Jumatatu 31 Agosti 2026 - 13:12
“Bila ya Mtume Muhammad (s.a.w.w.) Hakuna Amani Duniani”

Hawza/ Sheikh Maulidi Hussein Sombi, amesisitiza umuhimu wa kumuenzi Mtume Muhammad (s.a.w.w.) kwa kuzingatia mafundisho yake ya amani, umoja na mshikamano, huku akieleza kuwa Mtume Mtukufu ni msingi muhimu wa kuenea amani na rehema kwa wanadamu.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, akizungumza katika hafla ya matembezi ya zafa iliyofanyika jana jioni Kigogo Posti, Jijini Dar es Salaam, Sheikh Sombi alisema kuwa: Mtume ni rehema kwa waumini, hivyo maadhimisho ya Maulidi yanapaswa kuwa zaidi ya sherehe, bali iwe ni fursa ya kutafakari na kutekeleza mafundisho aliyoyaacha Mtume kwa umma wake.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Sayyid Shuhadaa alisema: Moja ya malengo makubwa ya Maulidi ni kuleta furaha katika nyoyo za watu, huku akirejea mafundisho ya Mtume Muhammad (s.a.w.w.) yanayosisitiza umuhimu wa kuingiza furaha katika nyoyo za waumini na kuwafanyia mema wengine.

Aidha, sheikh Maulid amesisitiza kuwa; mafundisho hayo ni miongoni mwa mafunzo ambayo Mwenyezi Mungu na Mtume wake wamewaachia waumini, huku akiwataka Waislamu kuyazingatia katika maisha yao ya kila siku kwa kudumisha umoja, amani na mshikamano katika jamii.

Akihitimisha ujumbe wake, Sheikh Sombi amewataka waumini kutumia maadhimisho ya kuzaliwa Mtume Muhammad (s.a.w.w.) kama fursa ya kuimarisha amani na mshikamano, huku akisisitiza kuwa hayo ni miongoni mwa mambo muhimu yaliyosisitizwa na Mtume Mtukufu kwa ajili ya kuijenga jamii yenye upendo na umoja.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha