Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, “Jukwaa la Kielimu la Harakati ya Kiislamu” (AFIM) nchini Nigeria, chini ya uongozi wa Sheikh Ibrahim Yaqub Zakzaky, limetangaza kufanyika kwa duru ya thelathini na saba ya “Wiki ya Imam” ikibeba kaulimbiu isemayo: “Mapambano ya Imam Khomeini (ra) dhidi ya utawala wa ulimwengu.”
Tukio hili la kila mwaka ambalo hufanyika kwa lengo la kuenzi urithi wa fikra, mapambano na juhudi za mwanzilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Imam Ruhullah Khomeini (ra), katika njia ya kupambana na dhulma na ubeberu wa kimataifa, mwaka huu litaambatana na programu mbalimbali katika maeneo tofauti ya Nigeria.
Maelezo ya ratiba
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa, tukio hili litafanyika katika sehemu kuu mbili:
Kampeni za uhamasishaji wa kitaifa: Kuanzia tarehe 31 Mei hadi 1 Juni 2026, shughuli za kitamaduni na za uhamasishaji zitafanyika katika taasisi na jumuiya mbalimbali kote nchini Nigeria, jukwaa la Kielimu la Harakati ya Kiislamu limewataka wanaopenda kushiriki kurejea kwa waratibu wa majimbo wa taasisi hiyo kwa maelezo zaidi.
Sherehe ya hitimisho: Mkusanyiko mkuu na wa mwisho wa tukio hili utafanyika tarehe 3 Juni 2026 katika mji wa Abuja.
Makhatibu na wahadhiri waalikwa
Katika sherehe ya hitimisho ambayo itahudhuriwa na shakhsia za kielimu pamoja na wanaharakati wa kijamii, mada mbili kuu zitajadiliwa na kuchambuliwa:
1. “Vyombo vya habari na aina mpya za ubeberu wa kimataifa” hutuba itakayo tolewa na Bi Marzieh Hashemi.
2. “Kutoka Mapinduzi hadi Muqawama: Athari za kimataifa za fikra za Imam Khomeini (ra)” hotuba itakayotolewa na ndugu Nureddin Omeidji.
Aidha, katika sehemu ya programu hiyo, kutafanyika kikao maalumu chenye anuani isemayo: “Nafasi ya wasomi wa vyuo vikuu katika kupinga dhulma za kimataifa.”
Hafla hiyo itahitimishwa kwa hotuba ya mwisho ya Sheikh Ibrahim Zakzaky, jukwaa la Kielimu la Harakati ya Kiislamu limewaalika wananchi wote, wanafunzi, walimu, wanaharakati wa kijamii na wapenda haki wote kushiriki katika tukio hili.
Maoni yako