Kwa mujibu wa Kitengo cha tarjuma cha Shirika la Habari la Hawza, Sheikh Adel Al-Shu'la, mmoja wa wanazuoni wa Kishia nchini Bahrain, alitoa wito wa kuwa na kiwango cha juu kabisa cha uangalifu na tahadhari dhidi ya kile alichokielezea kuwa “utawala fisadi”, huku akisisitiza kwamba: Ufisadi wa serikali unaongeza mambo mapya katika changamoto ambazo mwanadamu hukabiliana nazo katika kushikamana na dini yake, itikadi yake, maadili yake na maslahi yake.
Sheikh Al-Shu'la alisema kwamba; pale madaraka yanapokuwa fisadi, hayafikirii jambo lolote isipokuwa maslahi yake yenyewe. Alisisitiza: “Watu wenye tabia za kishetani” hujiunga na mfumo wa ufisadi katika mazingira kama hayo, jambo ambalo linatishia imani, maadili na maslahi ya wananchi.
Akieleza kwamba haya siyo tu hofu ya kinadharia, bali ni ukweli halisi ambao watu husikia, huona na kuupitia kila siku, alisisitiza kwamba: Dalili za ufisadi huenea katika nyanja mbalimbali za maisha, zikiwemo kwa kiwango cha juu elimu na malezi, uchumi, ajira, usalama na mahakama.
Aidha, alitoa tahadhari kwamba; vitabu na mitaala ya elimu vinaweza kuathiri “fiqhi, itikadi, fikra na utamaduni safi” wa mwanadamu, akirejelea kile alichokiita “operesheni ya kuingiza maudhui ya kielimu kwa jina la kuhalalisha uhusiano na utawala wa Kizayuni unaotawala kwa mabavu.”
Ukosefu wa Ajira, Madeni na Madhara ya Hali ya Kiuchumi
Katika uwanja wa uchumi, Sheikh A'dil alieleza kuhusu kuongezeka kwa ukosefu wa ajira—hususan ukosefu wa ajira unaohusiana na taaluma maalumu—pamoja na ongezeko la madeni ambayo nchi inahangaika nayo, akiona hali hiyo kuwa ni ishara ya “kushindwa kusimamia rasilimali kwa uwajibikaji.”
Mwanazuoni huyo wa Bahrain alieleza upinzani wake dhidi ya matumizi ya utajiri wa nchi kwa ajili ya kujenga vituo vya kijeshi vya Marekani, akisema: Anatumaini kwamba “ujenzi mpya wa vituo vya Marekani kwa kutumia utajiri wa” taifa hautafanyika.
Alirejelea matumizi ya mamilioni ya fedha kutoka katika uwezo na utajiri wa nchi kwa ajili ya kujenga vituo hivyo na kuvipatia uwezo unaohitajika.
Sheikh Al-Shu'la aliunganisha sera hizo na kile alichokielezea kuwa ni nafasi ya vituo hivyo katika “kuiunga mkono serikali ya Kizayuni na kuunga mkono ubeberu wa kimataifa.” Pia alizikosoa sera za ajira, akizielezea kuwa zinaua taaluma, kwa sababu wahitimu huajiriwa katika fani tofauti na taaluma zao maalumu, jambo linalosababisha kuendelea kwa ukosefu wa ajira miongoni mwa maelfu ya vijana na wahitimu wa vyuo vikuu.
Wakati huo huo, Sheikh Al-Shu'la alitoa tahadhari kwamba; hali ngumu ya maisha inaweza kuwafanya baadhi ya watu kuelekea katika kazi ambazo yeye amezielezea kuwa ni haramu (zilizokatazwa); miongoni mwa kazi hizo ni ajira katika shughuli za riba, au kazi ambazo, kwa mujibu wa maelezo yake, zinahusisha kuvunjwa kwa heshima na hadhi ya watu.
Ukosoaji Kuhusu Usalama na Mahakama
Akizungumzia masuala ya usalama na mahakama, Sheikh huyo alisema kwamba; katika kipindi cha miaka ya uasi na maandamano ya mara kwa mara, makumi ya maelfu ya watu walipelekwa magerezani. Alisisitiza kwamba familia za waliokamatwa zimepitia hofu, wasiwasi, mateso na ukiukwaji wa haki, huku maelfu yao wakiteswa.
Alirejelea kuuwawa baadhi ya waliokamatwa na kusema: “Hata wale waliofariki ni mashahidi ambao tunawahesabu kuwa wako kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu.”
Sheikh Al-Shu'la alivitaja vyombo vya usalama na mahakama kuwa ni “vya kifashisti,” akivishutumu kwa kutumia ukandamizaji ili kunyamazisha sauti zinazodai haki zao, pamoja na kutumia mateso, vitisho na udhalilishaji.
Kuhukumiwa Wanazuoni
Sheikh A'dil alikosoa kile alichokielezea kuwa ni juhudi za “kuficha uhalifu na dhulma ya serikali,” na akasema kwamba; kuhukumiwa kwa wanazuoni ndani ya siku hizi katika nyanja za usalama na mahakama ni “ushahidi wa wazi kabisa wa dhulma na uasi wa kiusalama na kimahakama.”
Tahadhari Kuhusu “Idara ya Wakfu wa Jaafari”
Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Sheikh huyo alitoa tahadhari kuhusu “Idara ya Wakfu wa Jaafari,” na kutoa wito wa kuwa waangalifu dhidi ya kutendeka uhalifu dhidi ya Mashia.
Sheikh Al-Shu'la, mwishoni mwa hotuba yake, aliwapongeza wafungwa waliokuwa wameachiwa huru, huku akichukulia kuachiwa kwao kuwa ni maana kwamba Mwenyezi Mungu “amewaokoa kutoka katika dhulma na giza la magereza ya Khalifa.” Pia alizipongeza familia zao na kumuomba Mwenyezi Mungu awaandikie katika daftari la matendo yao hali ya kudhulumiwa waliyopitia, na awawezeshe kupata faraja na ukombozi kwa wafungwa wengine waliobaki.
Maoni yako