Kwa mujibu wa ripoti ya Kitengo cha tarjama cha Shirika la Habari la Hawza, Harakati ya Amal kwa mnasaba wa Arubaini ya Imam Hussein (as) na siku ya tatu ya shahada ya Hussein Yasin Ibrahim, iliandaa hafla kubwa katika Husseiniyya ya mji wa Toulin.
Katika hafla hiyo alihudhuria msimamizi mkuu wa masuala ya utamaduni na Mufti wa Sur na Jabal Amil, Qadhi Hujjatul-Islam Sheikh Hassan Abdullah, msimamizi wa miundo ya eneo la tano, viongozi na makada mbalimbali wa harakati hiyo pamoja na vijana wa skauti, mkurugenzi wa Hospitali ya Serikali ya Tebnin Dkt. Muhammad Hammadi, wenyeviti na wajumbe wa mabaraza ya miji na vijiji, shakhsia za kisiasa, vyama, kijamii, kielimu na kitabibu, pamoja na kundi la wakazi wa mji huo na maeneo ya jirani.
Hotuba ya Sheikh Hassan Abdullah
Baada ya kundi la Shahidi Abdullah Awaleh kutoka kwa Skauti wa Risalatul-Islamiyya kuwasilisha nyimbo za kiroho, na programu kutambulishwa na Hussein Hassan Awaleh, msomaji wa kimataifa wa Qur’ani Hussein Ghanem alisoma aya za Qur’ani Tukufu. Kisha Sheikh Hassan Abdullah, kwa niaba ya Harakati ya Amal, alianza hotuba yake kwa kupitia historia ya “njia ya haki katika kukabiliana na batili na kujitolea kwa kutoa nafsi na mali kwa ajili ya kuhifadhi dini na ujumbe halisi wa Muhammadi.”
Alirejea mateso yote, mzingiro na mauaji ambayo Mtume Mtukufu Muhammad (saww) na Ahlul-Bayt wake watoharifu walikumbana nayo, na akaongeza: Njia hii iliendelea hadi zama za Imam Hussein (as). Yazid na wafuasi wake walidhani kwamba wameishinda njia na mwenendo wa Hussein, lakini pale muadhini katika baraza la Yazid alipotamka jina la Mtume Muhammad (saww), walipatwa na mshangao na simulizi lao likaanguka. Imam Zainul-Abidin (as) alimwuliza Yazid: Je, Muhammad (saww) ni babu yangu au babu yako? Ukisema ni babu yako, umesema uongo na umetenda dhambi; na ukisema ni babu yangu, basi kwa nini ulimuua baba yangu Hussein? Kisha Bibi Zainab Kubra (sa) kwa maneno yake yenye nguvu alitikisa kiti cha Yazid na akasema: Fanya hila yoyote unayoweza na tumia juhudi zako zote, lakini kwa Mwenyezi Mungu hutafuta kumbukumbu yetu wala hutauua ufunuo wetu, hivyo basi, njia hii ya Muhammadi-Husseini iliasisiwa na kuendelea hadi leo kwa ajili ya kupambana na dhulma na kuisaidia haki na mwenye kudhulumiwa.
Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Sheikh Abdullah alizungumzia hali ya kisiasa na ya ndani ya Lebanon na kusisitiza usahihi wa njia na fikra za Imam Musa Sadr katika kuhifadhi umoja wa kitaifa.
Alisema: Hiki ndicho ambacho Spika wa Bunge la Lebanon Nabih Berri anakitumikia ili Lebanon iendelee kubaki kuwa taifa la mwisho kwa watoto wake wote. Tunapaswa kutumia uwezo wote wa kitaifa kuilinda nchi dhidi ya changamoto, na sisi sote, Wakristo na Waislamu, tuishi katika taifa moja linalotawaliwa na uadilifu wa kijamii na tuwe sawa katika haki na wajibu.
Alibainisha kuwa; baadhi ya mihimili ya dola inahalalisha mashambulizi na kiburi cha adui Muisraeli; adui ambaye anaua, anajeruhi, anawafukuza makwao na kuwatesa baadhi ya Walebenon kwa sababu ya kuhusishwa na jiografia fulani au dhehebu maalumu.
Sheikh Hassan Abdullah, kwa niaba ya Rais wa Harakati ya Amal, Nabih Berri, uongozi wa harakati hiyo na wapiganaji wake, alitoa salamu za rambirambi kwa familia za mashahidi wawili, Ali na Hussein Yasin Ibrahim.
Mwishoni aliongeza kuwa; ingekuwa vyema zaidi kama viongozi tawala wangechukua hatua ya kwanza kulaani jinai hii na nyingine zinazofanana nayo ambazo zimetendeka hadharani mchana kweupe.
Pia alizitakia familia za mashahidi subira na kusisitiza kwamba; damu yao haitapotea bure, na kwamba njia ya haki bila shaka itashinda, hata kama itachukua muda.
Hafla hiyo ilihitimishwa kwa kisomo cha maombolezo ya Imam Hussein (as) kilichoongozwa na Sheikh Mustafa Shakrun. Aidha, ujumbe wa Mudhif Abul-Fadhl Al-Abbas (as), familia za mashahidi hao wawili, kikosi cha ulinzi wa kiraia cha Risali mjini Toulin pamoja na wahisani, kwa mapenzi ya Imam Hussein (as) na Ahlul-Bayt wake watoharifu, waliandaa karamu ya chakula kwa washiriki.
Maoni yako