Kwa mujibu wa Kitengo cha tarjama cha Shirika la Habari la Hawza, Hujjatul-Islam wal-Muslimin Sayyid Ahmad Swafi, msimamizi wa kisheria wa Haram Tukufu ya Hadhrat Abal-Fadhl al-Abbas (as) na mwakilishi wa Ayatullah Sistani, wakati wa ziara yake katika “Kamati Kuu ya Kuhuisha Turathi” inayohusiana na Ataba Tukufu ya Abbasiyya, pamoja na kukutana na Sheikh Muslim al-Radhai, mshauri wa kamati hiyo, alisisitiza ulazima wa kufanya juhudi zote kwa ajili ya kuandaa maadhimisho ya maelfu ya miaka tangia kuanzishwa kwa Hawza ya Najaf Ashraf.
Katika mkutano huo, Hujjatul-Islam wal-Muslimin Safi aliarifiwa kuhusiana na mafanikio muhimu zaidi yaliyopatikana na Kamati Kuu ya Kufufua Turathi, pamoja na miradi ya kitamaduni ambayo kamati hiyo inaendelea kuikamilisha.
Mwakilishi wa Ayatullah Sistani katika mkutano huo, huku akisisitiza umuhimu wa kufanya juhudi zinazohitajika kwa ajili ya kuadhimisha maelfu ya miaka ya Hawza ya Najaf Ashraf, alisema:
“Tukio hili lina maana na thamani kubwa zinazodhihirisha hadhi ya kielimu na kiakili ya Hawza hii tukufu; Hawza ambayo imelea maelfu ya mafaqihi, wanafikra na wanafasihi, na imebeba jukumu la kueneza Uislamu na madhehebu ya Shia katika sehemu mbalimbali duniani.”
Kamati Kuu ya "Kufufua Turathi na Jumuiya ya Al-Amid" Zanajadili Maandalizi ya Kongamano la Tatu la Awali la Maadhimisho ya Miaka Elfu ya Hawza ya Najaf Ashraf
Kamati Kuu ya Kufufua Turathi inayohusiana na Ataba Tukufu ya Abbasiyya ilifanya kikao cha uratibu pamoja na Jumuiya ya Kisayansi na Kifikra ya Al-Amid ili kupitia maandalizi yanayohusiana na kongamano la tatu la awali la maadhimisho ya miaka elfu ya Hawza ya Najaf Ashraf.
Kongamano hili katika awamu yake ya tatu litafanyika kwa anuani isemayo:
“Turathi ya Lugha na Fasihi katika Hawza ya Najaf Ashraf ndani ya Karne za Kumi na Tatu na Kumi na Nne Hijria.”
Kikao hicho, kilichoongozwa na Sheikh Muslim al-Radhai, mshauri wa kamati hiyo, kilishuhudia kuandaliwa kwa mipango ya kiutendaji ambayo inaweza kuhakikisha kufanyika kwa mafanikio ya kongamano hili la kielimu. Kongamano hilo linatarajiwa kufanyika mwezi Desemba ujao, sambamba na Siku ya Lugha ya Kiarabu.
Mkutano huu umefanyika katika mfumo wa mfululizo wa vikao vinavyolenga kuangazia juhudi za wanazuoni wa Hawza ya Najaf Ashraf na huduma zao za kielimu katika kipindi cha maelfu ya miaka iliyopita.
Kamati Kuu ya Kufufua Turathi imefanya mazungumzo na Chuo cha Imam Kadhim (as) Kuhusu Maandalizi ya Kongamano hilo.
Ujumbe kutoka Kamati Kuu ya Kufufua Turathi inayohusiana na Ataba Tukufu ya Abbasiyya ulikitembelea Chuo cha Imam Kadhim (as) mjini Najaf Ashraf kwa lengo la kujadili maandalizi yanayohusiana na kongamano hilo.
Katika mkutano huo, pande zote mbili zilijadiliana kuhusu njia za uratibu kwa ajili ya kutekeleza kazi ya pamoja ili kuhakikisha mafanikio ya programu za kongamano hilo, kwa namna inayolingana na malengo yake ya kielimu na kitamaduni, na kuimarisha ushiriki wa taasisi za vyuo vikuu katika kufufua tukio hili muhimu.
Vilevile, pande hizo mbili zilikubaliana kuandaa kikao cha kielimu kuhusiana na Sheikh Miqdad al-Siyuri, kikao ambacho kitachunguza wasifu wake pamoja na mafanikio yake ya kielimu katika mfumo wa programu ya kisayansi ya kongamano hilo.
Mwishoni mwa ziara hiyo, ujumbe uliotembelea ulitoa zawadi ya mkusanyiko wa vitabu na kazi za kielimu kuikabidhi maktaba ya chuo hicho, hatua iliyolenga kuwasaidia wanafunzi na watafiti, pamoja na kuimarisha rasilimali zake za kielimu na maarifa.
Maoni yako