Jumatatu 12 Oktoba 2026 - 20:00
Simulizi ya Upendo na Matumaini Yachipuka Katikati ya Maangamizi ya Gahza

Hawza/ Katikati ya mahema ya wakazi wa Ghaza waliolazimika kuyakimbia makazi yao ambako vita vimezivunja familia na kugeuza nyumba kuwa magofu, Ibrahim na Maryam wameamua kuanza maisha yao ya ndoa wakiwa na matumaini ya siku bora zijazo, licha ya kuwapoteza wanafamilia wao wote.

Kwa mujibu wa Idara ya Kimataifa ya Shirika la Habari la Hawza, simulizi ifuatayo ni hadithi ya upendo inayotoka ndani ya maisha ya ukimbizi huko Ghaza, ambako licha ya uharibifu na kupoteza wapendwa wao, mapenzi na matumaini bado yanafungua njia ya kuendelea kuishi.

Katika kona moja ya kambi ya wakimbizi iliyoko katika mji wa Deir al-Balah, katikati ya Ukanda wa Ghaza, ambako mahema yanafanana kwa rangi lakini kila moja lina simulizi tofauti kuhusu maisha ya wakazi wake, furaha ndogo ilikuwa ikianza kuchipua taratibu.

Hapa hapakuwa na ukumbi wa harusi uliopambwa kwa maua, wala taa za kuvutia zilizoweza kuwashangaza watu. Hata hivyo, sauti za vifijo vya furaha kutoka kwa wanawake zilizokuwa zikisikika katikati ya mahema yaliyochakaa zilitosha kufikisha ujumbe kwa kila mtu: “Hapa maisha bado yanaendelea, na kuna mapenzi ambayo hayakubali kuahirisha mwanzo wake.”

Katika siku ambayo ilikuwa ya kipekee katika maisha ya Ibrahim, kijana mwenye umri wa miaka 26 alifunga ndoa na Maryam, msichana mwenye umri wa miaka 22, ili waanze maisha yao ya pamoja chini ya paa la kitambaa. Huo ulikuwa mwanzo wa maisha yao ya ndoa uliofanyika licha ya matatizo yote na uchungu wa hali halisi wanayoikabili.

Majeraha ya Pamoja na Matumaini Mapya

Hadithi ya Ibrahim na Maryam si simulizi tu kuhusu vijana wawili waliokutana na kuamua kuoana, bali ni hadithi ya majeraha mawili yaliyounganishwa na kuwa karibu na kuanza kupona kupitia huruma, kuelewana na mapenzi.

Ibrahim ndiye pekee aliyenusurika katika familia yake, ambayo wanafamilia yake wote waliuawa katika shambulio la anga lililolenga nyumba yao. Alitolewa chini ya vifusi akiwa amejeruhiwa, na athari za majeraha hayo bado zinaonekana mwilini mwake na mguuni, ambao hutegemea wakati anapotembea.

Maryam naye alipitia janga linalofanana na hilo, nyumba ya familia yao pia ilishambuliwa, na akawa ndiye pekee aliyenusurika miongoni mwa ndugu zake, pamoja na baba na mama yake. Maryam alikaa hospitalini kwa miezi mingi ili kutibiwa majeraha makubwa yaliyokuwa yameathiri sehemu mbalimbali za mwili wake.

Ibrahim alisema huku akiimarisha moja ya pembe za hema alilolijenga kambini kwa msaada wa majirani zake: “Nilipoipoteza familia yangu na mimi mwenyewe kujeruhiwa, nilidhani maisha yalisimama wakati huo huo, lakini nilipoona jinsi hali ya maisha yangu na ya Maryam ilivyofanana, nilihisi kwamba Mwenyezi Mungu ametupa nafasi nyingine ya kuyaweka majeraha yetu pamoja na kujenga familia mpya kutoka kwenye majivu ya maangamizi.”

Aliongeza kusema: “Katika hali hii ngumu ya kiuchumi, hatukuweza kufanya sherehe ya kawaida ya harusi wala kununua dhahabu, hata hivyo, tulikubaliana kwamba ili kuanza maisha yetu, hatuhitaji kitu kingine isipokuwa makazi yatakayotukusanya pamoja na ahadi ya dhati baina yetu.”

Katika hema lililokuwa jirani, Maryam alikuwa akijiandaa kwa siku kubwa ya maisha yake huku akitegemea azma yake imara. Wakati huohuo, wasichana wa kambini walikuwa wakitengeneza shada la maua la ubunifu kwa kutumia karatasi za kadibodi zenye rangi mbalimbali, ili wampe bibi harusi kama zawadi.

Maryam alisema huku akiitazama nguo ya kitamaduni na rahisi aliyokuwa ameiandaa kwa ajili ya siku hiyo maalumu: “Sisi sote wawili tuna majeraha yasiyoweza kusahaulika, yaliyo kwenye miili yetu na katika kumbukumbu zetu. Tumepoteza familia zetu, nyumba zetu na kila kitu tulichokuwa nacho. Hata hivyo, tumeamua kutobaki mateka wa huzuni na majonzi ya kuwapoteza wapendwa wetu.”

Aliendelea kusema kwa sauti yenye msimamo: “Tunajua kwamba hakutakuwa na magari yatakayotusindikiza kuelekea kwenye nyumba yetu ya ndoa, lakini furaha ya dhati tunayoiona leo machoni mwa majirani zetu kambini, wanapotusaidia kuandaa hema letu, ni ya kweli zaidi na itadumu katika kumbukumbu zetu kuliko sherehe na taratibu nyingine zozote.”

Maryam aliongeza kusema: “Tunataka kujithibitishia sisi wenyewe na kuuthibitishia ulimwengu mzima kwamba haiwezekani kutuvunja moyo kabisa, na kwamba hema hili ni la muda tu, hadi pale Ghaza itakaporejea katika hali yake ya zamani.”

Hadithi ya Ibrahim na Maryam inaonesha uzoefu wa kipekee wa kibinadamu wa kizazi cha manusura wa vita katika Ukanda wa Ghaza, ni kizazi ambacho hata katikati ya mazingira magumu zaidi, kinasisitiza kufafanua upya maana ya utulivu na amani katika maisha.

Maelezo madogo ya sherehe ya ndoa ya vijana hawa wawili hayakuwa tu matokeo ya kulazimishwa na hali ngumu ya maisha, bali yalifanana na ushindi wa kweli wa roho na utashi wa mwanadamu, kwa mara nyingine tena, tukio hili limeonesha kwamba mapenzi yanaweza daima kupanda mbegu ya uhai na kumfungulia mwanadamu upeo mpya, hata katikati ya magofu na mahema.

Chanzo: Shirika la Habari la Safa la Palestina.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha