Jumatatu 12 Oktoba 2026 - 16:00
Jibu la Alama Amini Lililomshawishi Mwanazuoni wa Kisunni

Hawza/ Katika kikao kimoja cha kielimu, Alama Amini alikosolewa kuhusiana na sifa za pekee zinazotumiwa kumuelezea Imam Ali (a.s). Hata hivyo, kwa kutoa jibu lenye hoja na ushahidi, aliweza kukifanya kikao hicho kitawaliwe na ukimya.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, kitabu Mihojiano 101 ya Kuvutia na Kusisimua, kilichoandikwa na Muhammad Muhammadi Ishtihardi, kimekusanya mijadala mbalimbali inayohusu masuala ya kiitikadi na kidini. Shirika la Habari la Hawza litaendelea kuchapisha mijadala hiyo katika matoleo yake mbalimbali.

Alama Amini (r.a), mwandishi wa kitabu muhimu cha Al-Ghadir, alishiriki katika kikao kimoja wakati wa safari zake, katika kikao hicho mmoja wa wanazuoni wa Kisunni alimwambia: “Ninyi Mashia mnapitiliza na kuzidisha katika kumuelezea Imam Ali (a.s). Kwa mfano, mnampa majina kama ‘Mkono wa Mwenyezi Mungu’ na ‘Jicho la Mwenyezi Mungu’, si sahihi kumuelezea mmoja wa Maswahaba kwa namna hii ya kupitiliza!”

Alama Amini alijibu bila kuchelewa: “Ikiwa Umar bin Khattab ndiye aliyemtaja Imam Ali (a.s) kwa majina hayo, mtasemaje?” Mwanazuoni huyo akajibu: “Kauli ya Umar ni hoja kwetu.”

Katika kikao hicho hicho, Alama Amini aliomba aletewe mojawapo ya vitabu vya msingi vinavyokubalika katika madhehebu ya Kisunni, kitabu hicho kililetwa naye akaanza kukipitia kurasa zake. Hatimaye, alifungua ukurasa mmoja uliokuwa na hadithi ifuatayo:

Mwanaume mmoja alikuwa akifanya tawafu kuzunguka Al-Kaaba, akiwa hapo alimtazama mwanamke ambaye hakuwa mahram wake kwa mtazamo usiofaa, Imam Ali (a.s) alimwona akiwa katika hali hiyo, akampiga usoni kwa mkono wake na hivyo kumuadhibu. Mwanaume huyo, akiwa ameushikilia uso wake kwa mkono na akiwa amekasirika sana, alikwenda kwa Umar bin Khattab na kumweleza kilichotokea, akilalamika kuhusu kitendo cha Imam Ali (a.s). Umar alimjibu kwa kusema:

قَدْ رَأَى عَيْنُ اللهِ وَضَرَبَ يَدُ اللهِ

“Hakika, jicho la Mwenyezi Mungu limeona, na mkono wa Mwenyezi Mungu umepiga.”

Kauli hii ilikuwa na maana ya kwamba jicho la Imam Ali (a.s) haliwezi kukosea katika yale linayoyaona, kwa sababu ni jicho linaloongozwa na kumuamini Mwenyezi Mungu; na jicho la namna hiyo halikosei. Vilevile, mkono wa Imam Ali (a.s) hautendi jambo lolote isipokuwa lile linalofanywa kwa ajili ya kutafuta radhi za Mwenyezi Mungu.

Mwanazuoni aliyekuwa ameuliza swali alipoiona hadithi hiyo ndani ya kitabu hicho, alielewa hoja iliyotolewa na Alama Amini na akashawishika na jibu lake.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha