Jumapili 9 Agosti 2026 - 21:15
Imamu wa Swala ya Ijumaa Baghdad Atahadharisha Juu ya Juhudi za Marekani za Kudhoofisha Umoja wa Vikosi vya Ulinzi vya Iraq

Hawzah/ Ayatullah Sayyid Yasin Mousavi ameitaja ziara ya Arubaini kuwa ni “ngao ya kiroho” dhidi ya hali ya kukata tamaa inayoukabili Umma, na kwa kurejelea uwepo wa mamilioni ya mazuwari, amesema kuwa; ziara hiyo ni tiba halisi ya hofu na kujitenga. Aidha, ameonya kuhusu juhudi za Marekani za kuleta mgawanyiko miongoni mwa vikosi vya ulinzi vya Iraq na kusisitiza umuhimu wa umoja wa kitaifa mbele ya adui wa pamoja.

Kwa mujibu wa Idara ya Kimataifa ya Shirika la Habari la Hawza, Ayatullah Sayyid Yasin Mousavi, Imamu wa Swala ya Ijumaa Baghdad na mwalimu wa Hawza ya Najaf Ashraf, katika khutuba za Swala ya Ijumaa ya tarehe 16 Mordad 1405, alisisitiza kwamba: Ziara ya Arubaini imekuwa tukio la kipekee na linalovuka mipaka ya eneo, ambalo haliwezi kufasiriwa kwa mitazamo ya kimaada pekee. Uwepo wa mamilioni ya mazuwari unaweza kuchukuliwa kuwa “hitaji la kisheria” na “tiba ya kiroho” kwa ajili ya kurejesha heshima na kuvunja hali ya kukata tamaa na kushindwa miongoni mwa Umma.

Ayatullah Sayyid Yasin Mousavi katika maelezo yake ya kina, akirejelea idadi ambayo haijawahi kushuhudiwa ya mazuwari wa Arubaini, alisema: Idadi ya mazuwari imevuka watu milioni 22, na makadirio yanaonesha kwamba idadi ya watu ambao, kutokana na msongamano mkubwa, hawakuweza kufika katikati ya mji, ni mara kadhaa ya idadi hiyo.

Aliongeza: Uwepo huu wa mamilioni ya watu umevuka hata baadhi ya mikusanyiko mikubwa zaidi ya kidini duniani, na tukio la “utoaji na ukarimu” pamoja na ukarimu wa kipekee wa wananchi wa Iraq limevutia umakini wa watafiti na wawakilishi wa dini mbalimbali.

Imamu wa Swala ya Ijumaa Baghdad pia alirejelea mabadiliko makubwa ya kitabia miongoni mwa wananchi wa Iraq na kusema: “Hata watu wenye hasira na wale ambao huwa wagumu katika kutumia mali zao, huyeyuka mbele ya fahari ya kuwahudumia mazuwari.”

Alisema kwamba; mwenendo huu unatokana na uhusiano wa kina wa kiitikadi wa wananchi na Imam Hussein (as), na akautaja kuwa miongoni mwa “siri za ulimwengu” ambazo ndio sababu kuu ya kujitolea huku.

Ayatullah Mousavi pia, kuhusu tukio la matembezi ya Arubaini, licha ya hali ya hewa ngumu, alisema: Harakati hii haiwezi kuelezwa kwa kutumia vipimo vya kimaada pekee, bali ina mizizi katika vipengele vya kiroho na vya ghaibu, Mazuwari wanahisi kwamba Imam Hussein (as) anawatazama kwa mtazamo wa kimalaika; kwa sababu hiyo, wanaelekea katika ziara kwa shauku isiyoweza kuelezeka, na changamoto za maisha haziwazuii kusonga mbele.

Mkusanyiko na uwepo wa mamilioni ya watu; hitaji la kidini

Imamu wa Swala ya Ijumaa Baghdad, akiwajibu wakosoaji na wale wanaotia shaka kuhusu ufanisi wa mikusanyiko kama hiyo, alisisitiza: “Idadi na mikusanyiko” katika mafundisho ya dini ni hitaji la kisheria, na matini za Qur’ani pamoja na hukumu za Kiislamu zinasisitiza umuhimu wa kukusanyika.

Katika suala hili, alirejelea wajibu wa Swala ya Ijumaa na ibada ya Hija, na kusema: Hija ni “mkusanyiko mkubwa zaidi” wa Waislamu.

Ayatullah Mousavi alisema: Hikima ya Mwenyezi Mungu katika kuandaa mikusanyiko mikubwa ya aina hii ni kuunda “ngao ya kisaikolojia” dhidi ya hisia za udhaifu na kujitenga ambazo madola makubwa huzilazimisha kwa mataifa.

Alitaja mikusanyiko ya mamilioni ya watu kuwa “tiba halisi” ya magonjwa ya kiroho kama vile hofu na woga, na kuongeza: Hisia ya udhaifu humpelekea mwanadamu katika huzuni na kukata tamaa; lakini mwanadamu anapojiona akiwa katikati ya bahari ya mazuwari na kusikia kaulimbiu zenye heshima na za kishujaa za Imam Hussein (as), hali ya kujiona ameshindwa huondoka na kubadilika kuwa nguvu ya kiroho inayoinua kiwango cha ibada ya mwanadamu na uhusiano wake na Mwenyezi Mungu.

Tahadhari kuhusu juhudi za nje za kuzuia kufanyika ziara ya Arubaini

Imamu wa Swala ya Ijumaa Baghdad katika sehemu nyingine ya hotuba yake alionya kuhusu juhudi za nje za kuzuia kufanyika kwa ibada hii ya kidini, na kuishutumu Marekani kwa kujaribu kuweka vikwazo katika njia ya kufanyika kwa ziara ya Arubaini kupitia mashinikizo ya kisiasa na kiusalama.

Alisisitiza kuwa: Juhudi za kuleta ukosefu wa usalama na kufanya mashambulizi zimefeli kutokana na uangalifu wa wananchi wa Iraq, na uwepo mkubwa wa wananchi katika ziara ya Arubaini unaonesha kupungua kwa ushawishi wa Marekani katika eneo hilo.

Onyo kuhusu mipango ya Marekani ya kuleta mgawanyiko miongoni mwa vikosi vya ulinzi vya Iraq

Ayatullah Mousavi aliendelea kwa kurejelea masuala ya usalama wa kitaifa wa Iraq na kuonya kwamba: Kuna mipango inayotekelezwa ambayo Tom Barrack, afisa wa Marekani, anajaribu kuitumia ili kuibua migogoro ya ndani na kuleta mgawanyiko katika umoja wa vikosi vya ulinzi vya Iraq, na kuvisukuma vikabiliane na makundi ya Muqawama na eneo la Kurdistan.

Akisisitiza umuhimu wa kuhifadhi mshikamano wa vikosi vya ulinzi vya Iraq, alisema kwa msisitizo: “Damu ya Mashia ni mstari mwekundu,” na ni lazima kuzuia juhudi zozote za kuvisukuma vikosi vya Iraq katika fitina zinazolenga kuidhoofisha Serikali na muundo wa kijeshi wa nchi.

Kusisitiza umoja mbele ya adui wa pamoja

Imamu wa Swala ya Ijumaa Baghdad, mwishoni, akisisitiza umuhimu wa umoja wa kitaifa, alisema: Tofauti za kimadhehebu na kisiasa hazipaswi kuzuia safu kuungana mbele ya “adui wa pamoja”, yaani Marekani na utawala wa Kizayuni.

Katika ujumbe wake wa kindugu na wa kifamilia, alisema: “Sisemi kwa mtazamo wa kisiasa, bali nasema kwa kama baba; watoto wetu wote walioko katika vikosi vya usalama, Al-Hashd Al-Shaabi na Muqawama ni ndugu zetu, na juhudi yoyote ya kuuvunja umoja huu au kutumia nguvu dhidi ya upande wowote miongoni mwao, itakutana na umoja wa wananchi.”

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha