Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, maandishi kamili ya ujumbe wa Ayatullah A‘rafi, Mkurugenzi wa Hawza za Kielimu nchini Iran, ni kama ifuatavyo:
Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema Mwenye kurehemu
Kwa hadhara tukufu ya waheshimiwa maulamaa, wanachama watukufu wa Baraza la Manaibu na Wakurugenzi na Makao ya “Balagh Mubiin”, pamoja na wakurugenzi waheshimiwa wa mikoa, maeneo, shule, vituo na taasisi za hawza za Qum na kote nchini (Mwenyezi Mungu adumishe daraja zao)
Salaam na maamkizi pamoja na kutakia mafanikio zaidi
Kufuatia jumbe, taarifa na hotuba zilizotangulia, ninaona kuwa ni wajibu wangu kuwapongeza, kuwasifu, kuwashukuru na kuwathamini kwa unyenyekevu nyote nyinyi waheshimiwa pamoja na washirika wenu watukufu, taasisi kuu za hawza, walimu, wabebaji wa ujumbe wa dini, wanafunzi wa dini na waheshimiwa, kwa sababu ya juhudi zenu zinazostahili kusifiwa, uwepo wenu wa uwanjani na uongozi wenu wa tablighi na ubainishaji katika mazingira haya nyeti, maalumu na katika kipindi hiki muhimu cha kihistoria. Pia, pamoja na usia wote wa wakubwa wa hawza na maelekezo yaliyotangulia, napenda kuwasilisha kwenu wasiwasi na tahadhari yangu katika mambo yafuatayo, huku nikisisitiza kwa nguvu juu ya umuhimu wa kuyapa hima na kuchukua hatua za haraka na zenye hekima:
1. Umuhimu wa kuendelea, kupanua na kuimarisha uwepo wa wananchi wapendwa na vijana waungwana katika nyanja, medani, barabara, mitaa, vituo na misikiti uko wazi, na ni lazima itumike fursa hii kwa ajili ya kuinua dini, mwamko, kuimarisha na kueneza maarifa ya maadili ya kidini pamoja na mshikamano wa kitaifa na umoja wa kijamii. Hususan, ni lazima kufunguliwa na kupanuliwa njia za mawasiliano ya fikra na yenye kujenga na kizazi cha vijana pamoja na mabinti na wavulana wetu wapendwa. Haya yote yanategemea ubunifu, uvumbuzi, hamasa, hisia za kitamaduni, tablighi, jihadi, busara na kufanya biashara na Mwenyezi Mungu. Ushindi katika vita hii isiyo sawa unahitaji ubainishaji na kuridhisha umma, jihadi ya uwanjani, kuendelea kwa uwepo wa wananchi na kuwatetea wanajeshi, mfumo wa Kiislamu na uongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu. Na kati ya njia na mbinu zote, kufufua misikiti na kustawisha swala za jamaa na swala za Ijumaa kuna umuhimu wa pekee.
2. Suala jingine muhimu sana ni kuitambulisha hawza ya kielimu, taasisi ya hawza na taasisi ya uulamaa kwa wananchi, vijana, wanafunzi wa shule, wanafunzi wa vyuo vikuu, wasomi na watu wa tamaduni, kuwa ni taasisi inayobeba ujumbe wa maarifa, kiroho, ukombozi, nusura na saada, na taasisi inayowahudumia wananchi na kuhifadhi utambulisho na usalama wa nchi. Jambo hili linahitaji juhudi zaidi, hasa katika kuonyesha sura ya kielimu, kiroho, ya wananchi, ya kimapinduzi na ya kihuduma ya taasisi ya uulamaa; na hilo lisifanyike kwa maneno pekee, bali kwa mwenendo na vitendo vizuri na vyenye mvuto. Nafasi ya baadaye ya hawza na taasisi ya dini inategemea kuongezeka kwa mtaji wa kijamii na wa wananchi, pamoja na urafiki na maingiliano ya taasisi ya uulamaa na hawza na wasomi wa vyuo vikuu, vijana, makundi mbalimbali ya wananchi na wanyonge, hususan tabaka zilizonyongeka na zenye mahitaji. Miongoni mwa mambo muhimu ambayo Ruhollah Khomeini, kiongozi shahidi, wakubwa wa hawza na mara'ji' wakuu wamekuwa wakisisitiza daima ni kushirikiana na kuhusiana na wananchi wa kawaida, kuishi maisha ya wananchi, kuelekea kwa wanyonge, kuwa pamoja na vijana, kupambana na wakandamizaji, pamoja na umoja na ushirikiano baina ya hawza na chuo kikuu.
3. Kwa mtazamo huohuo, ni lazima kuinuliwa mwenendo wa kuvutia, kuchagua na kupokea wanafunzi kwa ajili ya hawza za kielimu katika nyanja za kiwango na ubora, na kutumia vizuri fursa zilizopo. Mustakabali wa hawza, mabadiliko yake na maendeleo ya malengo na mipango yake ya mageuzi, yote yanategemea wanafunzi bora, wenye vipaji, wanaostahili na walio wengi watakaoingia. Hatua ambazo mimi na nyinyi tumechukua hadi sasa hazijafikia lengo linalotarajiwa. Kwa haraka na kwa hekima, ni lazima shule zote, vituo vyote, wanafunzi wa dini, walimu na wakurugenzi waanze kazi kwa ajili ya kuongeza udahili na kuchagua walio bora kwa mwaka huu na mwaka ujao. Kwa roho ya kijihadi na ubunifu wa mipango, kwa ushirikiano wa makao makuu na kituo cha udahili na elimu, waandae mpango mpya na kuleta mageuzi ya msingi.
Mwisho, huku nikitoa shukrani na pongezi pamoja na kuomba radhi kwa mapungufu yote, namuomba Mwenyezi Mungu awape afya, heshima na mafanikio wapendwa wote wa hawza walio na roho ya jihadi na waliopo mstari wa mbele, na pia ushindi wa jeshi la Uislamu dhidi ya ukafiri na dhulma.
Na kutoka kwa Mwenyezi Mungu ndiko kunakotoka tawfiki, nusura na ushindi.
Alireza A‘rafi
Mkurugenzi wa Hawza za Kielimu
Maoni yako