Jumatano 22 Julai 2026 - 08:55
Hatutafanya Makubaliano kwa Damu ya Mashahidi Wetu na Tumnataka Adui Aondoke Kikamilifu katika Ardhi Yetu

Hawza/ Makamu Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Kiislamu la Mashia nchini Lebanon amesisitiza: Hatukubali aina yoyote ya mapatano yanayohusu damu ya mashahidi wetu, na tunataka adui wa Kizayuni aondoke kikamilifu katika ardhi yetu, wananchi wetu warejee kwa heshima katika miji, vijiji na nyumba zao.

Kwa mujibu wa Kitengo cha tarjama cha Shirika la Habari la Hawza, Sheikh Ali Al-Khatib, Makamu Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Kiislamu la Mashia nchini Lebanon, amesema: "Tunakataa aina yoyote ya mapatano yanayohusu damu ya mashahidi wetu, iwe ni wapiganaji wa Muqawama au raia wa kawaida. Tunataka adui wa Kizayuni aondoke kikamilifu katika ardhi yetu, wananchi wetu warejee kwa heshima katika miji, vijiji na nyumba zao, ujenzi wa maeneo yaliyoharibiwa uanze, na wafungwa wa Lebanon waachiliwe kutoka katika magereza ya Israel. Baada ya mambo hayo kutekelezwa, ndipo mazungumzo kuhusu mkakati wa kitaifa wa ulinzi yataanza, kwa lengo la kuwa na jeshi lenye uwezo wa kuwalinda wananchi wetu, kuilinda ardhi yetu na kuhakikisha mamlaka kamili ya taifa."

Sheikh Al-Khatib alisema kuwa; historia ya maadui imejaa mifano ya aibu, ikiwemo kuwaua wafungwa, kufanya mauaji ya halaiki dhidi ya raia wasio na ulinzi na kuvunja ahadi walizotoa. Aliongeza kuwa; mwenendo wa Marekani katika kufanya mashambulizi, mauaji na uharibifu dhidi ya wananchi wasio na hatia ni mfano bora wa tabia hiyo.

Alisema kuwa; kipimo chao ni "nguvu", na lengo lao ni "kupora utajiri wa mataifa na kuyadhoofisha." Kwa mujibu wake, hakuna sheria ya kimataifa, mkataba, haki za binadamu wala uadilifu wa kimataifa unaowazuia. Aidha, alisema wanajivunia kwa kiburi vitendo vyao, hawana chochote kinachowazuia, wanahalalisha umwagaji damu na kuharibu maisha ya watu.

Aliongeza: "Kinachosikitisha ni kwamba, baada ya yote haya, bado tunawaona watu wanaohalalisha uhalifu huu, wanaousaidia na hata kuwahamasisha wahusika kuendelea kufanya uhalifu zaidi. Watu hao ni raia wenzetu ambao, kwa madai yao ya kulinda mamlaka ya taifa, walipaswa kusimama kuitetea ardhi na nchi yao dhidi ya wavamizi wauaji, na tushikamane pamoja katika vita vya kulinda heshima na utu."

Makamu Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Kiislamu la Mashia alisema: "Vita vyetu vya leo dhidi ya adui ni vita vya haki dhidi ya dhuluma na uchokozi, na bila shaka haki ndiyo itakayoshinda. Mwenyezi Mungu huwapa madhalimu muda lakini Hawasahau, na mwisho wao ni mbaya, sisi tumepata heshima, nao wameangukia katika fedheha ya ujasusi na usaliti. Aliyeuawa miongoni mwetu amepata daraja ya shahada; waliouawa wetu wako Peponi na waliouawa wao wako Motoni, na aliyebaki hai miongoni mwetu ameishi kwa heshima na utukufu."

Aliendelea kusema: "Tunapigana vita hivi huku, baada ya Mwenyezi Mungu, tukitegemea uungaji mkono wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ambayo yenyewe pia imekuwa ikikabiliwa na uchokozi na uhalifu wa wazi. Iran imesimama pamoja nasi na pamoja na Ghaza, katika njia hii, tumetoa sadaka ya vitu vyetu vya thamani zaidi, na kwetu hakuna tofauti kati ya sisi kuufuata umauti au umauti kutufuata. Sisi hatukuenda Marekani kuishambulia; bali wao ndio walikuja kwetu kwa kiburi na majivuno yao, mpaka Mlango-Bahari wa Hormuz ukawa mtego ambao Mwenyezi Mungu amewavuta humo ili wawazamishe kama alivyomvuta Firauni kwenye Mto Nile akazama humo."

Sheikh Al-Khatib alisisitiza: "Tuna yakini kwamba maadui hawatafanikiwa kufikia malengo yao, kwa sababu tegemeo letu kwanza ni Mwenyezi Mungu, na baada ya hapo ni azma ya kusimama imara ambayo wananchi wetu, familia zetu na Muqawama wetu nchini Lebanon, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Iraq, Yemen na Ghaza wameidhihirisha na wanaendelea kuidhihirisha."

Aliendelea kusema kuwa; adui wa Marekani na Mzayuni anasisitiza kuwapigisha magoti na kuwavunjia heshima, huku akivunja ahadi na kujiepusha na wajibu wake; jambo ambalo limekuwa sehemu ya tabia yake katika mahusiano yake yote.

Alisema kwamba; nchini Lebanon, adui anajaribu kuwadanganya kwa kuzungumzia kujiondoa katika maeneo ambayo kimsingi hayajawahi kuwa chini ya uvamizi, na kuyafanya maeneo hayo kuwa uwanja wa majaribio kwa kupeleka Jeshi la Lebanon huko.

Alihoji: "Ni uongo wa aina gani huu, hata kwa mtazamo wa lugha? Inawezekanaje adui ajiondoe katika eneo ambalo hakuwahi kulikalia kwa uvamizi? Na inawezekanaje serikali ya Lebanon, ambayo inafanya mazungumzo na adui, ikubali uongo huu? Vilevile, inawezekanaje Jeshi la Lebanon lihusishwe katika mchezo huu, isipokuwa kama lengo ni kuligongesha jeshi hilo na Muqawama pamoja na wananchi?"

Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Sheikh Al-Khatib alisisitiza tena: "Tunakataa aina yoyote ya makubaliano yanayohusu damu ya mashahidi wetu, wawe ni wapiganaji wa Muqawama au raia wa kawaida. Tunamtaka adui wa Kizayuni aondoke kikamilifu katika ardhi yetu, wananchi warejee kwa heshima katika miji, vijiji na nyumba zao, ujenzi wa maeneo yaliyoharibiwa uanze, na wafungwa wa Lebanon waachiliwe kutoka magereza ya Israel. Baada ya hapo ndipo mazungumzo kuhusu mkakati wa kitaifa wa ulinzi yataanza, ili tuwe na jeshi lenye uwezo wa kuwalinda wananchi, kuilinda ardhi na kuhakikisha mamlaka kamili ya taifa."

Aliendelea kusema: "Hatutaki wananchi wetu waendelee kubeba mzigo wa mateso, umwagaji damu na uharibifu zaidi, Serikali inapaswa kubeba jukumu hili, lau ingelitekeleza wajibu wake tangu mwanzo mambo yasingefikia hapa na tungeepuka gharama zote hizi, tulilisema jambo hili juzi kwa Balozi wa Ufaransa aliyekuja kutuaga na tuliona anaelewa msimamo wetu, hali hii inaibebesha Ufaransa pamoja na nchi nyingine za Ulaya wajibu wa kufanya juhudi za vitendo kuunga mkono msimamo huu."

Makamu Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Kiislamu la Mashia alisema: "Tunafuatilia kwa karibu operesheni za kimfumo za kubomoa, kuharibu na kusawazisha ardhi zinazofanywa na adui wa Kizayuni katika eneo la kusini, kiasi kwamba wananchi wengi hawawezi tena kutambua jiografia ya vijiji vyao, kwa huzuni na hasira kubwa tunarekodi ukimya huu wa viongozi wa Lebanon pamoja na jumuiya ya kimataifa mbele ya unyama huu, hali imefikia kiwango ambacho hata mjumbe wa Lebanon katika mazungumzo hana ujasiri wa kulizungumzia suala hili mbele ya Wamarekani na Wazayuni, je, mjumbe huyo wa Lebanon anatoa taswira ya aina gani ya udhalilishaji kwa nafsi yake na kwa nchi yake, wakati majeshi ya uvamizi yanaendelea na kuharibu miji na vijiji vya kusini kwa namna inayofanana na mauaji ya kizazi?"

Aliongeza: "Kwa msingi huo, tunaitaka serikali ya Lebanon iliweke suala hili katika mstari wa mbele wa vipaumbele vyake na ipaze sauti katika majukwaa ya Kiarabu na kimataifa kwa ajili ya kulinda mali zilizobaki za wananchi, hata hivyo tunafahamu kwamba wamechelewa sana kufanya hivyo, na inaonekana kwamba wao pamoja na baadhi ya mikondo ya kisiasa wanaridhia uhalifu huu wa wazi."

Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Sheikh Al-Khatib alisema: "Wiki iliyopita tulishiriki katika maziko ya Kiongozi Shahidi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Imam Shahidi Sayyid Ali Khamenei, na tukafanya mikutano na baadhi ya viongozi wa kisiasa na kidini wa Iran. Kutoka kwa wote hao tulisikia kauli na ahadi kuhusu Lebanon zikisisitiza kwamba hatuko peke yetu katika mapambano haya, na kwamba Jamhuri ya Kiislamu ina dhamira thabiti ya kuisaidia nchi yetu ili kusitisha vita na kuikomboa ardhi yetu kutoka katika uvamizi wa Israel, mpaka imefikia hatua kwamba Iran imefanya kuondoka kikamilifu kwa adui wa Israel katika ardhi ya Lebanon kuwa sharti la kufikiwa kwa makubaliano yoyote ya mwisho na Marekani."

Aliendelea kusema: "Kinachosikitisha ni kwamba viongozi wa Lebanon hawaipi umuhimu wowote dhamira hii ambayo kwao ni karata muhimu na chanzo cha nguvu, badala yake wanaendelea na mwenendo wao usiofaa dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu katika ngazi mbalimbali, hususan katika uwanja wa kidiplomasia; kana kwamba wanataka kukata uhusiano na Iran, huku wakati huo huo wakisisitiza kufanya mazungumzo ya moja kwa moja na adui, kwa hiyo tunaitaka tena serikali ya Lebanon kupitia upya misimamo yake na kurekebisha uhusiano wake na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ambayo baada ya Mwenyezi Mungu inapaswa kuwa tegemeo lao kuu."

Akichambua hali ya sasa, Sheikh Al-Khatib alisema: "Mgogoro halisi katika hatua hii ni kwamba maadui, iwe Marekani au utawala wa Kizayuni, wameingia katika kipindi cha uchaguzi kilichojaa misukosuko, kwa kusema ukweli tuna hofu kwamba Wamarekani na Waisraeli wanaweza kuchelewesha hatua zozote za kutekeleza malengo tunayoyatazamia na kuahirisha kila kitu hadi baada ya uchaguzi wa msimu wa vuli ujao. Kwa hiyo, tunalazimika kuwa tayari wakati wote; si tu katika uwanja wa kijeshi, bali pia katika nyanja za kisiasa, kiusalama na kijamii. Kwa sababu hiyo tunawaomba viongozi wa Lebanon wasidanganywe na makadirio yasiyo sahihi, waipitie upya misimamo yao na angalau wahifadhi heshima yao kabla ya kufika wakati ambao majuto hayatakuwa na faida."

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha