Ijumaa 7 Agosti 2026 - 13:50
Maridhiano kati ya Syria na Hizbullah ni hatua yenye baraka katika njia ya umoja wa Umma wa Kiislamu.

Hawza/ Mratibu Mkuu wa Mhimili wa Harakati ya Kiislamu nchini Lebanon, huku akirejea Aya Tukufu isemayo: «وَاعْتَصِمُوا بِحَبْلِ اللَّهِ جَمِيعًا وَلَا تَفَرَّقُوا», ameashiria dalili za kukaribiana kati ya Syria na Hizbullah.

Kwa mujibu wa ripoti ya Kitengo cha tarjama cha Shirika la Habari la Hawza, Sheikh Zuhair Al-Juaid, Mratibu Mkuu wa Mhimili wa Harakati ya Kiislamu nchini Lebanon, akirejea Aya Tukufu isemayo:

«وَاعْتَصِمُوا بِحَبْلِ اللَّهِ جَمِيعًا وَلَا تَفَرَّقُوا»

Shikamaneni nyote katika Kamba ya Mwenyezi Mungu wala msifarikiane, ameashiria dalili za kukaribiana kati ya Jamhuri ya Kiarabu ya Syria na Hizbullah.

Katika taarifa yake alisema: Mabadiliko ambayo eneo letu linayashuhudia chini ya mwendelezo wa mashambulizi ya utawala wa Kizayuni dhidi ya Palestina, Lebanon na Syria, pamoja na malengo ya upanuzi mradi wa Israel unaolenga usalama na utulivu wa eneo hili, yanazilazimu nguvu zote za kitaifa, Kiislamu na za kijamii kupandisha kiwango cha wajibu wao wa kihistoria. Nguvu hizo zinapaswa kufanya mazungumzo, mshikamano na ushirikiano kuwa chaguo la kimkakati linalouimarisha Umma na kuziba njia mbele ya miradi ya mgawanyiko na utawala wa mabavu.

Sheikh Al-Juaid aliongeza: Kutokana na mtazamo huo, tunazitazama kwa furaha na kuthamini ishara chanya zilizojitokeza katika siku za hivi karibuni; ishara zinazoakisi nia ya pande zote mbili ya kufunga ukurasa wa tofauti na kufungua upeo mpya wa mawasiliano kati ya Syria na Hizbullah. Misimamo iliyotangazwa na Rais wa Syria Ahmad Al-Sharaa, pamoja na msisitizo wa Waziri wa Mambo ya Nje Ahmad Al-Shaibani wakati wa ziara yake ya kukutana na Spika wa Bunge Nabih Berri, kwamba serikali ya Syria iko tayari kufanya mazungumzo na Hizbullah pale maslahi ya taifa yatakapohitaji, imeweka msingi wa mazingira chanya na yenye kuwajibika. Kisha hatua ya Sheikh Naim Qassem aliyoitangaza katika hotuba yake kwenye hafla ya Arubaini ya Imam Hussein (as), ya kuonesha utayari wa kukutana na uongozi mpya wa Syria na kufungua ukurasa mpya wa mahusiano, ni uthibitisho wa kuwepo kwa dhamira ya kweli inayostahili kuungwa mkono na kutiwa moyo.

Sheikh Al-Juaid aliendelea kusema: Sisi ndani ya Harakati ya Kiislamu nchini Lebanon tunaukaribisha moyo huu wa kuwajibika na tunauona kuwa ni hatua yenye baraka katika njia sahihi; kwa sababu mazungumzo kati ya wana wa Umma, bila kujali ukubwa wa tofauti zao, ni bora kuliko kuendelea kutengana, na maelewano ni bora kuliko uadui. Ushirikiano katika kukabiliana na hatari za pamoja una kipaumbele zaidi kuliko kupoteza uwezo wa nguvu katika migogoro ya ndani.

Aliongeza kuwa; uzoefu umethibitisha kwamba wanufaika wa kwanza wa mpasuko wowote wa Kiarabu au Kiislamu ni wavamizi wa Kizayuni, ambao wanaendelea na mashambulizi yao dhidi ya Ghaza, Ukingo wa Magharibi, kusini mwa Lebanon na ardhi za Syria, huku wakitumia kila udhaifu au mgawanyiko kupanua ushawishi wao na kulazimisha uhalisia mpya ardhini. Aidha, kauli za mara kwa mara za viongozi wa Israel zinazoonesha sera za upanuzi na tamaa za kikanda zinahitaji umakini na mshikamano mkubwa zaidi kati ya mataifa ya eneo hili na nguvu zake hai.

Kiongozi huyo mwandamizi wa Harakati ya Kiislamu alitoa wito wa kunufaika na mazingira haya chanya na kutoruhusu upande wowote kuyavuruga au kurudisha mambo nyuma. Alisisitiza kwamba hatua ya sasa inahitaji mazungumzo ya kina, sera yenye hekima na dhamira ya kweli inayotanguliza maslahi ya Umma mbele ya maslahi ya kimadhehebu na ya muda mfupi.

Alifafanua kuwa; Syria yenye nguvu na utulivu, pamoja na Lebanon iliyo salama na yenye umoja, sambamba na Palestina, vinaunda ngome ya kimkakati dhidi ya wavamizi, na kuimarisha madaraja ya kuaminiana na ushirikiano kati ya wote wenye ikhlasi katika medani hizi ni wajibu wa kitaifa, wa kijamii na wa Kiislamu usiokubali kucheleweshwa.

Sheikh Zuhair Al-Juaid alisema: Mtazamo wetu wa kisheria na kisiasa katika Harakati ya Kiislamu daima umejengwa juu ya kuunganisha nyoyo, kupatanisha waliokosana, kujiepusha na fitna na kujenga madaraja ya mazungumzo kati ya sehemu zote za jamii, kwa mujibu wa kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu:

«إِنَّمَا الْمُؤْمِنُونَ إِخْوَةٌ فَأَصْلِحُوا بَيْنَ أَخَوَيْكُمْ»

Hakika Waumini ni ndugu, basi patanisheni baina ya ndugu zenu.

Tunaamini kwamba umoja wa Umma si chaguo la kisiasa pekee, bali ni wajibu wa kisheria na ulazima wa ustaarabu katika kukabiliana na hatari zinazoizunguka.

Mwishoni alisisitiz kuwa: Tunamuomba Mwenyezi Mungu Mtukufu aziunganishe nyoyo na awajaalie wote mafanikio katika yale yenye kheri kwa Lebanon, Syria, Palestina na Umma wetu. Tunatumaini kuwa juhudi hizi zitakuwa mwanzo wa hatua mpya ambayo ndani yake ushirikiano na maelewano vitatawala, na uwezo wote utaelekezwa katika kupambana na wavamizi, kutetea ardhi, kuhifadhi heshima na kutimiza maslahi ya mataifa yetu.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha