Kwa mujibu wa Kitengo cha tarjama cha Shirika la Habari la Hawza, Joseph Aoun, Rais wa Jamhuri ya Lebanon, katika taarifa aliyotoa amesema: “Kwa uangalifu mkubwa nimefuatilia kutangazwa hati ya makubaliano iliyoafikiwa kati ya Marekani na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, pamoja na msisitizo wake juu ya kusitishwa kwa hatua za kijeshi na kuongezeka mvutano katika eneo hili, ikiwemo Lebanon.”
Ameongeza kuwa: “Katika muktadha huo, ninathamini yaliyomo katika hati hii ya makubaliano, ambayo yanajumuisha kuheshimu uhuru na mamlaka ya Lebanon, pamoja na kuthibitisha kwamba utulivu na usalama wa Lebanon ni sehemu isiyotenganishwa ya juhudi yoyote ya dhati ya kuimarisha utulivu katika eneo hili, hasa baada ya Walebanon kubeba mizigo mikubwa katika kipindi kilichopita.”
Aoun aliendelea kusema: “Wananchi wa Lebanon, hususan wakazi wa maeneo yaliyokumbwa na mashambulizi na uharibifu, ambao wamepoteza wapendwa wao, vyanzo vyao vya mapato na makazi yao, leo wanatarajia kwamba makubaliano haya yatageuzwa kuwa hatua za vitendo ambazo hatimaye zitamaliza mzunguko wa vurugu na kuanzisha kipindi cha utulivu, usalama, kuimarika hali ya maisha na ujenzi upya.”
Rais wa Lebanon pia alisema: “Vilevile, ninazishukuru kwa dhati nchi zote na pande zote zilizoshiriki katika kufanikisha hati hii ya makubaliano, pamoja na wale wote waliojitahidi kuijumuisha Lebanon katika juhudi za kumaliza ongezeko la mvutano na kusitisha hatua za kijeshi katika medani mbalimbali. Juhudi hizi zimefanyika kutokana na uelewa wao wa kiwango cha mateso ambayo wananchi wa Lebanon wameyabeba katika miezi iliyopita.”
Maoni yako