Jumanne 13 Oktoba 2026 - 15:11
Majlisi za Fatimiyyah Zilenge Kuimarisha Ushiriki wa Wananchi Mitaani na Kujiandaa Kukabiliana na Changamoto za Malezi, Utamaduni na Jamii kwa Busara

Hawza/ Ayatullah A‘rafi, akiwahutubia wahubiri wa siku za Fatimiyyah, amesisitiza umuhimu wa kutumia fursa zote za ufafanuzi na uenezi wa mafundisho ya dini, hususan katika siku za Fatimiyyah, kwa ajili ya “kuimarisha ushiriki wa wananchi waliohamasishwa katika mitaa” na kujiandaa kukabiliana kwa busara na changamoto pamoja na hatua ngumu zinazotarajiwa katika siku zijazo.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, ujumbe wa Ayatullah A‘rafi, Mkurugenzi wa Hawza nchini Iran, uliotolewa kwa mnasaba wa siku za kumbukumbu ya kuuawa kishahidi Bibi Fatimah Zahra (sa), ni kama ifuatavyo:

Kwa jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, Mwenye Kurehemu.

Ewe Mwenyezi Mungu! Mteremshie rehema na amani Siddiqah al-Tahirah Fatimah al-Zakiyyah, na uwe, Ewe Mwenyezi Mungu, mwenye kulipiza kisasi kwa ajili ya damu yake, damu za watoto wake na damu za mashahidi wetu.

Ninatoa rambirambi zangu kwa wananchi wote waheshimiwa wa Iran, Hawza, wanazuoni wakuu, wanazuoni wa dini wenye ufahamu na utambuzi, pamoja na wahubiri walio macho na wenye mwamko, kufuatia siku za kumbukumbu ya kuuawa kishahidi Bibu Fatimah Zahra (sa).

Vilevile, ninatangaza kusitishwa masomo ya ngazi za juu ya kifiqhi na vituo pamoja na taasisi maalumu za Hawza zilizopo Qum, kuanzia tarehe 13 ya mwezi wa Jumada al-Ula hadi mwisho wa wiki, ambayo inalingana na tarehe 2 hadi 7 ya mwezi wa Aban, kwa uratibu na Mara'ji wakuu wa kidini, Baraza Kuu la Hawza na taasisi za Hawza. Hatua hii inalenga kuwawezesha wanafunzi wa Hawza na wanazuoni vijana kuhudhuria maeneo mbalimbali kwa ajili ya kufanya kazi ya tablighi kwa ari ya jihadi na kujitolea katika harakati za kidini.

Masuala yanayohusiana na mipango ya shughuli za tablighi, likizo katika mikoa na masomo ya ngazi ya kwanza ya Hawza, yakabidhiwe kwa wakurugenzi husika kwa uratibu na Naibu Mkuu.

Ninatumia fursa hii, katika mnasaba wa siku za tablighi za Fatimiyyah (sa), kukumbusha mambo kadhaa:

1. Umuhimu wa kufafanua nafasi na utukufu wa Bibi Fatimah Zahra (sa)

Nafasi na utu wa Bibi Fatimah Zahra (sa), bibi wa wanawake wa walimwengu wote wawili, imeakisiwa katika urithi wa Qur’ani, riwaya, historia na mafundisho ya Kiislamu. Vilevile, hazina kubwa ya mafundisho na urithi ulioachwa na Bibi huyo inaonesha vyeo na daraja zake za juu, ambazo ziko nje ya mipaka ya fikra za kawaida za mwanadamu.

Kwa hakika, hakuna anayeweza kufahamu undani wa utu na nafasi yake isipokuwa Maasumu (as), kwani daraja zake ni za juu kiasi kwamba haziwezi kufikiwa kikamilifu wala kuelezwa kwa ukamilifu. Hata hivyo, kama ambavyo haiwezekani kuchota maji yote ya bahari, mtu hapaswi kuacha kabisa kunywa maji hayo; bali anapaswa kuchota kwa kadiri ya kiu yake.

