Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, katika sherehe hizo, Mufti wa Tanzania na Sheikh Mkuu wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) Sheikh Abuubakr bin Zubeir, amesisitiza umuhimu wa Waislamu na Watanzania kwa ujumla kudumisha umoja na amani, akieleza kuwa mshikamano na kuheshimiana ni misingi muhimu katika kujenga taifa lenye utulivu na maendeleo endelevu.
Mufti amewataka waumini kutumia maadhimisho ya Maulidi kama fursa ya kutafakari kwa kina mwenendo na mafundisho ya Mtume Muhammad (s.a.w.w), hususan katika masuala ya upendo, kuvumiliana, kusameheana, kusaidiana na kuishi kwa amani na watu wa imani na makundi mbalimbali.
Amesema kuwa Tanzania inapaswa kuendelea kuulinda umoja na amani iliyopo, huku akisisitiza kwamba tofauti za kidini, kimtazamo au kijamii hazipaswi kuwa sababu ya kuvuruga mshikamano wa wananchi. Badala yake, Watanzania wanapaswa kuheshimiana na kushirikiana katika kulijenga taifa lao kwa misingi ya amani, maadili mema na utu.
Sherehe hizo za Maulidi ya Kitaifa katika Viwanja vya Mnazi Mmoja zimekuwa sehemu muhimu ya kuwakutanisha Waislamu na viongozi mbalimbali katika kuenzi maisha na mafundisho ya Mtume Muhammad (s.a.w.w). Ujumbe wa kudumisha umoja, amani, upendo na mshikamano umetawala katika hafla hiyo, huku waumini wakihimizwa kuyafanya mafundisho hayo kuwa sehemu ya maisha yao ya kila siku kwa ajili ya kuijenga jamii yenye utulivu na Tanzania yenye amani zaidi.



Maoni yako