Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, mfululizo wa tafiti za Mahdawiyya zenye anuani isemayo “Kuielekea Jamii Bora”, unaotolewa kwa lengo la kusambaza mafundisho na maarifa yanayohusiana na Imam wa Zama (a.f), unawasilishwa kwa waheshimiwa wasomi kama ifatavyo:
Katika toleo lililopita tuliashiria ushiriki wa pamoja wa mwanamke na mwanaume katika kufanikisha malengo ya Mwenyezi Mungu. Katika utekelezaji huo, kuna majukumu ya jumla na ya pamoja kama vile kushikamana na kumcha Mwenyezi Mungu, kuamrisha mema, kukataza maovu na kujisitiri (ambapo kwa mwanamke, miongoni mwa mifano iliyo wazi ni kuilinda heshima, haya na hijabu), ambayo yameelezwa na Muumba Mmoja Asiye na mfano katika aya za Qur’ani Tukufu.
Lakini jambo lisilopaswa kupuuzwa ni nafasi maalumu na ya kipekee ya wanawake katika jamii ya Kiislamu na katika utekelezaji wa malengo ya Mwenyezi Mungu.
Huenda ikasemekana kwamba jukumu muhimu zaidi la wanawake kwenye jamii katika njia ya kutekeleza malengo ya Mwenyezi Mungu, na hasa katika kuandaa mazingira ya kudhihiri Mwokozi wa wanadamu, ni suala la “malezi ya watoto”, au kwa maneno mengine “kuwalea wanaosubiri”.
Kuwalea wanaosubiri
Ingawa baba na mama wote wawili wana mchango mkubwa katika malezi ya mtoto, lakini nafasi ya mama ni ya kipekee; nafasi ambayo ikiwa haitatekelezwa kwa usahihi, basi shakhsia ya mtoto haitajengeka ipasavyo kwa ajili ya majukumu ya Mwenyezi Mungu.
Imam Khomeini (r.a) kuhusu ukubwa wa nafasi ya malezi ya mwanamke amesema:
Mwanamke ni binadamu, na tena ni binadamu mkubwa, mwanamke ni mlezi wa jamii, kutoka katika mikono ya mwanamke ndipo wanadamu hupatikana, mwanamke ndiye mlezi wa wanadamu, furaha na maangamizi ya nchi hutegemea uwepo wa mwanamke, mwanamke kwa malezi yake sahihi humlea mwanadamu mwema, na kwa malezi yake sahihi huijenga nchi.”
(Sahifeh Imam, Juzuu ya 7, uk. 239)
Na huenda asili ya athari kubwa na za ajabu za nafasi ya malezi ya mwanamke akiwa mama ikapatikana katika kauli ya Amirul-Mu’minin Ali (a.s). Yeye amesema:
«اَلْوَلَدُ مَطْبُوعٌ عَلَی حُبِّ أُمِّهِ»
“Mtoto ameumbwa juu ya mapenzi ya mama yake.”
(Ghurar al-Hikam wa Durar al-Kalim, Juzuu ya 1, uk. 100)
Mapenzi ambayo Mwenyezi Mungu ameyaweka katika uhusiano wa mama na mtoto hayawezi kupatikana katika uhusiano mwingine wowote, ndiyo maana mwanamke akiwa katika nafasi ya mama — kwa kutumia nyenzo hii muhimu ya malezi (yaani mapenzi ya kimama) aliyopewa — anaweza kuifanya roho na nafsi ya mtoto kuwa tayari kupokea mafunzo ya Mwenyezi Mungu na ya kiroho, na kumuandaa kwa ajili ya kushiriki zaidi na kwa namna bora zaidi katika njia ya kudhihiri Mwokozi wa wanadamu na kusimamisha serikali ya Mwenyezi Mungu.
Kwa hiyo, iwe kwa mtazamo wa jumla au wa pekee, nafasi ya mwanamke katika kuandaa mazingira ya kudhihiri na pia katika serikali ya Mahdawiyya haiwezi kamwe kudogoshwa au kupuuzwa.
Yaliyotajwa hapo juu ni muhtasari wa tafiti muhimu zaidi zinayohusiana na nafasi na hadhi ya mwanamke katika kudhihiri na serikali ya Mahdi, ambazo zimewasilishwa kwa wasomaji waheshimiwa. Kilichobakia ni tafiti za pembeni zinayohusiana na mada hii, kama vile:
“Uwepo au kutokuwepo kwa wanawake miongoni mwa watu 313 masahaba maalumu wa Imam Mahdi (a.f)”, “Kurejea kwa wanawake (Raj’a) wakati wa kudhihiri na serikali ya Imam” na kadhalika, ambazo InshaAllah zitajadiliwa katika sehemu inayofuata.
Utafiti huu unaendelea...
Maoni yako