Shirika la Habari la Hawza | Utawala wa Kizayuni kwa muda mrefu ulikuwa ukizungumzia kuuangamiza uwezo wa kivita wa Hizbullah, lakini uhalisia wa vitani katika siku hizi za mapigano kusini mwa Lebanon unasimulia ukweli mwingine kabisa. Hapa chini tunachambua tofauti kubwa iliyopo baina ya ahadi za ushindi za jeshi la utawala huo na hali halisi katika vita dhidi ya Hizbullah huko kaskazini.
Mhimili wa kwanza wa pengo hili ni mgongano uliopo baina ya taarifa rasmi na ukweli wa uwanjani.
Kinyume na madai ya makamanda wa kijeshi kuhusu kuangamizwa kwa sehemu kubwa ya uwezo wa kivita wa Hizbullah, maendeleo ya vitani yanaonyesha kuwepo kwa “pengo la ufahamu”. Jeshi la utawala huo, licha ya kuwa na taarifa sahihi na za kina, lilijaribu kuwasilisha picha ya ushindi kamili kwa maoni ya umma ili kuficha kushindwa kwake kufikia malengo ya kimkakati.
Pili, hisia za kudanganywa miongoni mwa wakazi wa maeneo ya mpakani zinaonekana wazi kabisa.
Wakazi wa maeneo ya kaskazini, hususan katika mji wa “al-Mutla”, wameonesha malalamiko yao dhidi ya utendaji wa utawala wa Kizayuni. Mkuu wa baraza la eneo hilo ametangaza waziwazi kuwa maneno yenye kuvutia kuhusu kulemazwa kwa uwezo wa adui yalikuwa ni kwa ajili ya kuwapotosha walowezi, na kwamba uhalisia katika mitaa ya kaskazini si chochote isipokuwa kukata tamaa na hisia ya kudanganywa.
Tatu, kushindwa kuangamiza uwezo wa makombora na ndege zisizo na rubani wa Hizbullah kumejitokeza wazi.
Katika hali ambayo jeshi la utawala wa Kizayuni lilikuwa likizungumzia kuangamizwa kwa asilimia 80 ya uwezo wa makombora wa mpinzani wake, kuendelea kwa mashambulizi ya kila siku kumefanya takwimu hizo ziwekwe chini ya mashaka. Wataalamu wanaamini kuwa vikosi vya Hizbullah bado vinamiliki zaidi ya makombora elfu 20 hadi 25.
Nne, unyumbufu wa muundo wa uongozi wa Hizbullah umefanya mauaji ya viongozi wa ngazi za juu kutokuwa na athari.
Ripoti za uwanjani zinaonesha kuwa; kuuliwa kwa viongozi wa ngazi za juu wa Hizbullah hakukusababisha kupooza kwa harakati hiyo. Vikosi hivi, kwa kutegemea muundo wa “kutokuwa na uongozi wa kati” pamoja na makamanda wa ngazi za kati, vimeweza kwa haraka kuziba nafasi za viongozi waliopotea. Muundo huu wenye unyumbufu umefanya isiwezekane kwa jeshi la utawala wa Kizayuni kulemaza kikamilifu uwezo wao wa kiutendaji.
Tano, mabadiliko ya mizani kutoka mashambulizi ya moja kwa moja kwenda katika vita vya kumchosha adui yamejitokeza.
Wachambuzi wa Kizayuni wanaamini kuwa Hizbullah imebadilisha mkakati wake kutoka “mashambulizi makubwa” kwenda katika “uchoshaji wa kimfumo” kaskazini. Uwepo wa vikosi maalumu katika mfumo wa timu ndogo ndogo na huru umeifanya misheni ya ulinzi wa anga na ardhini ya utawala wa Kizayuni ya kuhakikisha usalama wa kurejea kwa walowezi kukabiliwa na mkwamo.
Yote haya yanaonesha kuwa propaganda rasmi za wavamizi zimeshindwa mbele ya uhalisia wa ardhini. Kushindwa kuwasilisha simulizi la kweli kumesababisha kuongezeka kwa mgogoro wa kuaminiana baina ya walowezi na taasisi za kijeshi, na kumethibitisha kuwa ushindi wa mwisho uliokuwa ukitangazwa haukuwa chochote isipokuwa kaulimbiu ya kisiasa iliyokuwa mbali sana na uhalisia wa kijeshi.
Alireza Dharkahi
Maoni yako