Jumatatu 12 Oktoba 2026 - 18:00
Siku ya Tatu ya Kampeni ya Kimataifa ya Kuiunga Mkono Palestina

Hawza/ Kampeni ya siku tatu ya mshikamano wa kimataifa na Palestina ilianza siku ya Ijumaa, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya mwaka wa tatu tangu kuanza vita vya Israel dhidi ya wananchi wa Ghaza, shughuli mbalimbali zilizoratibiwa zinatarajiwa kufanyika katika mamia ya maeneo duniani kote.

Kwa mujibu wa Idara ya tarjuma ya Shirika la Habari la Hawza, Muungano wa Kimataifa wa Kuiunga Mkono Palestina umewataka wananchi wa kawaida, harakati za kijamii, mashirika ya kutetea haki za binadamu, vyama vya wafanyakazi, makundi ya asasi za kiraia na mitandao ya mshikamano na Palestina kushiriki katika matukio yaliyopangwa kufanyika kuanzia Ijumaa hadi Jumapili, tarehe 9 hadi 11 Oktoba.

Katika taarifa iliyotolewa siku ya Alhamisi, muungano huo mkubwa uliwataka wafuasi wake kuyafanya maeneo mbalimbali, kiwemo mitaa, viwanja vya umma, mabunge, majukwaa ya habari na mitandao ya kidijitali, kuwa sehemu hai za kuonesha mshikamano na Wapalestina. Aidha, ulitaka kuongezwa shinikizo la wananchi na kisiasa ili kudai haki, uwajibikaji na kukomeshwa ukaliaji wa ardhi ya Palestina unaofanywa na Israel.

Muungano huo ulionya dhidi ya kulifanya kuwa jambo la kawaida au kuukubali ukweli wa miaka mitatu ya mauaji, uharibifu, kuhamishwa kwa nguvu wananchi na kuzingirwa kijeshi Ghaza. Pia, ulitaka kukomeshwa aina zote za ushirikiano wa kisiasa, kijeshi na kiuchumi zinazowezesha uhalifu wa Israel dhidi ya Wapalestina.

Vilevile, wanachama wa muungano huo walitaka kukomeshwa hali ya Israel kutowajibishwa kisiasa katika majukwaa ya kimataifa, hasa katika mazingira ambayo baadhi ya serikali za nchi za Magharibi, zikiongozwa na Marekani, zinaendelea kuiunga mkono rasmi Israel.

Muungano huo ulieleza kwamba; mshikamano haupaswi kuishia katika matamko pekee, bali unapaswa kugeuka kuwa shinikizo la vitendo linalolenga kusimamisha ukiukaji wa sheria na uhalifu unaofanywa na utawala wa Israel.

Kundi hilo lilieleza kuwa; uhalifu wa utawala wa Israel huko Ghaza bado unaendelea, huku likirejelea mashambulizi ya mabomu na mashambulizi mengine yanayoendelea, ambayo yamesababisha vifo vya Wapalestina zaidi ya 1,460 tangu makubaliano hayo yaanze kutekelezwa.

Muungano wa Kimataifa wa Kuiunga Mkono Palestina ulianzishwa mjini London tarehe 26 Julai 2025, kwa ushiriki wa viongozi wa mabunge, vyama vya wafanyakazi na wanaharakati wa haki za binadamu. Muungano huo unafanya kazi ya kuratibu juhudi za wananchi na jumuiya za kimataifa katika kuunga mkono haki na harakati za Wapalestina.

Chanzo: english.palinfo.com

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha