Kwa mujibu wa kitengo cha tarjuma cha Shirika la Habari la Hawza, Hujjatul Islam wal Muslimin Sheikh Ali Al-Khatib, Naibu Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Kiislamu la Mashia nchini Lebanon, katika taarifa yake amesema kuwa; kumbukumbu ya miaka ishirini na sita ya ukombozi inakuja katika mazingira magumu ambayo nchi inateseka kutokana na mashambulizi ya mara kwa mara ya Israel dhidi ya Lebanon; hata hivyo, tukio hili haliwezi kuchukuliwa kuwa ni kumbukumbu ya kupita katika historia ya Lebanon, kwa sababu lina maana ya kina katika fikra za watu, hususan katika kipindi hiki maalumu.
Alisema: Katika tukio hili tunawakumbuka wapiganaji mashujaa, watu wa muqawama na mashahidi watukufu ambao waliandika ukurasa usiosahaulika katika historia; ukurasa ambao kwa sababu ya misingi na hakika zilizojikita katika nyoyo za Walebanon, Waarabu na Waislamu, hautafutwa na kupita kwa zama. Hili linapaswa kuwa funzo kwa wote wanaojihusisha na masuala ya kisiasa rasmi na yasiyo rasmi, huenda ukumbusho ukawanufaisha Waumini, katika siku hii yenye baraka, tunawakumbuka watu wa taifa walioandika misimamo iliyochongwa kwa kina katika kurasa za historia na kuwa nyimbo katika vitabu vya watoto na watu wazima, katika vikao vya baba na mama pamoja na mashairi ya washairi na waandishi.
Sheikh Al-Khatib aliongeza kuwa: Katika siku hii yenye baraka tunamkumbuka Sayyid wa Muqawama na kiongozi wake, shahidi mtukufu Sayyid Hassan Nasrallah, ambaye akiwa hatua chache kutoka kwa utawala ghasibu, alisimama mjini Bint Jbeil na kutangaza kwa sauti kubwa kwamba “Israel ni dhaifu kuliko nyumba ya buibui.” Kauli hii iligeuka kuwa nembo mashuhuri katika fasihi ya kisiasa na kijeshi ya muqawama, na akautoa ushindi huu mkubwa kwa Lebanon yote na kwa Waarabu na Waislamu wote, na kuiomba serikali ya Lebanon ijitahidi kufuta athari za uchokozi na ukaliaji kutoka katika sura ya kusini; lakini mwito huu haukupata mwitikio, na mpango wa maendeleo ya kusini ulifanywa upya kwa juhudi za wananchi wake, wakaazi wake na wahamiaji wake pamoja na baadhi ya misaada yenye thamani kutoka kwa Waarabu.
Naibu Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Mashia aliendelea: Katika siku hii tunakumbuka misimamo ya Imam Musa Sadr, kiongozi aliyetekwa, ambaye alikuwa mwanzilishi wa muqawama wenye ushindi na aliyetangaza kauli mbiu kwamba “Israel ni shari tupu na kufanya muamala nayo ni haramu.” Kauli mbiu hii baadaye iligeuka kuwa moja ya misingi ya Waumini katika kukataa uhalali wa kuiteka Palestina na Wazayuni duniani.
Aliongeza: Katika siku hii tunakumbuka misimamo ya Mheshimiwa Nabih Berri, Spika wa Bunge, ambaye katika uchambuzi wake wa tukio hili kubwa alitabiri kwamba dunia ya Kiarabu na Kiislamu haitaukumbatia ushindi ambao watu wa Jabal Amil waliuandika, alisema: “Ukombozi unapaswa kuwa tukio la kuimarisha umoja wa taifa, kuijenga upya kusini na kuthibitisha mamlaka ya Lebanon.”
Sheikh Al-Khatib alisema: Katika siku hii tunamkumbuka Rais mpambanaji Emile Lahoud ambaye alikuwa mshirika katika ushindi huu; kwani aliiweka siku hii kuwa Idi ya kila mwaka ya Muqawama na Ukombozi, akatembea katika ardhi ya kusini na kuhamasisha ari kwa ajili ya mustakabali bora zaidi, na akasisitiza kuthibitisha muungano wa jeshi, taifa na muqawama, na baadaye akakataa kupuuzwa hata kipande kidogo cha ardhi ya Lebanon.
Aliongeza: Katika siku hii tunakumbuka dhamiri ya Lebanon, rais marehemu Dkt. Salim Al-Hoss, ambaye kwa kufanya kikao cha baraza la mawaziri katika shule ya mji uliokombolewa wa Bint Jbeil, alichukua hatua ya kitaifa, ya kishujaa na ya kihistoria kwa ajili ya kuthibitisha mamlaka ya nchi, na akasisitiza kwamba; kujiondoa kwa mkoloni hakumaanishi kabisa kukubali amani na “Israel”, bali utawala huo utachukuliwa kama dola adui.
Naibu Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Mashia alisema: Tunapokumbuka misimamo hii na mingine ya watu wetu, wawe ni wanasiasa, vyama, waandishi au wanazuoni, lengo letu ni kufufua kumbukumbu ya kitaifa iliyojengwa juu ya muqawama ambao uliikomboa ardhi na mwanadamu; ukweli ambao leo baadhi wanajaribu kuufuta na kuusahau. Katika siku hii yenye baraka, tunasisitiza tena misingi ya kitaifa mbele ya uchokozi wa kinyama wa Israel na ukaliaji wa Kizayuni juu ya ardhi yetu; hakuna mtu nchini Lebanon anayeweza kubaki mtazamaji mbele ya kiwango hiki cha uharibifu, kwa hiyo tunataka kuwepo uratibu wa haraka na kamili kati ya serikali ya Lebanon, inayowakilishwa na jeshi, kwa upande mmoja, na muqawama kwa upande mwingine; kwa namna ambayo maamuzi yote ya vita na amani yawe ni maamuzi ya pamoja ya kitaifa na ya kimamlaka, siyo serikali kuwa chombo cha kutekeleza ajenda za nje dhidi ya muqawama.
Aliongeza: Hatutakubali tangazo lolote la kuonesha nia njema kwa adui Muisraeli na hatutatambua uhalali wowote wa njia yoyote ya mazungumzo ya moja kwa moja, bila kujali aina yake, kitu pekee kinachokubalika ni mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kwa upatanishi wa kimataifa usioegemea upande wowote na si kwa upatanishi wa Marekani na Israel, kwa sharti kwamba lengo kuu liwe kusimamisha vita kwa ukamilifu na bila masharti, kujiondoa kwa Israel kutoka katika kila kipande cha ardhi ya Lebanon inayokaliwa, kurejea kwa wakimbizi, kuachiwa kwa wafungwa na kuanza kwa mchakato wa ujenzi upya.
Sheikh Al-Khatib aliendelea: Suluhisho la suala la silaha za muqawama litapatikana kupitia mazungumzo ya Kilebanoni pekee kati ya Walebanon wenyewe; si kwa jeshi lolote ambalo Washington italiunda kwa ajili ya kuondoa silaha za muqawama, ndiyo, tunakubali mazungumzo ya kitaifa ya kweli chini ya mwamvuli wa katiba na sheria ambapo Walebanon wataweka mkakati wa kitaifa wa ulinzi utakaoilinda Lebanon na kuhifadhi haki ya muqawama katika kujibu mashambulizi, silaha za muqawama si sababu ya uchokozi, bali ni radi amali ya ukaliaji na vitisho vya kudumu.
Sheikh Al-Khatib, huku akitoa wito kwa Jumuiya ya kimataifa kutekeleza Azimio 1701, alitaka kusimamishwa kwa ukiukwaji wa kila siku wa azimio hilo kunakofanywa na Israel na kusisitiza kwamba; azimio hilo haliwezi kutekelezwa kwa upande mmoja tu (dhidi ya Lebanon na Hizbullah), ilhali Israel inalikiuka ardhini, baharini na angani bila kizuizi chochote.
Alisisitiza kwamba; serikali ya Lebanon inapaswa kufungua kesi za kimataifa dhidi ya Israel na jeshi lake kwa tuhuma za kufanya jinai za kivita na jinai dhidi ya ubinadamu katika vijiji na miji ya Lebanon, na kutumia njia zote za kisheria kuhifadhi nyaraka za uharibifu na hasara kama ushahidi katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai. Lebanon badala ya kuitegemea Washington ambayo imethibitisha upendeleo wake kamili kwa Israel, inapaswa kuchukua hatua za haraka kuhuisha uhusiano wake na nchi rafiki za Kiarabu na Ulaya na kuunda safu ya msaada wa kisiasa na kifedha kwa ajili ya ujenzi upya na kulinda mamlaka ya nchi, na kufichua juhudi za Marekani za kuitaka Lebanon kutoa fidia chini ya jina la kuondoa silaha kama sharti la amani.
Alisema; Katika tukio hili, hatuna budi isipokuwa kutoa shukrani nyingi kwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambayo tangu mwanzo wa kuanzishwa kwa muqawama kwa ajili ya ukombozi, imeiuunga mkono na bado imesimama imara katika msimamo wake wa uaminifu kwa Lebanon na wananchi wake, kwani inaona makubaliano yoyote na serikali ya Marekani kuwa yanategemea kusimamishwa kwa vita nchini Lebanon na kurejea kwa amani na utulivu katika ardhi hii.
Mwisho, Sheikh Al-Khatib alisema: Kwa msingi huu, tunatoa wito tena kwa viongozi wa Lebanon kutathmini upya misimamo yao na kuweka sera mpya ya kitaifa inayojengwa juu ya kuwahamasisha Walebanon wote katika njia ya ukombozi badala ya kuzama katika mazungumzo yasiyo na matunda, na kuchukua mafunzo kutoka katika roho ya tarehe 25 Mei 2000 kwa ajili ya kuiokoa Lebanon na watu wake kutoka katika shimo la maangamizi.
Na amani iwe juu ya anayefuata uongofu.
Maoni yako