Kwa mujibu wa ripoti ya mwandishi wa Shirika la Habari la Hawza kutoka Mashhad, Hujjatul-Islam wal-Muslimin Hussein Ghabris, mmoja wa makamanda wa Hizbullah ya Lebanon, Jumapili ya tarehe 13 Mei katika mkutano wa waandishi wa habari kwenye Kongamano la Pili la Kimataifa la Ghadir na Muqawama lililofanyika katika Ofisi Kuu ya Wakfu na Masuala ya Hisani ya Khorasan Razavi, alipowasilisha ujumbe wa urafiki na shukrani wa taifa la Lebanon kwa wananchi wa Iran, alisisitiza juu ya kuendelea kwa njia ya Muqawama na uhusiano wake wa kina na utamaduni wa Ghadir.
Akijibu swali kuhusu hali ya sasa ya mhimili wa Muqawama na mtazamo wake wa siku zijazo alisema: “Nimeleta kutoka Lebanon jumbe mbili kwa taifa la Iran; wa kwanza ni ujumbe wa urafiki, mapenzi na shukrani kutoka kwa wananchi wa Lebanon kwa Wairan wote, wakiwemo viongozi, vikosi vya kijeshi, wasimamizi na wananchi kwa ujumla ambao daima wamekuwa pamoja na taifa la Lebanon.”
Hujjatul-Islam wal-Muslimin Ghabris aliongeza: “Wananchi wa Lebanon wanathamini misaada yote na ushirikiano wa taifa la Iran, na wanawasilisha salamu zao pamoja na shukrani zao za dhati kwa wananchi wapendwa wa Iran.”
Kamanda huyu wa Hizbullah ya Lebanon, akizungumzia hali ngumu iliyopo Lebanon alisema: “Ujumbe wangu wa pili unahusu mateso, migogoro, matatizo na mashinikizo ambayo taifa la Lebanon linayabeba katika njia ya Muqawama; ugumu ambao si wa siku moja tu, bali kila saa na kila dakika wananchi wa Lebanon wanakabiliana nao.”
Aliendelea kusema: “Pamoja na matatizo haya yote, taifa la Lebanon linafuatilia malengo na matarajio makubwa, na lengo letu muhimu zaidi ni kutekeleza wajibu wa Mwenyezi Mungu na wa kisheria; wajibu ambao kwa ajili ya kuutekeleza hatutasita kujitolea.”
Hujjatul-Islam wal-Muslimin Ghabris alisisitiza: “Kwetu sisi, kufa shahidi na ushindi vyote ni kheri na mafanikio; kwa sababu jambo lenye umuhimu ni kutekeleza wajibu wa Mwenyezi Mungu na kusimama imara katika njia ya haki.”
Akizungumzia nafasi ya Idi ya Ghadir katika mfumo wa fikra wa mhimili wa Muqawama alisema: “Kuadhimisha Ghadir si sherehe au tukio la kihistoria pekee, bali ni wajibu wa Mwenyezi Mungu juu ya Waislamu wote ili kuandaa misingi ya kielimu, kitamaduni na kijamii inayohitajika kwa ajili ya kudhihiri kwa Hadhrat Waliyul-Asr (aj).”
Kamanda huyu wa Hizbullah ya Lebanon alieleza: “Juhudi zetu zote, shughuli zetu na mapambano yetu yanapata maana katika njia ya kuiandaa jamii ya Kiislamu kwa ajili ya kusimama na kudhihiri kwa Imam Mahdi (aj), na Ghadir ndiyo sehemu muhimu zaidi ya kuanzia njia hii.”
Hujjatul-Islam wal-Muslimin Ghabris akifafanua hali ya vita vya sasa katika eneo alisema: “Leo kuna vita kubwa kati ya kambi mbili; kwa upande mmoja kuna Hizbullah ya Lebanon, Ansarullah ya Yemen, Hashd al-Shaabi ya Iraq, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na mhimili wa Muqawama, na kwa upande mwingine kuna kambi ya ubeberu wa kimataifa pamoja na nguvu zote zinazouunga mkono.”
Aliongeza kuwa: “Sababu kuu ya mgongano huu si tofauti za kisiasa au kijiografia, bali mizizi yake imo katika njia ya Wilayah na njia ya Amirul-Muuminina Ali (as); njia ambayo ilianza Ghadir na imeendelea hadi leo.”
Hujjatul-Islam wal-Muslimin Ghabris alisisitiza: “Njia ya Wilayah ni njia ya Imam Ali (as), njia ya Uimamu na uongozi wa Mwenyezi Mungu, na njia hii itaendelea hadi kudhihiri kwa Hadhrat Waliyul-Asr (aj).”
Kamanda huyu wa Hizbullah ya Lebanon akizungumzia jinai za utawala wa Kizayuni nchini Lebanon alisema: “Leo nchini Lebanon kuna vijiji ambavyo vimesawazishwa kabisa na ardhi, na hakuna athari yoyote iliyobaki ya nyumba au wakazi wake.”
Aliendelea: “Pamoja na kiwango hiki cha uharibifu, wananchi wa Lebanon bado wako imara na wenye kusimama kidete katika uwanja, na hawajarudi nyuma kutoka katika malengo yao.”
Hujjatul-Islam wal-Muslimin Ghabris alisema: “Adui inadhani kwamba; kwa kuharibu nyumba na miundombinu anaweza kuvunja azma ya taifa la Lebanon, lakini Muqawama umeota mizizi ndani ya mioyo ya wananchi na hautaangamia kutokana na hatua hizi.”
Akiwashukuru tena wananchi wa Iran alisema: “Wananchi wa Lebanon wanafuatilia daima habari za Iran kupitia vyombo vya habari na vituo vya televisheni na wanafatilia kwa makini maendeleo ya Jamhuri ya Kiislamu.”
Kamanda huyu wa Hizbullah ya Lebanon aliongeza: “Taifa la Lebanon katika swala zake za kila siku huwaombea ushindi Umma wa Kiislamu, heshima ya Waislamu na mafanikio ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.”
Mwisho, akifikisha salamu na shukrani za wananchi wa Lebanon kwa taifa la Iran kwa kusema: “Wananchi wa Lebanon daima wanamuomba Mwenyezi Mungu kwa ajili ya ustawi wa Iran ya Kiislamu, heshima ya Umma wa Kiislamu na mafanikio ya Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu, na wanamuomba Mwenyezi Mungu ushindi wa kambi ya haki dhidi ya kambi ya batili.”
Maoni yako