth alihitimisha hotuba yake kwa kutoa wito wa umoja katika jamii ya Waislamu na kuikomboa Palestina.
Chanzo: ILKHA
Maoni yako