Kwa mujibu wa ripoti ya kitengo cha tarjama cha Shirika la Habari la Hawza, Ihab Hamada, mwakilishi wa Kambi ya “Uaminifu kwa Muqawama” nchini Lebanon, katika hotuba yake wakati wa hafla iliyofanyika katika Husseinia ya Imam Sadiq (as) katika eneo la Al-Marh al-Shamali, mkoani Hermel, kutokana na mnasaba wa kumbukumbu ya siku arobaini tangia kupata shahada shahidi Muhammad Nabil Aloueh, alisema: Kusisitiza kuvuliwa silaha kwa Muqawama, kwa hakika ni kusisitiza kuondoa sehemu ya nguvu ya jamii hii; hatua hii inalenga kuifanya jamii iwe katika hali ya udhaifu na kuwa shabaha ya mashambulizi ili hali yake ibadilishwe, iwe katika kiwango cha idadi ya watu au katika kiwango cha jiografia, jambo ambalo linawakilisha hatari kubwa kwa uwepo wa Lebanon.
Hamada aliongeza: Kiwango cha mashambulizi, uharibifu wa vijiji na kushambuliwa kwa maeneo yote ya Lebanon kinaongezeka sambamba na maendeleo ya mazungumzo yanayoongozwa na serikali. Wao (maafisa wa serikali) wanakaa pamoja na adui yetu katika meza moja, wanaweka mikono yao mikononi mwa wauaji, halafu baadaye wanatupatia nadharia kwa jina la mamlaka ya taifa na uhuru wa nchi.
Pia alionya dhidi ya kufuatilia simulizi ambazo vyombo vingine vya habari vinajaribu kuzieneza; simulizi zinazodai kwamba Muqawama umeshindwa na katika mapambano umemruhusu adui kukalia sehemu kubwa ya Lebanon, alisema madai hayo ni ya uongo na akaongeza: “Ukweli ni kwamba wapiganaji wa Muqawama wapo uwanjani, wanatimiza jukumu lao la jihadi, na kwa kutumia mbinu tofauti wanamtega adui, mbinu hizi si lazima zilenge kuhifadhi kila eneo la kijiografia, bali lengo lake ni kumvuta adui katika maeneo ya kuvizia na mitego ya kijeshi ili kuisababishia vifaa na askari wake kushindwa kwa kiwango kikubwa zaidi.”
Mjumbe wa Kambi ya Muqawama aliendelea kusema: Adui anajaribu kudhibiti hali bila ya kujikita moja kwa moja katika maeneo hayo, lakini wakati wote anapigwa na kudhoofishwa hata katika mstari wa kwanza wa vijiji vya mpakani. Leo mashambulizi kwa kutumia makombora maalumu yalilenga makazi yote yaliyokaliwa kaskazini mwa Palestina, na yatakayokuja baadaye yatakuwa makubwa zaidi na yatawageuza Wazayuni kuwa maiti zilizotawanyika.
Akiwa na masikitiko aliongeza kusema: Muqawama ulilazimika kurudi tena vitani chini ya mazingira tofauti na magumu kusini mwa Mto Litani, baada ya kuwa ulikuwa umeondoka eneo hilo kwa mujibu wa makubaliano ya Oktoba 2024. Tulikubali makubaliano hayo kwa msingi wa kuhifadhi “Serikali ya Lebanon” iliyokuwa imesaini maelewano hayo; lakini katika kipindi cha miezi 15, hakuna athari yoyote iliyobaki ya mahandaki na vichuguu, na vijana wetu wamelazimika kupigana katika maeneo ya wazi. Hata hivyo bado wanaendelea kusababisha hasara kubwa kwa adui.
Hamada aliendelea kusema: Hali hii ni matokeo ya njama za serikali na maamuzi yake ya kuwahesabu wapiganaji wa Muqawama kuwa wahalifu; wale wanaouawa kishahidi katika kuitetea Lebanon, serikali huwapeleka mahakamani. Huku wengine wakijitokeza kwenye televisheni na kudai kuwa serikali ina njia moja tu ya kusimamisha mapatano ya kusitisha vita na kuifanya Israel ijiondoe, nayo ni “mazungumzo ya moja kwa moja”.
Wao wanatumia mkakati wa “kulia na kutoa machozi” mbele ya mnyama wa Kizayuni; adui ambaye dunia yote inamwona kuwa yuko nje ya viwango vya kibinadamu, isipokuwa serikali ya Lebanon ambayo inataka kupata ushindi kupitia mazungumzo hayo na kuikomboa Lebanon.
Maoni yako