Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Ayatullah Nouri Hamedani, mmoja wa Marajii wakuu wa taqlidi, katika ujumbe wake kutokana na mnasaba wa kuwadia mwezi mtukufu wa Muharram, ametoa mkono wa pole kwa Imam Mahdi (aj) na kwa wafuasi wa Ahlul-Bayt (as), huku akisisitiza ulazima wa kuadhimisha kwa utukufu na fahari zaidi majlisi za maombolezo ya Mtukufu Aba Abdillah al-Hussein (as).
Matini ya ujumbe huo ni kama ifuatavyo:
Kwa Jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, Mwenye Kurehemu.
Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu ambaye ameumba kila kitu kwa ubora wake kisha akakiongoza, na rehema na amani zimshukie Mbora wa Mitume na Mwongozaji wa njia, Bwana wetu na Nabii wetu Abul-Qasim Muhammad na Ahlul-Bayt wake watoharifu, viongozi waongofu waliyoongozwa, hususan Imam Mahdi anayesubiriwa (as), na laana iwe juu ya maadui wao waliopotea na wanaopoteza wengine.
Mwezi mtukufu wa Muharram umewadia na siku za maombolezo ya Hadhrat Aba Abdillah al-Hussein (as), bila shaka katika kusimamisha na kuadhimisha nembo na alama za Hussein, haipaswi kuwepo uzembe wa aina yoyote, na hakuna programu wala tukio lolote linalopaswa kuyafanya maombolezo ya Bwana wa Mashahidi (as) yawe ya pembeni au kufunikwa; bali mambo yote yanapaswa kuwa katika njia ya kuadhimisha alama za Mwenyezi Mungu na kueneza utamaduni wa Ashura.
Wahubiri waheshimiwa na wasomaji wa kasida na marsiya wanapaswa daima kuzingatia ukweli huu kwamba mhimili wa ulimwengu wa uwepo ni Maimamu Maasumu (as), na hakuna shakhsia yoyote inayoweza kulinganishwa na familia hii ya nuru; kama ilivyokuja katika riwaya tukufu:
«لا یُقاسُ بآلِ مُحمدٍ (صلیالله علیه و آله) مِن هذه الأمة أحد»
“Hakuna yeyote katika umma huu anayelinganishwa na Aali wa Muhammad (saw).”
Kwa msingi huo, inafaa misikiti, huseinia, vikundi vya kidini vya maombolezo na vituo pamoja na mikusanyiko yote ya kidini, sambamba na kujitahidi kuandaa kwa utukufu zaidi sherehe na majlisi za maombolezo, pia zisiwe na uzembe katika kubainisha hukumu za kisheria, mafundisho ya kiitikadi na kujibu shubha; na ziziadhimishe siku hizi kwa hamasa na utambuzi wa Hussein.
Vilevile, ni lazima hali ya sasa ya nchi izingatiwe; Mwenyezi Mungu aepushe mbali, pasiwepo mifarakano, na ziepukwe kauli, tabia na hatua yoyote itakayodhoofisha umoja, mshikamano na muungano wa kitaifa.
Wananchi na viongozi wanapaswa kujiepusha na kila kauli na mwenendo unaosababisha kupotea kwa imani ya umma, viongozi wazungumze na wananchi kwa ukweli na uaminifu, na wananchi pia, kwa kuhifadhi umakini na tahadhari, wasidanganywe na njama za maadui; kwa sababu moja ya malengo muhimu zaidi ya maadui ni kuleta pengo na kutokuaminiana kati ya wananchi na viongozi.
Jambo la mwisho; katika kilele cha mfumo wa Kiislamu kuna Waliyul-Faqih, ambaye maamuzi yake yanapaswa kufuatwa kikamilifu.
Katika hafla zote, zikumbukwe na kuenziwa kumbukumbu za kiongozi shahidi na mashahidi wote walioitetea Iran, na wananchi wahimizwe na kutiwa moyo kuyalinda Mapinduzi ya Kiislamu ambayo mizizi yake imo katika utamaduni wa Ashura na harakati ya Bwana wa Mashahidi, Imam Hussein (as).
Inshaallah Mwenyezi Mungu Mtukufu, kwa baraka za Maimamu Maasumin (as), ailinde na kuihifadhi nchi hii pamoja na taifa tukufu la Iran dhidi ya hatari na madhara yote.
Hussein Nouri Hamedani.
Maoni yako