Kwa mujibu wa Kitengo cha Kimataifa cha Shirika la Habari la Hawza, Sheikh Ibrahim Zakzaky alitoa kauli hiyo katika hafla ya kufunga mkutano wa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari za Mafunzo ya Kitaaluma ya Kiislamu (IVC) mjini Abuja. Mpango huo ulifanyika asubuhi ya Jumamosi, tarehe 22 Agosti, na uliandaliwa na Jumuiya ya Wanafunzi na Wasomi ya Harakati ya Kiislamu wakati wa likizo za shule.
Sheikh Zakzaky katika hotuba yake aliutaja mpango wa IVC kuwa ni fursa muhimu kwa malezi na maandalizi ya watoto na vijana, akieleza kwamba; lengo la mpango huo si kufundisha tu masomo ya shule, bali pia juhudi zinafanywa kurekebisha fikra na mitazamo ya wanafunzi ili waweze kufikiri kwa usahihi na kuijua na kuielewa dini kwa njia sahihi.
Akieleza umuhimu wa kuwajenga watoto kiakili, alisema: Akili ya mwanadamu inahitaji kuhuishwa na kuwekwa hai na yenye shughuli kupitia fikra sahihi na zenye kujenga; hivyo, wanafunzi wanapaswa kutumia kipindi cha ujana wao kujipatia elimu na kuimarisha uwezo wao wa kufikiri.
Kiongozi huyo wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria pia alisisitiza umuhimu wa nia katika kutafuta elimu, na kuwataka wanafunzi kujifunza elimu kwa ajili ya kutafuta radhi za Mwenyezi Mungu na kwa lengo la kuitumikia jamii.
Alisisitiza kwamba: Kila elimu ambayo ina manufaa kwa mwanadamu duniani na Akhera, na ambayo pia ina manufaa kwa jamii, ikiwa itatafutwa kwa nia ya Mwenyezi Mungu, huhesabiwa kuwa ni ibada. Aliitaja elimu ya tiba na afya, kilimo, sayansi, usafirishaji na taaluma nyingine zenye manufaa kuwa miongoni mwa elimu hizo.
Sheikh Zakzaky aliendelea kusema kwamba; elimu ni miongoni mwa sababu za maendeleo ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na nguvu ya nchi hiyo katika mazingira ya sasa, akielezea kwamba elimu imekuwa na nafasi muhimu katika kuimarisha uwezo na msimamo wa Iran wa kukabiliana na changamoto zilizopo.
Mwisho, Sheikh Zakzaky aliwataka wanafunzi kuongeza juhudi katika kujifunza elimu yenye manufaa kwao wenyewe na kwa jamii, na akasisitiza umuhimu wa kutumia elimu katika kutafuta suluhisho kwa matatizo na mahitaji ya jamii.
Maoni yako