Bila shaka, kuna umuhimu mkubwa wa kujifunza na kupata mwongozo kutoka katika mwenendo wake wenye nuru, kwani yeye ni dhihirisho la nuru ya Mwenyezi Mungu, njia ya kufikishwa neema za Mwenyezi Mungu, na mfano bora wa kuigwa kwa Maimamu Watoharifu (as) pamoja na wanawake na wanaume wote duniani. Yeye ni mtu mwenye nafasi na utukufu mkubwa, ambaye hakusita kujitolea kwa namna yoyote ile katika kutetea eneo takatifu la Wilaya na uongozi wa kidini.

Kwa hiyo, kufafanua daraja yake, utukufu wake, dhuluma aliyofanyiwa, kauli zake na mwenendo wake mtakatifu, hususan katika siku za Fatimiyyah, ni wajibu wa wanafunzi na wanazuoni wa Hawza, wahubiri na wanazuoni wa dini kwa ujumla.

Kutokana na hilo, inafaa vituo vya uenezaji na ufafanuzi wa dini, walimu wote, wanazuoni vijana, wahutubiaji, wahubiri na wasomi wa Hawza, katika siku hizi za tablighi na kipindi hiki nyeti cha kihistoria, watekeleze wajibu wao kama askari wa kulinda ngome za dini na wabeba bendera ya tablighi, ufafanuzi na usimamishaji wa dini, sambamba na majukumu yao ya kielimu na kiutendaji.

Kwa kutegemea aya hii tukufu:

«أَنْ تَقُومُوا لِلّهِ مَثْنى وَ فُرادى»

“Msimame kwa ajili ya Mwenyezi Mungu wawili wawili na mmoja mmoja.”

Wanapaswa kuunda makundi ya tablighi, kuhuisha na kuchangamsha misikiti pamoja na mikusanyiko ya Fatimiyyah, huku wakizingatia hasa lengo la “kuimarisha ushiriki wa wananchi waliohamasishwa katika mitaa.”

Aidha, wanapaswa kutoa kipaumbele maalumu katika kufafanua nafasi ya kiutambuzi na kielimu, kiibada, kijamii na kisiasa ya mwanamke huyo wa pekee, na kuanzisha harakati nyingine ya jihadi ya ufafanuzi katika maeneo yote ya nchi.

2. Mafanikio katika tablighi yanategemea kutatua matatizo ya wananchi na kuimarisha umoja

Ni wazi kwamba ushindi katika uwanja wa tablighi, malezi ya kidini na malezi yenye misingi ya Mapinduzi ya Kiislamu unategemea kutatua matatizo ya wananchi, kujitahidi kupunguza maumivu na mateso yao, kuwasaidia viongozi na maafisa waheshimiwa katika kutekeleza majukumu yao, pamoja na kuwawajibisha kwa njia ya haki na ujasiri, huku umoja na mshikamano vikihifadhiwa chini ya uongozi wa Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Mujtaba Khamenei (Mwenyezi Mungu amuhifadhi).

Kwa sababu hiyo, ni jambo la lazima kuunda vikundi vya kudumu vya huduma kwa wananchi na vijana. Vilevile, viongozi na maafisa waheshimiwa wa nchi katika ngazi mbalimbali, wanapaswa kuboresha zaidi juhudi zao za kutatua matatizo na kuendeleza maendeleo ya nchi, na kupunguza matatizo ya wananchi, hususan matatizo ya kiuchumi.

Wananchi wenye azma na viongozi waheshimiwa wanaweza, kwa kutegemea utamaduni na uchumi wa kujitegemea na kustahimili shinikizo, kuivusha nchi katika kipindi hiki nyeti.

3. Ujasiri, subira, muqawama na mshikamano ni hazina muhimu ya taifa la Iran

Ujasiri na ushujaa, uwezo wa kustahimili hali ngumu na kupambana na changamoto, kuwa macho na kuwa imara, umoja mtakatifu na mshikamano wa kijamii, kufuata Uislamu na uongozi, na kwa ujumla utamaduni wa jihadi na shahada, ni hazina zisizo na kifani za taifa la Iran lenye azma na mhimili wa Muqawama.

Hazina hizi ni muhimu katika kuvuka hatari kubwa, kuelekea katika ustaarabu mpya wa Kiislamu, kuipa Iran yetu pendwa, yenye nguvu na inayoendelea heshima na hadhi inayostahili, na kufanikisha ushindi wa Umma wa Kiislamu, taifa la Iran na vikosi vyetu vya kijeshi dhidi ya wenye kujiona wakuu duniani, wanyonyaji wa dunia na wavunja mikataba wa Marekani na Uzayuni.

Kwa hiyo, ni lazima kutumia fursa zote za ufafanuzi, tablighi, elimu na malezi, hususan katika siku za Fatimiyyah, ili kuimarisha utamaduni huu na kuendeleza mazungumzo na mtazamo huu wa kimafundisho. Vilevile, ni lazima kuimarisha utayari wa kukabiliana kwa busara na changamoto zote pamoja na hatua ngumu zinazotarajiwa katika siku zijazo.

4. Umuhimu wa kufafanua mwenendo wa maisha ya Bibi Fatimah Zahra (sa) katika kukabiliana na changamoto za kitamaduni, malezi na kijamii

Katika mazingira ya sasa, tunapokabiliana na changamoto za kitamaduni ambazo zimeziweka katika hatari misingi ya familia, jamii yenye afya na maendeleo, pamoja na thamani za hijabu na kujisitiri, kufafanua mwenendo wa maisha ya kistaarabu, yenye imani na yenye kujisitiri ya Bibi Fatimah Zahra (sa), mwanamke mwenye nafasi ya kwanza katika ulimwengu, ni miongoni mwa wajibu muhimu wa wananchi wote.

Wajibu huu unawahusu hasa wanawake wacha Mungu, wasichana wenye usafi wa maadili, pamoja na ndugu zetu wanaume na wanawake miongoni mwa wanazuoni wa dini na wahubiri.

Ni lazima kutumia uwezo na fursa zote zilizopo katika vyombo vya habari na majukwaa ya kidijitali, mikusanyiko ya kitamaduni na kidini, pamoja na mbinu mbalimbali za malezi na tablighi, ili kupunguza madhara ya kimaadili, kitamaduni na kijamii.

Vilevile, ni lazima kutumia fursa ya siku za Fatimiyyah kwa ajili ya kufikia malengo hayo na kuzitaka taasisi zote zenye dhamana kutafuta suluhisho na kuchukua hatua zinazohitajika kwa mujibu wa sheria.

Kwa kuwasalimu Manabii, Mawalii na wasii wa Mwenyezi Mungu, hususan Mwisho wa Manabii, Muhammad (saww), na Hadhrat Baqiyyatullah al-A‘dham (aj), Mwenyezi Mungu aharakishe kudhihiri kwake, pamoja na Imam Khomeini (Mwenyezi Mungu aiweke roho yake takatifu katika rehema Zake), mashahidi wote wa Vita vya Tatu Vilivyolazimishwa, hasa Kiongozi na Imam aliyekufa kishahidi (Mwenyezi Mungu aiweke roho yake katika rehema Zake), Mara'ji wakuu wa kidini, Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu, vikosi vya kijeshi na mhimili wa Muqawama, ninamuomba Mwenyezi Mungu awajaalie afya, heshima na ushindi wananchi wa Iran wanaostahimili changamoto, Umma wa Kiislamu uliopewa jukumu la kuleta mabadiliko, viongozi wa kuongoza Umma (Mwenyezi Mungu awarehemu) na wanazuoni watukufu wa dini.

Natumaini kwamba shughuli zote za maombolezo na juhudi za wote wanaojishughulisha katika uwanja huu zitapata uangalizi na upendeleo maalumu kutoka kwa Mwenyezi Mungu, Aliye Mtukufu na Aliye Juu kabisa.

Sifa zote njema ni za Mwenyezi Mungu, Mola wa walimwengu wote.

Ayatullah Alireza A‘rafi
Mkurugenzi wa Hawza nchini Iran.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha