Jumatano 8 Julai 2026 - 12:25
Ayatullah A'rafi Apongeza Ushiriki wa Marajii wa Taqlid, Wanazuoni wa Dini, Hususan Wananchi wa Tehran na Qum katika Mazishi ya Mamilioni ya Kiongozi Shahidi

Hawza/ Mazishi haya ya kihistoria na yasiyo na mfano yaliyofanyika mjini Tehran na Qum yameunda mnyororo wa utukufu wa imani, Muqawama, umoja na ngome imara dhidi ya maadui. Kwa kupata msukumo kutokana na tukio hili, viongozi waheshimiwa wa vikosi vya ulinzi na Mhimili wa Muqawama wanapaswa kusimama kidete mbele ya wavamizi na wenye tamaa za kujitanua.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Ayatullah A'rafi, Mkurugenzi wa Hawza nchini Iran, kupitia jumbe mbili tofauti, amepongeza na kutoa shukrani kwa ushiriki wa hamasa na uthabiti wa wananchi, Marajii wa Taqlid, wanazuoni wa dini na wananchi wote wa Iran walioungana katika mazishi ya Kiongozi Shahidi yaliyofanyika Tehran na Qum. Matini ya jumbe hizo ni kama ifuatavyo:

Matini ya Ujumbe wa Shukrani kwa Wananchi wa Tehran

Kwa Jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, Mwenye Kurehemu

فَضَّلَ اللَّهُ الْمُجَاهِدِینَ بِأَمْوَالِهِمْ وَأَنْفُسِهِمْ عَلَی الْقَاعِدِینَ دَرَجَةً ۚ وَکُلًّا وَعَدَ اللَّهُ الْحُسْنَیٰ ۚ وَفَضَّلَ اللَّهُ الْمُجَاهِدِینَ عَلَی الْقَاعِدِینَ أَجْرًا عَظِیمًا

Enyi wananchi wenye uoni wa mbali, wa kimapinduzi na wenye heshima wa Tehran;

Enyi vijana mashujaa na waliopo daima mstari wa mbele wa mji mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu;

Kwa salamu na maamkizi kwa Hadhra tukufu ya Imamu wa Zama, Hadhrat Waliyul-Asr (arwahuna fidah), na kwa kutoa mkono wa pole katika siku hizi za maombolezo ya Aali wa Mwenyezi Mungu, kufuatia ushahidi wa Kiongozi mwenye hekima na mpiganaji asiyechoka, Hadhrat Ayatullah al-Udhma Khamenei (Quddisa Sirruhu az-Zakiyy), pamoja na mashahidi watukufu;

Tehran, Mama wa Miji wa ulimwengu wa Kiislamu, kwa mara nyingine tena, katika moja ya nyakati nyeti zaidi za historia ya Mapinduzi ya Kiislamu, imetekeleza wajibu wake wa kihistoria. Kupitia ushiriki wa uelewa, wa utukufu na uliojaa uthabiti katika mazishi ya mwili mtukufu wa Kiongozi Shahidi na kipenzi cha taifa, mmeumba hamasa ya kudumu iliyotokana na imani na heshima.

Ninyi wananchi watukufu wa Tehran, kuanzia wazee na vijana, wanawake na wanaume, wafanyabiashara na makundi ya taaluma mbalimbali, wanataaluma wa vyuo vikuu, wasomi na wanazuoni wakuu wa dini, kwa ushiriki wenu wa mamilioni katika mitaa ya jiji hili, mmeudhihirishia ulimwengu uhusiano usiovunjika kati ya "Umma na Uimamu", na kwa kushikamana na malengo matukufu ya Mapinduzi ya Kiislamu na kutoa bay'ah kwa Kiongozi Mkuu, Hadhrat Ayatullah Sayyid Mujtaba Hosseini Khamenei (Damat Barakatuhu), mmefanya upya ahadi yenu.

Bahari hii iliyochafuka ya umati wa watu katika mji mkuu wa Iran, haikuwa tu dhihirisho la bay'ah kwa Wilayah, bali pia ilikuwa ni sauti kubwa iliyowatetemesha wavamizi na maadui wa nchi hii. Mmeonesha kwamba Tehran bado ni kitovu kinachochemka cha uoni wa mbali na Muqawama, na kwamba katika kuendeleza njia ya Maimamu wawili wa Mapinduzi na mashahidi waliotoa damu zao, hamtaruhusu chembe yoyote ya shaka iingie mioyoni mwenu.

Ushiriki huu wa kishujaa wa Tehran ulikuwa ujumbe ulio wazi kwa watu wote huru duniani na kwa Mhimili wa Muqawama kwamba njia ya kudai kisasi cha damu safi ya mashahidi na kusimama dhidi ya mabeberu itaendelea kwa azma iliyo thabiti zaidi kuliko wakati mwingine wowote.

Mimi, huku nikieleza shukrani na heshima zangu nyingi mbele ya hamasa hii, uelewa na uaminifu, ninawashukuru kwa dhati wananchi wote wa Tehran na miji mingine ya Iran ya Kiislamu, viongozi waheshimiwa, vikosi vya huduma, familia za mashahidi, wapiganiaji waliojitoa muhanga, wageni walioshiriki kutoka nchi mbalimbali na wapendwa wote waliochangia kuumbwa kwa hamasa hii ya kihistoria.

Namuomba Mwenyezi Mungu Mtukufu aufanye ushiriki huu wa kishujaa kuwa akiba ya Akhera yenu, na chini ya uangalizi wa Hadhrat Waliyul-Asr (aj) na dua njema za roho safi za mashahidi, aipe Iran heshima, utukufu na usalama wa kudumu.

Tunatumaini kwamba ushiriki huu wenye maana na mawakibu za Ashura vitaendelea, na kwamba ushiriki mpana wa wananchi wapendwa katika majlisi za ukumbusho, kufanya upya bay'ah na ahadi kwa malengo ya Mapinduzi ya Kiislamu, utaongeza utukufu na ukubwa wa jihadi na Muqawama, na kwamba yote haya yatakubaliwa mbele ya Mwenyezi Mungu Mtukufu na mbele ya Hadhrat Baqiyyatullah al-A'dham (arwahuna fidah), na kupata uangalizi Wake maalumu.

وَمَا النَّصرُ إِلّا مِن عِندِ اللَّهِ العَزیزِ الحَکیمِ

Alireza A'rafi
Mkurugenzi wa Hawza za Elimu ya Kiislamu

Matini ya Ujumbe wa Shukrani kwa Marajii wa Taqlid na Wananchi wa Qum

Kwa Jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, Mwenye Kurehemu

وَلَا تَحْسَبَنَّ الَّذِینَ قُتِلُوا فِی سَبِیلِ اللَّهِ أَمْوَاتًا ۚ بَلْ أَحْیَاءٌ عِنْدَ رَبِّهِمْ یُرْزَقُونَ

Enyi wananchi watukufu na vijana wapendwa wa Qum;

Enyi wanazuoni wa dini na wanafunzi waheshimiwa wa Hawza;

Kwa salamu, maamkizi na mkono wa pole katika siku hizi za maombolezo ya Bwana wa Mashahidi (as), kufuatia ushahidi wa Kiongozi na Imam Shahidi (ra) pamoja na mashahidi watukufu;

Ninyi wananchi wa Qum, kwa zaidi ya miaka elfu moja, mmesimama chini ya bendera ya Uislamu mtukufu na mmeandika historia ya heshima. Hususan katika kipindi cha miaka mia moja iliyopita, mkiwa pamoja na Marjaiyya na Wilayah, mmeonyesha kushikamana kwenu na maadili, kujitolea, imani na uthabiti.

Baada ya harakati za Imam Khomeini Mkuu (ra), katika kipindi cha zaidi ya miaka sitini, mmeonesha kilele cha utukufu, kujitolea nafsi na kuwa mstari wa mbele katika harakati na Mapinduzi ya Kiislamu.

Na sasa, katika mazishi ya mwili mtukufu wa Imam Mujahid na Kiongozi Mkuu, Ayatullah al-Udhma Khamenei (ra), na kwa kufanya upya bay'ah kwa Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Hadhrat Ayatullah Sayyid Mujtaba Hosseini Khamenei (Damat Barakatuhu), mmeongeza ukurasa mwingine wa dhahabu katika kitabu kikubwa cha historia yenu, na mawimbi makubwa ya wananchi, vijana, wanawake, wanaume, makundi mbalimbali ya kijamii, wanafunzi wa Hawza, wanazuoni, maulamaa, viongozi wakubwa, Marajii watukufu na wasomi wa Hawza na vyuo vikuu kutoka Qum na maeneo yote ya nchi, mmeumba hamasa kubwa ya Ashura isiyo na mfano katika historia ya Qum, Mapinduzi ya Kiislamu na Hawza, na mmeongeza heshima nyingine kubwa. Hongereni kwa azma yenu thabiti, uthabiti wenu, ushiriki wenu wenye hamasa, unaojenga umoja, unaowavunja moyo maadui na unaoleta heshima, pamoja na sauti yenu kubwa ya kuitetea Uislamu na Mapinduzi ya Kiislamu.

Mngurumo wa ushiriki wenu, hamasa na uelewa wenu, pamoja na mawimbi makubwa ya wazee na vijana wenu, unatoa bishara ya kuendelea kwa njia ya Maimamu wawili wa Mapinduzi ya Kiislamu na mashahidi watukufu, pamoja na njia ya jihadi na Muqawama dhidi ya maadui wa Uislamu, Iran na ubinadamu, na pia njia ya kudai kisasi cha damu ya Kiongozi wenu Shahidi na mpendwa, pamoja na mashahidi madhulumu lakini wenye nguvu wa Iran na wa Mhimili wa Muqawama.

Mazishi haya ya kihistoria na yasiyo na mfano yaliyofanyika Tehran na Qum yameunda mnyororo wa utukufu wa imani, Muqawama na umoja, na yamejenga ngome imara mbele ya maadui. Kwa kupata msukumo kutokana na tukio hili, viongozi waheshimiwa wa vikosi vya ulinzi na Mhimili wa Muqawama wanapaswa kusimama kidete mbele ya wavamizi na wenye tamaa za kujitanua.

Huku nikitoa shukrani na pongezi zangu nyingi kwa wananchi wote wapendwa wa Qum, viongozi waheshimiwa, waandaaji wa programu, watoa huduma na msaada, washiriki na wageni wapendwa kutoka kote nchini na duniani, pia ninawashukuru kwa dhati maulamaa watukufu, wanazuoni wapendwa wa Hawza, wanafunzi na wabora wa Hawza, pamoja na Marajii wakuu wa Taqlid, hususan Hadhrat Ayatullah al-Udhma Jawadi Amuli na Hadhrat Ayatullah al-Udhma Subhani (Damat Barakatuhuma).

Ninatumaini kwamba ushiriki huu wa wananchi mitaani na mawakibu za Ashura vitaendelea, na kwamba ushiriki wa wananchi wapendwa katika majlisi za kuwasomea marehemu Al-Fatiha, kufanya upya maombolezo, ahadi na bay'ah, utaongeza zaidi utukufu wa jihadi, Muqawama na ushiriki wa wananchi wapendwa. Pia ninamuomba Mwenyezi Mungu Mtukufu kwamba yote haya yakubaliwe mbele Yake, mbele ya Hadhrat Waliyul-Asr (Arwahuna Fidah), na chini ya mtazamo wa Hadhrat Fatimah Ma'sumah (sa), na yapate rehema na uangalizi Wake maalumu.

وَمَا النَّصرُ إِلّا مِن عِندِ اللَّهِ العَزیزِ الحَکیمِ

Alireza A'rafi
Mkurugenzi wa Hawza za Elimu ya Kiislamu

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha