Kwa mujibu wa Kitengo cha tarjama cha Shirika la Habari la Hawza, Muqtada Sadr, kiongozi wa Harakati ya Kitaifa ya Kishia nchini Iraq, siku ya Jumatano alitangaza kuwa; “Saraya al-Salam” itajitenga na Harakati ya Sadr.
Sadr alisema kuwa: Uamuzi huu umechukuliwa kwa kuzingatia maslahi ya taifa kwa ujumla na katika muktadha wa hatari zinazoikabili nchi.
Aliongeza kusema: Taasisi zisizo za kijeshi zinazohusiana na “Saraya al-Salam” zitahamishiwa kwenye “Bunyan Marsous”, bila kuwa na makao yoyote, silaha, sare, nembo au kitu kingine chochote.
Uamuzi huu wa Muqtada Sadr umefanyika sambamba na harakati za kisiasa zinazolenga kushughulikia suala la silaha za “makundi yenye silaha” na kukabidhi silaha hizo kwa serikali.
“Saraya al-Salam” ni tawi la kijeshi la Harakati ya Kitaifa ya Kishia (ambayo hapo awali ilijulikana kama Harakati ya Sadr) chini ya uongozi wa Muqtada Sadr. Muundo huu uko rasmi chini ya mwamvuli wa taasisi ya serikali ya Hashd al-Shaabi (vikosi vya 313, 314 na 315), na una jukumu la kutekeleza majukumu muhimu ya kiusalama katika maeneo mbalimbali ya Iraq, hususan mji wa Samarra.
Baadhi ya harakati za kisiasa pamoja na makundi yenye silaha pia — kwa mujibu wa maelezo ya chanzo cha serikali — vimeonesha msimamo wa kubadilika kuhusu suala la kuweka silaha chini ya mamlaka ya serikali, ilhali hapo awali vilikuwa na msimamo mkali kuhusu jambo hilo, chanzo hicho pia kiliongeza kuwa; mchakato wa kukabidhi silaha utafanyika kwa mujibu wa ratiba maalumu.
Katika mpango wa wizara ya serikali ya Ali al-Zaidi — ambayo ilifanikiwa kupata kura ya imani kutoka Bunge la Wawakilishi la Iraq — kuna kipengele kinachohusu kuhodhi silaha mikononi mwa serikali pekee, Sadr pia baada ya serikali hiyo kupata kura ya imani, alisisitiza suala hilo.
Maoni yako