Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Ayatullah Sayyid Muhammad Saidii ameyasema hayo katika hafla ya kusomewa khutuba maalumu kwa ajili ya watumishi wa Haram Tukufu ya Bibi wa Karama, iliyofanyika katika ukumbi wa Imam Khomeini (r.a.) ndani ya Haram ya Bibi wa Karama, ikiwa imehudhuriwa na viongozi na maafisa wa taasisi mbalimbali za kiutendaji za Mkoa wa Qum.
Akianza kwa kuwakumbuka Mashahidi wa Mapinduzi ya Kiislamu na mashahidi wa matukio ya hivi karibuni, Ayatullah Saeedi alisema: “Nafasi ya mashahidi ambao kwa miaka mingi walihudumu katika njia ya Mapinduzi ya Kiislamu na kulinda maadili yake itabaki kuwa ya kudumu miongoni mwa Umma wa Kiislamu. Kuwakumbuka kwao kunavikumbusha vizazi vijavyo njia ya uwajibikaji na utumishi.”
Akiashiria picha za mashahidi wa hivi karibuni pamoja na kiongozi shahidi wa Mapinduzi ya Kiislamu zilizowekwa katika eneo ilipofanyika hafla hiyo, aliongeza: “Picha hizi zinatukumbusha ukweli wa kwamba; dunia hii si mahali pa mwanadamu kubaki milele, na kinachobaki kwa mwanadamu ni namna alivyotekeleza wajibu wake na njia aliyoichagua katika kipindi cha maisha yake.”
Ayatullah Saeedi, akirejea Aya tukufu isemayo:
«یَا أَیُّهَا الَّذِینَ آمَنُوا اذْکُرُوا نِعْمَتَ اللَّهِ عَلَیْکُمْ»
“Enyi mlioamini! Kumbukeni neema ya Mwenyezi Mungu juu yenu,”
alisisitiza kwamba; kuwasili Bibi Fatima Ma’suma (s.a.) katika mji wa Qum ni tukio la kihistoria na kistaarabu ambalo linaweza kuangaliwa katika mwendelezo wa Hijra ya Mtume Mtukufu Muhammad (s.a.w.w.) kwenda Madina na kuanzishwa jamii ya Kiislamu.
Aliendelea kusema: “Tukio hili linapaswa kutambuliwa kuwa ni neema ya Mwenyezi Mungu, na kuihifadhi na kuilinda athari yake pia ni wajibu; kwa sababu uwepo wa watu wenye nafasi ya Mwenyezi Mungu na kuanzishwa kwa vituo vya kidini na kielimu kunapatikana katika njia ya kutimia ahadi ya Mwenyezi Mungu ya kueneza dini na maarifa ya Tauhidi.”
Msimamizi wa Kituo Kitukufu cha Bibi wa Karama, akizungumzia ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, alisema: “Kuibuka kwa Mapinduzi ya Kiislamu chini ya uongozi wa Imam Khomeini (r.a.) ni miongoni mwa madhihirisho muhimu ya harakati ya kihistoria ya Uislamu katika zama hizi. Katika miongo kadhaa iliyopita, watu wameshuhudia matukio mbalimbali, vita, mashambulizi na changamoto nyingi katika njia ya harakati hii.”
Ayatullah Saeedi alisisitiza: “Pamoja na changamoto hizi, nusura za Mwenyezi Mungu pia zimeonekana katika kipindi chote cha miaka hii, na hata leo harakati ya mfumo wa Kiislamu inaendelea licha ya kuwepo kwa shinikizo na vitisho mbalimbali.”
Akizungumzia mabadiliko na matukio yanayoendelea katika eneo la Mashariki ya Kati, aliendelea kusema: “Makabiliano kati ya upande wa haki na batili yamekuwa na mifano mbalimbali katika historia, na leo pia kambi ya ubeberu inasimama dhidi ya harakati ya Kiislamu; kama tunavyoyaona ukweli wa makabiliano haya na madhara yake huko Ghaza, Lebanon, Iraq, Yemen na maeneo mengine duniani.”
Msimamizi wa Kituo Kitukufu cha Bibi Fatima Ma’suma (s.a.), akieleza kwamba kuanzishwa kwa harakati ya kielimu ya Qum kuna mizizi yake katika uwepo wa Bibi Fatima Ma’suma (s.a.), alisema: “Miaka mingi kabla ya kuzaliwa kwa Bibi wa Karama, tayari kulikuwa kumetolewa habari kuhusu uwepo wake huko Qum, na mji huu, kwa sababu ya uwepo wake, ukawa miongoni mwa vituo muhimu zaidi vya elimu na fadhila.”
Akirejea riwaya kutoka kwa Ahlulbayt (as) kuhusu nafasi ya Qum, aliongeza: “Qum imetajwa katika riwaya kuwa ni mji ambao elimu na maarifa ya Ahlulbayt (as) vitaenea kutoka hapo hadi maeneo mbalimbali duniani. Hawza ya Kielimu ya Qum nayo imejengwa na kuendelea kukua katika mwendelezo wa uwezo huu wa kihistoria na kiroho.”
Ayatullah Saeedi pia alirejea riwaya ya Imam Musa Kadhim (as) kuhusu kuibuka kwa mtu kutoka Qum, akieleza: “Katika riwaya hiyo ametajwa mtu ambaye atawaita watu kuelekea kwenye haki, na kundi lenye msimamo thabiti na upinzani litaundwa kumzunguka; kundi ambalo halitarudi nyuma kutoka katika njia yake mbele ya matatizo na shinikizo kutoka kwa maadui.”
Msimamizi wa Kituo Kitukufu cha Bibi wa Karama, huku akisisitiza nafasi ya watumishi wa Haram Tukufu, alieleza: “Kuhudumu katika Kituo hiki Kitukufu si cheo au jina tu, bali ni jukumu kwa waumini na mahujaji wanaozuru, kwa ajili ya maarifa ya Ahlulbayt (as), pamoja na urithi wa kielimu na kiroho wa Qum. Watumishi wanapaswa kulitekeleza jukumu hili kwa njia ya kuwahudumia kwa ikhlasi wale wanaozuru na kulinda nafasi ya Haram Tukufu.”
Ayatullah Saeedi, mwishoni mwa hotuba yake, alieleza kwamba; kuwasili Bibi Fatima Ma’suma (s.a.) ndani ya Qum ilikuwa chimbuko la kuanzishwa kwa harakati ya kielimu, kiroho na kistaarabu ambayo, kupitia kuenea kwa maarifa ya Ahlulbayt (as) na kuanzishwa Hawza ya Kielimu ya Qum, imeendelea kupanuka kutoka mji huo hadi maeneo mbalimbali duniani.
Maoni yako