Jumatano 26 Agosti 2026 - 00:55
Maelfu ya Waumini Indonesia Waswali Swala ya Kuomba Mvua Ili Kukabiliana na Moto Mkubwa Unaoendelea

Hawzah/ Maafisa wa Mkoa wa Sumatra Kusini nchini Indonesia, wakati moto mkubwa sana ukiendelea kuteketeza misitu na maeneo oevu ya mkoa huo na kusababisha ukungu mzito katika baadhi ya maeneo ya nchi hiyo, waliswali Sala ya Kuomba Mvua.

Kwa mujibu wa kitengo cha tarjama cha Shirika la Habari la Hawza, kufuatia moto mkubwa uliotokea katika maeneo ya kusini, maafisa wa Sumatra Kusini nchini Indonesia, mkoa ambao ulikuwa na idadi kubwa zaidi ya maeneo yenye vyanzo vya moto misituni, waliswali Swala ya Kuomba Mvua.

Ukubwa wa moto huo umefikia kiwango ambacho kuudhibiti kumekuwa nje ya uwezo wa nguvu kazi za binadamu. Jumanne, wananchi walikusanyika ili kuswali Swala ya Kuomba Mvua na kumuomba Mwenyezi Mungu msaada, kwa sababu moto mkubwa katika maeneo ya kati na magharibi umeteketeza maeneo makubwa ya misitu na ardhi oevu na kusababisha moshi hatari ambao umeenea katika baadhi ya miji yenye wakazi wengi nchini humo, ambayo ina sehemu kubwa ya Waislamu duniani.

Mkusanyiko mkubwa wa kuswali Swala ya Kuomba Mvua umefanyika wakati nchi hiyo ikikabiliwa na hali ya hewa kavu katika kipindi kirefu cha ukame, jambo ambalo limeongeza hatari ya kutokea kwa moto katika misitu na maeneo oevu.

Takwimu za hivi karibuni za satelaiti kutoka Wizara ya Mazingira ya Indonesia zinaonyesha kwamba Sumatra Kusini ikiwa na maeneo 1,429 yaliyoathiriwa na moto, ndiyo iliyorekodi idadi kubwa zaidi ya maeneo hatarishi nchini kote. Ikifuatiwa na Kalimantan Magharibi yenye maeneo 1,226 na Kalimantan ya Kati yenye maeneo 811. Takwimu za Wizara ya Misitu zinaonesha kwamba katika mwezi wa Julai pekee, karibu kilomita za mraba 940 (maili za mraba 363) zimeteketea kwa moto, ikiwemo zaidi ya kilomita za mraba 20 (maili za mraba 8) katika Mkoa wa Sumatra Kusini.

Takribani wakazi 3,000 katika jiji la Palembang, mji mkuu wa Mkoa wa Sumatra Kusini, walikusanyika kwa ajili ya kuswali Swala ya Kuomba Mvua. Walijipanga bega kwa bega katika ua wa Ofisi ya Gavana wa mkoa huo na kuswali Swala ya Kuomba Mvua, huku moshi mzito ukiwa umefunika barabara, majengo na miundombinu ya umma na kupunguza kwa kiasi kikubwa uoni.

Herman Deru, Gavana wa Sumatra Kusini, alisema kabla ya swala hiyo: “Tumefanya kila tulichoweza kufanya na tumekuwa tukishirikiana kwa karibu na pande zote zinazohusika.” Aliongeza: “Sisi kama watu wenye imani, tunamuomba Mwenyezi Mungu atuletee mvua ili maisha yarudi katika hali ya kawaida.”

Chanzo: ABC News

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha