Kwa mujibu wa Idara ya tarjama ya Shirika la Habari la Hawza, Hujjatul-Islam Sayyid Muhammad Hadi Mousavi, mwanazuoni wa Kiislamu kutoka Kashmir, amekosoa misimamo ya baadhi ya nchi za Kiislamu kuhusu matukio yanayoendelea Yemen na Palestina. Pia, amesisitiza umuhimu wa umoja na mshikamano miongoni mwa Waislamu, kutatua tofauti zilizopo katika ulimwengu wa Kiislamu na kuwaunga mkono wananchi wa Palestina.
Akizungumzia matukio yanayoendelea katika ulimwengu wa Kiislamu, mwanazuoni huyo aliichambua hali ya Yemen, tofauti kati ya makundi mbalimbali ya Kiislamu na misimamo ya baadhi ya nchi za Kiislamu kuhusu migogoro ya kikanda. Alitoa wito wa kuwepo juhudi za dhati za kurejesha amani, kupunguza mivutano na kuimarisha mshikamano miongoni mwa Waislamu.
Hujjatul-Islam Sayyid Muhammad Hadi Mousavi, akizungumzia tofauti zilizopo nchini Yemen alisema kuwa; nchi kubwa za Kiislamu pamoja na watu wenye ushawishi katika ulimwengu wa Kiislamu zilikuwa na wajibu wa kutumia mafundisho ya Qur’ani Tukufu kufanya juhudi za kurekebisha uhusiano kati ya pande zinazozozana na kuleta amani pamoja na maridhiano.
Akikosoa mwenendo wa baadhi ya nchi za Kiislamu aliongeza kuwa; badala ya kupunguza tofauti na kuweka mazingira ya maelewano, misimamo ya nchi hizo imesababisha kuongezeka mivutano na kuzidi kupanuka mipasuko katika eneo hilo.
Katika kuendelea na hotuba yake, mwanazuoni huyo wa Kashmir alizungumzia mauaji ya raia na kuendelea kwa mashambulizi nchini Palestina, akieleza kukerwa kwake na ukimya pamoja na baadhi ya nchi za Kiislamu kutokuchukua hatua mbele ya uhalifu unaofanywa dhidi ya wananchi wa Palestina.
Akisisitiza umuhimu wa kuwaunga mkono wananchi wa Palestina alisema kuwa; katika hali ambayo Wapalestina wanakabiliwa na mauaji, vitendo vya kikatili na uharibifu mkubwa, baadhi ya nchi za Kiislamu zimeshindwa kutekeleza wajibu wao kwa ufanisi na kwa namna inayostahili katika kuwaunga mkono wananchi hao wanaodhulumiwa.
Vilevile, Hujjatul-Islam Sayyid Muhammad Hadi Mousavi, akizungumzia mwitikio wa baadhi ya nchi za Kiislamu kuhusu hatua zinazochukuliwa na Ansarullah ya Yemen, alieleza kuwa wakati wananchi wa Palestina wanakabiliwa na mashambulizi makubwa, misimamo ya Yemen ya kujilinda imekabiliwa na ukosoaji mkali kutoka kwa baadhi ya nchi za Kiislamu.
Alisisitiza kwamba haki ya kujilinda dhidi ya mashambulizi haiwezi kupuuzwa, na kwamba matukio ya kikanda yanapaswa kuchambuliwa kwa kuzingatia mazingira, hali na vipengele mbalimbali vya kila tukio.
Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, mzungumzaji huyo aliikosoa serikali ya Saudi Arabia kutokana na mwenendo wake. Akisisitiza kwamba serikali hiyo haiwezi kuchukuliwa kuwa mwakilishi wa Uislamu na mafundisho yake halisi, alidai kuwa ufisadi miongoni mwa watawala wa nchi hiyo uko wazi.
Mwisho wa hotuba yake, Hujjatul-Islam Sayyid Muhammad Hadi Mousavi aliwahimiza Waislamu kufuata mwenendo na mafundisho ya Mtume Muhammad Mustafa (s.a.w.w.). Alisisitiza umuhimu wa kudumisha umoja, kuimarisha mshikamano na kujiepusha na tofauti zinazoweza kuwagawa Waislamu.
Pia, aliwataka wanazuoni wa madhehebu na mikondo mbalimbali ya Kiislamu kuongeza hisia zao za kuwajibika kwa kufanya juhudi za kupanua uhusiano wa kindugu, kuimarisha maelewano na kupunguza tofauti miongoni mwa Waislamu.
Mwanazuoni huyo wa Kashmir alihitimisha kwa kusisitiza kwamba, katika hali ya sasa ya ulimwengu wa Kiislamu, umoja, maelewano na ushirikiano wa pamoja katika kutatua tofauti vina umuhimu mkubwa.
Kwa mujibu wake, wanazuoni wa dini wanaweza kutekeleza jukumu muhimu katika kupunguza mivutano, kuimarisha umoja wa Kiislamu na kukabiliana na changamoto zinazoukabili Umma wa Kiislamu, kwa kutegemea mafundisho ya Qur’ani Tukufu na mwenendo wa Mtume Muhammad (s.a.w.w.).
Maoni yako