Alhamisi 11 Juni 2026 - 15:15
Mtawala wa Bahrain Amechukua Msimamo Mkali dhidi ya Maombolezo ya Muharram ya Mashia

Hawza/ Waziri wa Mambo ya Ndani wa Bahrain, kama ilivyo desturi yake ya kila mwaka, kabla ya kuanza kwa mwezi wa Muharram al-Haram, aliwaita viongozi wa takiya, huseinia na waandaaji wa majlisi za maombolezo ili kuwafikishia maagizo na tahadhari zake.

Kwa mujibu wa Kitengo cha yarjama cha Shirika la Habari la Hawza, likinukuu gazeti la Mir’at al-Bahrain, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Bahrain, Rashid bin Abdullah Al Khalifa, kama ilivyo desturi yake ya kila mwaka, kabla ya kuanza kwa mwezi wa Muharram al-Haram aliwaita viongozi wa takiya, husainiya na waandaaji wa maombolezo ili kuwafikishia maagizo na maonyo yake.

Mwaka huu, kutokana na mazingira na hali ambayo raia wa Kishia wanakabilia nayo wakati wa kuadhimisha ibada hii ya kila mwaka ya Kiislamu, kila kitu kinaonekana kuwa tofauti. Vita vinavyochochewa dhidi ya utambulisho wa Kishia vinaendelea, na Ashura, kwa mtazamo wa serikali, ni mojawapo ya nyanja muhimu zinazoweza kutumiwa kuwabana na kuwatesa Mashia.

Katika mkutano wa Rashid bin Abdullah - ambaye ametajwa kuwa msimamizi wa mradi wa kiusalama nchini Bahrain — na viongozi wa takiya, alilishambulia waziwazi aqida ya Wilayat al-Faqih na kutangaza kwamba hakutakuwa na uvumilivu wowote kwa kile alichokiita kuingiza siasa kwenye Ashura.

Huenda hili ni kurejea katika hatua ya mwanzo, lakini leo serikali rasmi ya Bahrain imevuka mipaka yote katika mradi wake wa ukandamizaji wa kimadhehebu, inataka waziwazi kuimeza jamii ya Kishia na inalenga kuifuta mizizi yake katika ardhi yake pamoja na maadili ya kidini na misingi ya Kiislamu ya Kihussein inayoiwakilisha.

Kinachotokea leo hakiwezi kufupishwa kuwa ni hatua za kawaida za kiutawala au maagizo ya kiusalama yanayotolewa kabla ya maombolezo ya Ashura, kama serikali, hususan Rashid bin Abdullah, inavyojaribu kuonyesha. Suala hili ni kubwa zaidi kuliko hayo, tunakabiliwa na jaribio la wazi la kuunda upya maombolezo ya Hussein kwa mujibu wa mtazamo rasmi wa kiusalama, badala ya kuzingatia roho yake ya kidini, ya wananchi na ya kihistoria ambayo imejikita nchini Bahrain kwa miaka kadhaa.

Serikali haitaki tu kudhibiti mitaa, bali pia inataka kudhibiti kikamilifu ibada na nembo yenyewe: nini kisemwe, nini kipandishwe, nani azungumze, na katika mipaka gani Mshia aruhusiwe kuonesha utambulisho wake, itikadi yake, huzuni yake na uhusiano wake na Ahlul-Bayt (a.s.). Hiki ndicho kiini cha mapambano halisi yanayoendelea leo dhidi ya maombolezo ya Ashura.

Ndiyo maana mashambulizi ya moja kwa moja dhidi ya Wilayat al-Faqih yanaibuka, pamoja na maonyo yanayohusiana na bendera, kaulimbiu, matamshi ya maombolezo, mazungumzo ya kidini na mashairi. Serikali inaandaa mazingira ya maombolezo ya kipekee yatakayogubikwa na ufuatiliaji mkali, masharti magumu na vitisho.

Badala ya serikali kuichukulia Ashura kama tukio kubwa la kidini lenye sifa zake maalumu katika jamii ya Bahrain, inalichukulia kama jalada la kiusalama lililo wazi linalohitaji uangalizi wa kudumu na uhamasishaji wa kisiasa.

Hatari zaidi ni kwamba; lugha hii ya kuongeza mvutano haiwezi kutenganishwa na mazingira ya jumla ambayo Bahrain imekuwa ikiishi ndani yake katika miezi iliyopita: kunyang’anywa uraia, kuhojiwa na vyombo vya usalama, kampeni za uchochezi za vyombo vya habari, kuwafuatilia wanazuoni wa dini, na tuhuma zilizo tayari kwa kila anayeshikamana na utambulisho wake wa kiitikadi na kisiasa.

Kwa hiyo, vitisho dhidi ya maombolezo ya Ashura si jambo la pembeni, bali ni kiungo kipya katika mradi mpana unaolenga kuwalazimisha Mashia wa Bahrain kusalimu amri na kuvunja azma yao ya pamoja.

Serikali inajua vyema kwamba; Ashura si msimu wa maombolezo wa kupita tu, bali ni nafasi kubwa ya kihisia na ya wananchi ambapo watu hujikuta tena katika utambulisho wao, historia yao na hisia yao ya pamoja ya kuhusika na njia ya Hussein inayosimama dhidi ya dhulma, na hasa kwa sababu hiyo ndiyo maana inajaribu mara kwa mara kuliondoa tukio hili katika maudhui yake halisi na kuligeuza kuwa mila za kawaida zisizo na roho wala ujumbe.

Uzoefu wa Bahrain katika miongo iliyopita umeonyesha kwamba kadiri ukandamizaji ulivyozidi kuwa mkali, ndivyo watu walivyozidi kushikamana na ibada na nembo zao za kidini, kwa sababu wanaziona kuwa sehemu ya heshima na utambulisho wao, si tukio la msimu linaloweza kujadiliwa au kubadilishwa kwa maamuzi ya kiusalama.

Kwa hiyo, inaonekana kwamba Muharram ya mwaka huu nchini Bahrain hautakuwa msimu wa kawaida. Macho yote yanaelekezwa kwenye kiwango cha vikwazo na mashinikizo ambayo utawala wa Aal Khalifa utajaribu kuyaweka, na pia namna ambavyo vyombo vya usalama vitashughulikia majlisi za maombolezo, misafara, hotuba za kidini na alama za kiitikadi.

Serikali inataka Ashura iliyoko chini ya udhibiti wake kamili, ilhali wananchi wa Bahrain wanashikamana na haki yao ya kiasili ya kuadhimisha ibada zao kwa namna ambayo daima wameifahamu: kwa uhuru, kwa heshima na bila uingiliaji wa kisiasa au wa kiusalama.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha