Jumapili 31 Mei 2026 - 13:20
Imamu wa Swala ya Ijumaa wa Baghdad atahadharisha kuhusu kuongezeka kwa mpasuko kati ya tabaka la kisiasa na wananchi wa Iraq

Hawza/ Ayatullah Sayyid Yasin Mousawi ameonya kuhusu kuwepo kwa mpasuko mkubwa kati ya tabaka la kisiasa na wananchi wa Iraq, huku akisisitiza kuwa; nchi ipo katika njia panda kati ya mamlaka huru ya taifa au utegemezi wa matakwa ya Marekani.

Kwa mujibu wa Kitengo cha Kimataifa cha Shirika la Habari la Hawza, Ayatullah Sayyid Yasin Mousawi, Imamu wa Swala ya Ijumaa wa Baghdad na mmoja wa walimu mashuhuri wa Hawza ya Kielimu ya Najaf Ashraf, alisisitiza kuwa; uwanja wa kisiasa wa Iraq unakabiliwa na mpasuko unaozidi kuongezeka kati ya tabaka la kisiasa na wananchi; mpasuko ambao unaonekana miongoni mwa makundi yaliyopo madarakani pamoja na makundi yanayotaka kufikia madaraka hayo.

Akieleza kwamba ukosoaji wake wa hali ya kisiasa ya nchi si kwa lengo la kukosoa tu, bali unatokana na hofu ya kurekebisha makosa ya kimuundo na ya msingi ambayo yameathiri mustakabali wa serikali ya Iraq, aliongeza: “Makosa madogo yapo katika jamii zote na mifumo yote, lakini hatari kuu imo katika makosa makubwa ya kimkakati ambayo yanahusiana na namna nchi inavyoendeshwa na mtazamo wa viongozi kuhusu utawala.”

Ayatullah Mousawi alifafanua kuwa; sehemu kubwa ya tabaka la kisiasa hufanya kazi kwa msingi wa mitazamo finyu ya kichama, binafsi au kifamilia, na jambo hili husababisha kuchukuliwa maamuzi yaliyo mbali na maslahi ya umma.

Alielezea mtazamo finyu wa kisiasa na kutoweza kuelewa mahitaji ya jamii kuwa ni miongoni mwa sababu kuu za migogoro iliyojikusanya nchini, na akatoa wito kwa viongozi kujenga upya uhusiano wao na wananchi pamoja na kuzingatia mahitaji yao halisi.

Imamu wa Swala ya Ijumaa wa Baghdad aliendelea huku akirejelea mifano ya mafanikio ya uongozi, na akaitaja tajriba ya Imam Khomeini (rh), akisema: “Ushindi na kuendelea kwa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran halikuwa jambo la bahati mbaya, bali yalikuwa ni matokeo ya ufahamu wa kina kuhusu jamii ya Iran na mahitaji yake.”

Kwa kutegemea nukuu kutoka kwa Imam Khomeini (rh), alibainisha kwamba; siri ya mafanikio yake ikilinganishwa na baadhi ya tajriba zilizotangulia ilikuwa ni ufahamu sahihi wa wananchi wa Iran na uwezo wa kujibu matarajio na maadili yao.

Ayatullah Mousawi aliongeza: “Viongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu walisisitiza kujijenga binafsi, kujitakasa nafsi na kutekeleza jihadi kubwa kwa kuongozwa na mafundisho ya Qur’ani Tukufu na maneno ya Amirul-Muuminina Imam Ali (as), na mtazamo huo uliwafanya kuwa imara mbele ya vivutio vya madaraka na mali.”

Aliendelea kusema: “Njia hii ilisababisha viongozi kubaki karibu na wananchi na kushirikiana nao katika furaha na matatizo yao; jambo ambalo lilipelekea kuimarika kwa kuaminiana kati ya jamii na dola, kwa sababu hiyo hata leo, baada ya kupita siku 90, wananchi bado wanaendelea kujitokeza mitaani na kudai kulipiziwa damu ya kiongozi shahidi Ayatullah al-Udhma Sayyid Ali Khamenei.”

Imamu wa Swala ya Ijumaa wa Baghdad, kwa upande mwingine, aliashiria tajriba ya Iraq baada ya mwaka 2003 (1382 Hijria Shamsia) kuwa ni ushahidi wa kupungua hatua kwa hatua imani ya wananchi kwa tabaka la kisiasa, na akasema: “Wakati wananchi walitarajia kuona watu wa karibu nao wakisimamia uongozi wa nchi, umbali kati ya viongozi na wananchi uliongezeka siku baada ya siku.”

Alieleza sababu ya mpasuko huu kuwa ni mwelekeo wa kushughulikia mambo ya nje ya mwonekano, marupurupu, na kujitenga na matatizo ya kila siku ya wananchi, na akaonya kwamba; kuongezeka kwa idadi ya walinzi, misafara ya kifahari na kuishi katika majumba si ishara ya nguvu ya kweli, bali huongeza zaidi umbali wa kisaikolojia na kijamii kati ya watawala na wananchi.

Ayatullah Mousawi aliwataka viongozi kupambana na matamanio ya nafsi na kujiepusha na anasa pamoja na kujilimbikizia mali, akisema: “Wengi waliopo madarakani leo hapo awali walikuwa na maisha ya kawaida, lakini madaraka na mali vimebadilisha mtindo wa maisha yao.”

Alisisitiza: “Kuungwa mkono na wananchi kunahitaji unyenyekevu, kuendana na matakwa ya jamii na kujiepusha na mtazamo wa kibiashara kuhusu serikali na maslahi ya umma.”

Imamu wa Swala ya Ijumaa wa Baghdad pia alikosoa kuendelea kwa mgogoro wa umeme nchini Iraq licha ya fedha nyingi zilizotumika katika sekta hiyo, na akasema: “Licha ya kutangazwa matumizi ya mabilioni ya dola katika sekta ya umeme, bado hakuna suluhisho la msingi lililotolewa kwa tatizo hili, na wananchi hasa katika msimu wa joto bado wanakabiliwa na adha ya kukatika umeme mara kwa mara.”

Aliongeza: “Wakati umefika kwa serikali kuvuka hatua ya ahadi na kauli za vyombo vya habari, na kuelekea katika hatua za vitendo na zenye matokeo.”

Ayatullah Mousawi pia alitoa wito wa kushughulikiwa kwa uzito matatizo mengine ya maisha, yakiwemo ukosefu wa ajira, kupanda kwa bei na udhaifu wa huduma za afya, na akaonya kuwa; kuendelea kwa matatizo haya kutaleta changamoto kwa uthabiti wa kijamii na kiuchumi katika nchi.

Katika sehemu nyingine ya mazungumzo yake alizungumzia sera za Marekani katika eneo hili na akasema: “Misimamo iliyotangazwa na Donald Trump, Rais wa Marekani, kuhusu Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, imeonyesha wazi migongano kati ya kauli mbiu na uhalisia wa mambo.”

Imamu wa Swala ya Ijumaa wa Baghdad anaamini kuwa Washington katika baadhi ya vipindi imelazimika kukubali masharti ya Iran katika mchakato wa mazungumzo, lakini shinikizo la utawala wa Kizayuni limesababisha Marekani kuchukua misimamo mikali zaidi.

Pia alirejelea kuendelea kwa mashambulizi ya utawala wa Kizayuni dhidi ya Lebanon, hususan kusini na eneo la Biqaa, na akasema: “Mashambulizi haya ambayo yanaambatana na mauaji, huwafanya watu kuwa wakimbizi na kulenga raia, yanafanyika kwa lengo la kuleta mabadiliko ya idadi ya watu na kuwaondoa wakazi kutoka katika ardhi zao.”

Ayatullah Mousawi alisisitiza kiwa: “Mataifa yenye muqawama hayatasalimu amri mbele ya mashinikizo na hayatakubali njia ya maridhiano wala kurudi nyuma.”

Aliendelea kuzungumzia maendeleo yanayohusiana na Mlango wa Hormuz na uhusiano wa Iran na Oman, na akasema: “Shinikizo na vitisho vya Marekani dhidi ya Sultani wa Oman kwa sababu ya ukaribu wa nchi hiyo na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran vinaonyesha asili ya sera za Washington za kulazimisha matakwa yake kupitia mashinikizo ya kisiasa na kiuchumi.”

Imamu wa Swala ya Ijumaa wa Baghdad alibainisha kuwa: “Marekani haizitazami nchi za eneo hili kama washirika sawa, bali inatafuta kuimarisha utegemezi wao wa kisiasa na kiuchumi.”

Aliongeza kwa kusema: “Msimamo imara wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran umefanya baadhi ya nchi za eneo hili, ikiwemo baadhi ya nchi za Ghuba ya Uajemi, kupata nafasi kubwa zaidi ya kuchukua sera huru katika mahusiano yao ya kikanda.”

Mwisho, Ayatullah Sayyid Yasin Mousawi alitoa wito kwa makundi ya kisiasa na wananchi wa Iraq kushikamana na misingi ya mamlaka ya taifa na kuiheshimu nchi, na akasema: “Iraq haiwezi kwa wakati mmoja kuunganisha kati ya matakwa ya uhuru na matakwa ya utegemezi.”

Alifafanua kwa kisema: “Kuundwa kwa serikali yenye nguvu na yenye uadilifu kunahitaji uamuzi wa kujitegemea, kuzingatia maslahi ya wananchi, na kuwa tayari kubeba jukumu la mustakabali wa nchi, mbali na mashinikizo ya nje.”

Imamu wa Swala ya Ijumaa wa Baghdad alihitimisha kwa kukumbusha riwaya zinazohusu nafasi kuu ya Iraq na wananchi wake katika harakati za mageuzi na uadilifu wa dunia, huku akisisitiza umuhimu wa jukumu hili la kihistoria.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha