Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Maadhimisho hayo yamefanyika katika vituo mbalimbali vya Bilal Muslim vilivyopo sehemu tofauti za Tanzania, yakilenga kuwakumbusha waumini na jamii kwa ujumla kuhusu maisha matukufu ya Mtume Muhammad (saww), mafundisho yake na ujumbe wake wa kuhimiza upendo, umoja, huruma na mshikamano miongoni mwa wanadamu.
Miongoni mwa vituo vilivyoshiriki katika maadhimisho hayo ni Kituo cha Bilal Muslim Ikwiriri, Kilwa Kivinje, Lindi, Mafia, Ngarenairobi, Mtandi, Muangaza na Moshi.
Hafla hizo zilikuwa fursa muhimu kwa waumini kukutana pamoja, kusoma na kusikiliza mawaidha yanayohusiana na maisha na mwenendo wa Mtume Muhammad (saww), huku zikichochea zaidi moyo wa kumpenda na kufuata mwenendo wake katika maisha ya kila siku.
Aidha, maadhimisho hayo yameonesha namna vituo vya Bilal Muslim vinavyoendelea kuwa na nafasi muhimu katika kuimarisha elimu ya dini, malezi ya kiroho na mshikamano wa Waislamu katika maeneo mbalimbali nchini.
Sherehe za Maulid ya Mtume Muhammad (saww) zimeendelea kuwa wakati wa furaha na tafakuri kwa Waislamu, ambapo waumini hukumbushwa kurejea katika mafundisho ya Mtume Mtukufu na kuyafanya kuwa msingi wa kuijenga jamii yenye upendo, amani, maadili mema na mshikamano.





Maoni yako