Jumapili 14 Juni 2026 - 13:00
Ayatullah Kaabi Aeleza Masharti Yanayopaswa Kuzingatiwa kwa Ajili ya Kumaliza Vita vya Kulazimishwa

Hawza/ Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya ya Walimu wa Hawza ya Qom amesema: Mfumo Mtakatifu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kamwe hautavuka mistari myekundu inayohusiana na haki za taifa la Iran, na maamuzi yote yatachukuliwa ndani ya mfumo wa maslahi ya taifa, heshima ya nchi na kulinda haki za wananchi.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Ayatullah Abbas Kaabi katika mahojiano na mwandishi wa Shirika la Habari la Hawza, huku akisisitiza kushikamana kwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na haki za wananchi pamoja na misingi ya kimkakati ya mfumo wa Kiislamu, alisema: “Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kamwe haitavuka mistari myekundu inayohusiana na haki za taifa la Iran, na maamuzi yote yatafanywa kwa kuzingatia maslahi ya taifa, hadhi ya nchi na kulinda haki za wananchi.”

Masharti Yanayopaswa Kuzingatiwa kwa Ajili ya Kumaliza Vita

Mjumbe wa Baraza la Wataalamu wa Uongozi (Majlisi Khubregan) aliongeza: “Katika mijadala inayohusiana na kumalizika kwa vita vilivyolazimishwa na kutoka katika hali ya ‘si vita wala si amani’, masuala kama kurejeshwa kwa mali na rasilimali za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran zilizozuiliwa, kuanzishwa kwa mipango muhimu ya kiusalama kwa ajili ya kupita salama na bila madhara katika Mlango-Bahari wa Hormuz chini ya mamlaka ya Jamhuri ya Kiislamu na usimamizi wa vikosi vya ulinzi vya Iran, kuhifadhi umoja na mshikamano wa mhimili wa Muqawama, pamoja na kumalizika kwa vita katika nyanja zote ikiwemo Lebanon, ni miongoni mwa mambo yanayopaswa kupewa uzito mkubwa.”

Mazungumzo ya Nyuklia Hayana Uhusiano na Kumalizika kwa Vita

Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya ya Walimu wa Hawza ya Qom, akizungumzia kutenganishwa kwa mafaili ya kisiasa na kiusalama ya nchi, alisema: “Kumalizika kwa vita vilivyolazimishwa hakuna uhusiano wowote na suala la mazungumzo ya nyuklia. Mazungumzo ya nyuklia ni suala tofauti ambalo litajadiliwa na kuchunguzwa mahali pake baada ya kumalizika kwa vita, na haifai kuchanganya mambo haya mawili.”

Kurudi Nyuma Mara kwa Mara kwa Marekani ni Matokeo ya Kusimama Imara kwa Taifa la Iran

Ayatullah Kaabi, akirejelea maendeleo ya hivi karibuni katika mahusiano kati ya Iran na Marekani, alisema: “Miongoni mwa mambo muhimu ni kwamba, Donald Trump amelazimika kurudi nyuma mara nyingi katika vipindi mbalimbali, tukio la mwisho la kurudi nyuma lilitokea baada ya vikosi vamizi vya Marekani kupewa adhabu kufuatia matukio ya hivi karibuni ndsni ya kusini mwa eneo.”

Mwanazuoni huyo wa Hawza ya Qom aliendelea kusema: “Upande wa Marekani ulikuwa ukitafuta kutekeleza madai yanayozidi mipaka iliyokubalika na ulionyesha tamaa kubwa mno, lakini hatimaye ulilazimika kuachana na baadhi ya matakwa hayo, hata hivyo, hadi sasa hakuna uamuzi wa mwisho uliochukuliwa kuhusu makubaliano yoyote yanayowezekana.”

Tangazo la Makubaliano Yoyote Litafanywa Tu Kupitia Taasisi Rasmi

Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya ya Walimu wa Hawza ya Qom alisisitiza: “Iwapo uamuzi wowote kuhusu makubaliano ya mwisho utachukuliwa, suala hilo bila shaka litatangazwa na mamlaka husika pamoja na taasisi rasmi za nchi. Kwa hiyo, propaganda na makelele ya vyombo vya habari kuhusu jambo hili hayana uhalali wala athari yoyote.”

Aliongeza: “Maamuzi yote kuhusu masuala makubwa ya nchi hufanyika ndani ya mfumo wa taratibu za kisheria, na kupitishwa au kubadilishwa kwa maamuzi ya kimkakati hufanyika kupitia Baraza Kuu la Usalama wa Taifa na baada ya kuthibitishwa na kuidhinishwa na Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu.”

Uelewa Kamili wa Kiongozi wa Mapinduzi kuhusu Masuala ya Nchi na Kujali Haki za Taifa

Mjumbe wa Baraza la Wataalamu wa Uongozi, akizungumzia nafasi ya uongozi katika kuongoza mambo ya nchi, alisema: “Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu ana ufahamu kamili wa masuala yote ya nchi, na hatua zake maalumu kwa ajili ya kuhakikisha haki za taifa la Iran zinapatikana pamoja na kulinda mistari myekundu ya mfumo wa Kiislamu na maslahi ya taifa zimekuwa daima zikipewa umuhimu mkubwa.”

Ayatullah Kaabi alihitimisha kwa kusema: “Maamuzi ya kishujaa, ya hekima na ya kimkakati yaliyochukuliwa na Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ni mwendelezo wa njia iliyochorwa na Kiongozi Shahidi wa Mapinduzi ya Kiislamu, na yamechukuliwa kwa lengo la kulinda maslahi ya taifa, kuhifadhi nguvu na mamlaka ya nchi, pamoja na kutetea haki za wananchi wa Iran.”

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha