Kwa mujibu wa shirika la habari la hawza, katika khutuba yake, Sheikh Abdurazak Amiri, alianza kwa kusoma sehemu ya aya ya Qur’ani Tukufu inayosema:
{يَا أَيُّهَا النَّاسُ إِنَّا خَلَقْنَاكُم مِّن ذَكَرٍ وَأُنثَىٰ وَجَعَلْنَاكُمْ شُعُوبًا وَقَبَائِلَ لِتَعَارَفُوا}.
"Enyi watu! Hakika Sisi tumekuumbeni kutokana na mwanamume na mwanamke. Na tumekujaalieni kuwa ni mataifa na makabila ili mjuane".
(Alhujrat: 13)
Akifafanua ujumbe wa aya hiyo, Mkurugenzi wa Madrasa ya Ahlulbayt jiji Arusha alisema: Miongoni mwa mambo muhimu yanayosisitizwa ni umuhimu wa watu kufahamiana na kujenga uelewa wa pamoja.
Amesema migogoro mingi katika jamii hutokana na watu kutofahamiana ipasavyo, jambo ambalo husababisha mtu kumhukumu mwingine kwa msingi wa dhana, taarifa zisizo sahihi au mtazamo wa upande mmoja. Kwa hiyo, amesisitiza kuwa kufahamiana ni msingi muhimu wa kujenga mahusiano yenye amani na mshikamano.
Akitoa mfano kutoka katika maisha ya kila siku, Sheikh Abdu Razak amesema: Hata katika maisha ya ndoa, wakati mwingine mume na mke huingia katika mifarakano kwa sababu ya kutofahamiana. Amesema hali hiyo inaonesha wazi umuhimu wa watu kuelewana, kusikilizana na kufahamu mitazamo ya wenzao kabla ya kufikia hitimisho au kuchukua hatua zinazoweza kuvunja mahusiano.
Kwa mujibu wa Dk. Sheikh Abdurazak, ikiwa kufahamiana ni muhimu katika kudumisha uhusiano wa watu wawili katika ndoa, basi umuhimu wake unakuwa mkubwa zaidi katika jamii yenye watu wenye mitazamo, tamaduni na madhehebu mbalimbali.
“Mfahamu Mwrnzio Kwanza Kabla ya Kumuhukumu”
Katika kuhusisha suala hilo na tofauti za kidini na kimadhehebu, Dk. Abdurazak, amewataka Waislamu kutomkufurisha mtu au kundi kwanza kabla ya kufahamiana kwa kina. Amesema ni muhimu mtu anayemtazama mwenzake mwenye tofauti za kimadhehebu ajifunze kwanza mafundisho ya madhehebu hayo, ajue yanasemaje na afahamu ukweli pamoja na undani wa imani yake kabla ya kutoa hukumu.
Amesisitiza kuwa tofauti za kimadhehebu hazipaswi kuwa sababu ya kukata mahusiano baina ya Waislamu, bali zinapaswa kushughulikiwa kwa elimu, utafiti, mazungumzo na kuheshimiana. Kwa mtazamo wake, uelewa wa kweli unaweza kusaidia kupunguza dhana potofu na kuimarisha mshikamano miongoni mwa Waislamu.
“Watu Ni Maadui wa Wasiyoyajua”
Akihitimisha khutuba yake, Sheikh Abdurazak Amiri alirejea kauli maarufu isemayo:
«النَّاسُ أَعْدَاءٌ لِمَا جَهِلُوا»
“Watu Ni Maadui wa Wasiyoyajua”
Katika kufafanua maneno hayo alisema kuwa; mara nyingi watu huwa na uadui dhidi ya mambo ambayo hawajayafahamu. Kwa msingi huo, amesisitiza umuhimu wa Waislamu kusoma na kuchunguza vitabu na mafundisho ya madhehebu mbalimbali kabla ya kutoa hukumu dhidi yake.
Sheikh Amiri pia amesisitiza kanuni isemayo: «لا يُنكر المختلف فيه وإنما يُنكر المجمع عليه», huku akihitimisha kwa kusisitiza umuhimu wa kuheshimu maeneo yenye tofauti za kimtazamo na kuzingatia mambo yanayokubaliwa kwa pamoja. Amesema mtazamo huo unaweza kuwa njia muhimu ya kuimarisha umoja, kuheshimiana na kuondoa migawanyiko miongoni mwa Waislamu.
Maoni yako