Jumatatu 27 Julai 2026 - 07:30
Wananchi wa Bahrain wabebe jukumu la kumsimamisha mtawala wa Bahrain!

Hawza/ Muungano wa Vijana wa Mapinduzi ya Februari 14 nchini Bahrain umeionya tena serikali ya Aal Khalifa kwamba; kuendelea kutegemea nguvu za uvamizi na uharibifu zinazoongozwa na watu wanaowataja kuwa wahalifu kama Donald Trump na Benjamin Netanyahu kutaleta madhara makubwa kwa nchi na wananchi wake.

Kwa mujibu wa Kitengo cha tarjama cha Shirika la Habari la Hawza, Baraza la Kisiasa la Muungano wa Vijana wa Mapinduzi ya Februari 14 nchini Bahrain limeionya tena serikali ya Aal Khalifa kwamba kuendelea kutegemea nguvu za uvamizi na uharibifu zinazoongozwa na watu wanaowataja kuwa wahalifu kama Donald Trump na Benjamin Netanyahu, kutakuwa na matokeo mabaya yatakayodhuru nchi na wananchi wake.

Katika taarifa yake ya kila wiki iliyochapishwa kupitia tovuti ya muungano huo, baraza hilo lilisema: Baada ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kutumia haki yake halali ya kisheria kujibu mashambulizi ya Marekani ambayo wameyaita ya kihalifu, onyo letu linatokana na msimamo wa msingi wa vyama vya mapinduzi na makundi yote ya jamii nchini Bahrain. Msimamo huo unasisitiza kwamba; utegemezi wa utawala wa Aal Khalifa kwa mihimili ya kikoloni ya kigeni na kuigeuza nchi kuwa makao makuu ya mbele ya Kikosi cha Tano cha Wanamaji wa Marekani, hautailetea serikali hiyo ulinzi wowote, bali utaongeza azma ya wananchi ya kujikomboa kutoka chini ya utawala huo.

Taarifa hiyo iliendelea kusema kwamba; wananchi hawataacha haki yao ya kulipiza kisasi kwa njia ya haki dhidi ya viongozi wa Aal Khalifa wanaowatuhumu kwa uhalifu, pia ilisema kuwa kuendelea kwa utawala huo kufungua anga na ardhi ya Bahrain kwa mashambulizi ya kile ilichokiita "Marekani–Uzayuni" dhidi ya Iran, kunamaanisha kuwazamisha zaidi wananchi katika moto wa vita vya kikanda vinavyotumikia tu mipango ya Marekani na Wazayuni, licha ya madhara makubwa ya kiuchumi na kifedha yatakayofuata.

Baraza hilo, likiwahutubia wananchi wa Bahrain, liliwataka kubeba jukumu lao la kitaifa, kisheria na kimaadili, na kuchukua msimamo sahihi wa kihistoria kwa kusimama dhidi ya mtawala wanayemtaja kuwa dikteta, Hamad, na kuzuia kile walichokiita wazimu wake wa kuiangamiza nchi.

Baraza hilo lilisisitiza kuwa; mamlaka na uhuru wa taifa haviendani na uwepo wa kambi za kijeshi za kigeni zinazoshiriki katika vita dhidi ya nchi jirani na kuwaua Waislamu, liliongeza kuwa; kunyamaza mbele ya hali hiyo hakutamlinda yeyote, bali kutasababisha madhara na matokeo mabaya. Aidha, lilisema kuwa kulegeza msimamo na kutokuchukua hatua madhubuti dhidi ya kuhalalishwa kwa uhusiano kati ya utawala wa Aal Khalifa na Wazayuni kumeiwezesha serikali hiyo kujiunga zaidi na mhimili wa Kizayuni pamoja na miradi yake ya kihalifu katika eneo na duniani.

Taarifa hiyo iliendelea kusema kwamba, chini ya kivuli cha kile ilichokiita "mashambulizi ya Marekani–Uzayuni" dhidi ya Iran, utawala wa Aal Khalifa unajaribu kwa makusudi kutekeleza sura nyingine za mpango wake mweusi wa kulipiza kisasi dhidi ya wananchi wa Bahrain na kupambana na uwepo pamoja na utambulisho wao, huku ukivuka mipaka yote ya maadili na sheria. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, ripoti zilizoandikwa kuhusu ukiukwaji wa haki za maulamaa waliowekwa gerezani zinaonesha kuporomoka kwa maadili kwa mtawala Hamad, Waziri wa Mambo ya Ndani Rashid, na wafuasi wao, kwa kuwa hawazingatii kabisa misingi ya kibinadamu, hasa kutokana na nafasi ya kidini na kitaifa ya maulamaa hao ambao ni viongozi wa kiroho na kihistoria wa wengi wa wananchi.

Baraza hilo pia lilionya kuwa; kuendelea kuwashambulia maulamaa na kuwafanyia madhara ya kisaikolojia, kimwili, kuwafungulia mashitaka na kuwavunjia heshima maulamaa waliowekwa gerezani ni tangazo la vita jipya dhidi ya wananchi, dini yao na utambulisho wao wa asili. Hata hivyo, lilisema kuwa hatua hizo hazitawafanya wananchi washindwe au kujisalimisha, bali zitawaongezea mshikamano katika itikadi yao, utambulisho wao na ufuasi wao kwa maulamaa wapambanaji.

Taarifa hiyo iliongeza kuwa; wananchi hawatarudi nyuma katika msimamo wao wa kuikataa serikali ya Aal Khalifa na wataendelea kushikamana na kaulimbiu na mradi wao wa kuiangusha serikali hiyo wanayoitaja kuwa fisadi na kujinasua kutoka katika uovu wake.

Mwishoni, taarifa hiyo ilisisitiza kuwa; kuendelea kwa vita vinavyoendeshwa na mtawala Hamad dhidi ya kile walichokiita uwepo wa asili nchini Bahrain (Mashia), na juhudi za kukausha misingi yake kupitia kuwazuia wafuasi wa madhehebu ya Ahlul-Bayt (as) kushiriki katika Ziara ya Arubaini, kuweka vikwazo na kueneza hofu miongoni mwa wananchi ili wasijiunge na misafara ya mazuwari, ni hatua za kulipiza kisasi zinazoonesha kiburi na kupindukia kwa utawala huo. Taarifa hiyo ilieleza kuwa; hatua hizo ni sehemu ya mpango mpana unaolenga kuuzingira na kuupiga vita utambulisho wa wananchi wengi wa Bahrain kwa kila njia, jambo ambalo Ayatullah Sheikh Issa Qassim amelielezea kuwa ni "tishio kubwa la uwepo."

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha