Kwa mujibu wa Kitengo cha tarjama cha Shirika la Habari la Hawza, Sheikh Naim Qasim, Katibu Mkuu wa Hizbullah, katika taarifa iliyotolewa kufuatia kumbukumbu ya mwaka wa kufariki Imam Khomeini na kuhusu maendeleo ya mwisho ya kisiasa, alisisitiza kwamba; Mapinduzi ya Iran yalianza kutokana na msingi wa Kiislamu uliojengwa juu ya misingi ya kupambana na dhulma na ukaliaji wa mabavu, na yakatangaza kwamba hayako Mashariki wala Magharibi.
Aliongeza kuwa: “Licha ya matatizo yote ambayo Mapinduzi ya Iran yalikumbana nayo, Iran ilipiga hatua katika nyanja zote na ikaunga mkono harakati za wapenda uhuru.”
Alisema: “Sisi tunajivunia na tunamshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu kwamba tulimfanya Imam Khomeini kuwa mfano katika mwenendo wa maisha yetu na tukasimama pamoja na uthabiti na haki.”
Sheikh Qasim aliongeza: “Si Mashariki wala Magharibi zilizoiruhusu Iran kutulia katika njia ya tajriba yake ya kisiasa chini ya uongozi wa Imam Khomeini (q.s.), na kwa sababu hiyo wakubwa wenye kiburi waliianzishia Iran vita vya miaka minane. Magharibi na Marekani hazikubali mfano wa Iran wa uthabiti na uadilifu, bali zinataka kuifanya ifuate maslahi yao na uasi wao.”
Alisisitiza kwamba; muqawama wa Lebanon umehamasishwa na njia na fikra za Imam Khomeini, lakini akasema: “Sisi tunapigania ardhi yetu na watu wetu.”
Katibu Mkuu wa Hizbullah aliendelea kusema: “Tunaishukuru Iran ambayo inatusaidia katika kurejesha ardhi yetu na haki yetu katika kukabiliana na uchokozi wa ‘Kizayuni na Marekani’, licha ya changamoto kubwa inazokabiliana nazo.”
Matini kamili ya ujumbe wa Katibu Mkuu wa Hizbullah ni kama ifuatavyo:
بسم الله الرحمن الرحيم
Sifa zote njema ni za Mwenyezi Mungu ambaye aliwatuma Mitume Wake na mbora wao, Mtume wa Mwenyezi Mungu Muhammad (saww), kwa uongofu na dini ya haki; na baada yake akawaweka Maimamu wa uongofu waliolindwa na madhambi, watakatifu na waliotakaswa, pamoja na maswahaba wateule na wanazuoni wa kimungu ili wawafuate, ili wote wawe mizani ya wema na uthabiti na wawe mfano kwa wanadamu.
Kwanza: Salamu na kumuenzi Imam mkubwa marehemu, Imam Khomeini, mhuishaji wa dini na mvunjaji wa nguvu za madhalimu wenye kiburi.
Mwenyezi Mungu Mtukufu aliubariki ubinadamu kwa kuanzishwa harakati ya Imam Khomeini (q.s.) na mapinduzi yake ya kimungu nchini Iran; katika mazingira ambayo Marekani ilikuwa imeitawala Iran na mali zake, na ilikuwa imezitawala nchi nyingi duniani na katika eneo kupitia dhulma na uonevu, huku Umoja wa Kisovieti ukiwa umetawala sehemu nyingine ya dunia.
Mapinduzi haya yalianza kutoka katika msingi wa kimungu na Kiislamu uliosimama juu ya misingi ya haki, uadilifu, kujitegemea, uhuru wa kuchagua, umoja wa Kiislamu, kuheshimu utu wa mwanadamu, kupambana na dhulma na ukaliaji wa mabavu, na kuwatetea waliodhulumiwa duniani.
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilijengwa kwa kura ya maoni ya wananchi, ikaandaa katiba yake na sheria zake, na ikatangaza kwamba: si ya Mashariki wala Magharibi.
Imam Khomeini (q.s.), kwa mtazamo wa kidini na uchaguzi wa fikra na utamaduni, ni miongoni mwa dhihirisho la njia ya kimungu kwa wanadamu wote, kwa yeyote anayetaka kuchagua njia ya maisha ya kibinadamu iliyo imara na yenye uadilifu. Kwa sababu hiyo, makundi mengi ya watu duniani yaliharakia kuukubali uongozi wake na mtazamo wake wa kiimani na wa kimungu, na hii ni haki ya kisheria, hasa ikilinganishwa na chaguzi nyingine za kifalsafa, kimada au za kiadui.
Si Magharibi wala Mashariki zilizoiruhusu Iran kutulia katika tajriba yake ya kisiasa chini ya uongozi wa Imam Khomeini (q.s.). Kwa hiyo wakubwa wenye kiburi, kwa kuitumia Iraq kama njia yao waliianzishia Iran vita vya miaka minane kwa kuhamasisha nguvu za kimataifa na kikanda dhidi yake, kwa lengo la kuuangusha mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu.
Mfumo huu ulisimama imara mbele ya vita kupitia kujitolea kwa mamilioni ya watu, kuhimili mzingiro wa kiuchumi na wa kimataifa, pamoja na uthabiti wa uongozi, wananchi, Walinzi wa Mapinduzi, jeshi na wasomi wake.
Licha ya matatizo na changamoto zote, Iran ilipiga hatua katika nyanja zote na iliunga mkono harakati za ukombozi na safu ya haki, bila kuingilia mambo ya wengine.
Msimamo wake mkubwa zaidi na wenye kung'aa ulikuwa ni kuiunga mkono Palestina ili kuikomboa ardhi yake Quds, na kuiunga mkono harakati ya mapambano dhidi ya uvamizi wa kihalifu wa Israel, ambao ni tishio kwa eneo lote na hata kwa dunia nzima.
Imam Khomeini (q.s.) ni mfano wa kiongozi wa kimungu anayelinda haki na heshima ya mwanadamu, kinyume chake, mfano wa watu wa kitwaghuti ni Marekani, Israel na wengineo ambao wameeneza vita, machafuko, uhalifu, mauaji ya halaiki ya watoto na wanawake, pamoja na kuangamiza kilimo na kizazi katika kiwango cha dunia nzima, Ghaza ni mfano wa wazi wa uhalifu huu mbele ya macho ya walimwengu.
Basi, kati ya hawa, ni nani tunayemchagua kwa ajili ya heshima, utu wa mwanadamu na uthabiti?
Sisi tunajivunia na tunamshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu kwamba tulimfanya Imam Khomeini kuwa mfano katika mwenendo wa maisha yetu na tukasimama pamoja na uthabiti na haki.
Kwa nini Marekani, Magharibi na vibaraka wao wameendelea kuipiga vita Iran kwa kipindi cha miaka arobaini na saba? Kwa nini wanaizingira? Kwa nini wanataka kuizuia isimiliki uwezo wa kujilinda ambao ni haki halali ya kila taifa? Kwa nini wanataka kuzuia urutubishaji wa amani wa uranium ambao unaruhusiwa kwa mujibu wa sheria za kimataifa?
Jibu ni hili: Wao hawaikubali Iran kama mfano wa uthabiti, uadilifu na kujitegemea; bali wanataka Iran iwe mfuasi na mnyenyekevu kwa maslahi yao na ujeuri wao.
Marekani na utawala wa Israel walianzisha vita viwili dhidi ya Iran, na katika njia hiyo wakamuua kigaidi kiongozi wa kimungu Imam Khamenei (q.s.) pamoja na idadi ya makamanda wa kijeshi, kisiasa na wa nyuklia, na wakawaua raia na watoto katika shule zao pamoja na kuharibu miundombinu ya kiraia.
Zote hizi ni dhulma na uchokozi wa wazi mbele ya ulimwengu kwa lengo la kuuangusha mfumo na kuidhibiti Iran.
Lakini hawakufanikiwa, wala hawatafanikiwa dhidi ya taifa hili kubwa la Khomeini ambalo limelelewa juu ya njia ya Hussein, kujitolea na kutoa muhanga.
Na taifa hili, kwa idhini ya Mwenyezi Mungu, chini ya uongozi wa mrithi mwema, Kiongozi Ayatullah Mujtaba Khamenei (d.a.), litaendelea kung'aa.
Muqawama wa Lebanon umechukua msukumo kutoka katika njia na fikra za Imam Khomeini (q.s.) kwa ajili ya kuikomboa ardhi kutoka kwa adui mnyakuzi katika eneo hili, lakini sisi tunapigania ardhi yetu na watu wetu, kwa nia ya kumtii Mola wetu ili tusiwe watumwa kwa yeyote, na ili vizazi vyetu viishi kwa uhuru katika nchi yao pamoja na wananchi wenzao.
Muqawama huu ni zao la Imam Musa Sadr (Mwenyezi Mungu amrudishe salama), na njia ya Sayyid wa mashahidi wa Umma, Sayyid Hassan Nasrallah, pia umeungana na nguvu za kisiasa na makundi mbalimbali yanayoamini katika muqawama na kujitolea katika njia yake.
Pili: Katika kumbukumbu ya mwaka wa kufariki kwa Imam Khomeini (q.s.), ambayo imekutana na Idi ya Ghadir na Wilaya ya Amirul-Muuminin Ali (as) – kiongozi wa uadilifu na msaidizi wa haki – tunachambua hali zetu za kisiasa ambazo zimeathiriwa na matukio haya makubwa, kwa ajili ya kuimarisha njia ya uhalisia na haki.
Tunatoa shukrani kwa Iran ambayo inatusaidia kurejesha ardhi yetu na haki yetu katika kukabiliana na uchokozi wa Israel na Marekani, licha ya changamoto kubwa zinazoiandama, Iran inasimama imara kwa ajili ya kuthibitisha usitishaji wa mapigano wa jumla nchini Lebanon, kama sehemu ya kusimamisha uchokozi dhidi ya Iran.
Matokeo ya mazungumzo ya moja kwa moja yasiyo na maana, ya kudhalilisha na ya kuaibisha kwa Lebanon yamejitokeza, ambayo yamekataliwa kikamilifu na kwa sehemu kubwa ya wananchi wa Lebanon, matokeo haya yanaambatana na tamko la Washington ambalo linaonesha misingi ya Marekani na Israel ya kuitaka Lebanon ijisalimishe kwa mradi wa “Israel Kubwa.”
Kwamba lengo kuu liwe ni kuondoa silaha za muqawama kama mwanzo wa makubaliano yoyote, maana yake ni kuua nguvu ya Lebanon na kuwa tishio la kuwepo kwa mauaji ya halaiki dhidi ya wananchi wetu wenye muqawama.
Hili ni tangazo la kuiharibu Lebanon, kuondoa utulivu wake na kusababisha fitna kati ya Walebanon kwa manufaa ya Israel, ili Israel ipate kwa njia ya siasa kile ambacho haikuweza kukipata kwa njia ya vita.
Jambo hili haliwezekani kwa wale wanaotaka heshima, utu na kuhifadhi damu za mashahidi, majeruhi, wafungwa na wananchi hawa wakubwa wenye kujitolea; kwa sababu sisi si miongoni mwa wanaosaliti amana ya mashahidi, ardhi na mustakabali wa vizazi vyao.
Tamko hili ni ramani ya njia ya kuiangamiza sehemu ya watu wa Lebanon na kuwafanya wengine kuwa watumwa.
Kwamba ichukuliwe njia ya kiusalama chini ya kauli mbiu ya “kusitisha mapigano”, na kufasiriwa kwa namna kwamba Hizbullah inapaswa kusimamisha mapigano na wapiganaji waondoke katika eneo la kusini, huku uchokozi ukiendelea na chini ya shinikizo la kijeshi, kwa hakika hiyo ni kujisalimisha, kushindwa na kutekeleza malengo ya adui, na matumaini ya makubaliano ya namna hiyo ni kama ndoto ya Ibilisi ya kuingia Peponi.
Tutakuwa tunataka tu kusimamishwa kikamilifu kwa uchokozi, kusitishwa kwa mapigano na kuondoka kwa Israel. Usitishaji wa mapigano unapaswa kuwa wa jumla; yaani, pasiwe na mgawanyiko kati ya kusini na maeneo mengine ya Lebanon, na adui wa Kizayuni asiwe na uhuru wa kufanya mauaji katika ardhi ya Lebanon.
Maadamu ukaliaji wa mabavu unaendelea, muqawama utaendelea. Hatukutoa ahadi kwa yeyote kwamba hatutapambana na uchokozi na kutoujibu, maadamu uchokozi unaendelea, sisi tutaukabili kwa nguvu zote tulizonazo, na tutawalenga mahali popote tutakapoamua na kuweza kufanya hivyo.
Maadamu vijiji vyetu havina usalama, vinaendelea kushambuliwa kwa mabomu na kuharibiwa, na watu wetu wanaendelea kuuawa, basi makazi ya Waisraeli pia hayatakuwa salama; na endeleeni kwa nguvu zenu zote.
Wauaji wa Mitume hawatapumzika katika ardhi yetu, tutapigana na maadui hadi tuwatoe katika ardhi yetu na kusimamisha uchokozi wao, kwa kumtegemea Mwenyezi Mungu na msaada Wake, kwa ushujaa wa mashujaa wa muqawama, na kwa msaada wa wananchi wetu wakubwa na wa kipekee ambao wamejitoa muhanga, ambao tunawathamini na ambao wanasimama imara katika kuunga mkono muqawama; na kwa kutumia hazina ya damu za mashahidi.
Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema:
«ولاَ تَهِنُوا فِی ابْتِغَاءِ الْقَوْمِ إِنْ تَکُونُوا تَأْلَمُونَ فَإِنَّهُمْ یَأْلَمُونَ کَمَا تَأْلَمُونَ وَتَرْجُونَ مِنَ اللهِ مَا لاَ یَرْجُونَ وَکَانَ اللهُ عَلِیماً حَکِیماً»
“Wala msifanye ulegevu kuwafukuzia kaumu ya maadui. Ikiwa mnaumia, basi nao pia wanaumia kama mnavyo umia nyinyi. Nanyi mnataraji kwa Mwenyezi Mungu wasio yataraji wao. Na hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi na Mwenye hikima.”
(Surat an-Nisaa: 104).
Sisi tuna yakini ya ushindi wa muqawama huu wa Hussein:
«وَكَانَ حَقًّا عَلَيْنَا نَصْرُ الْمُؤْمِنِينَ»
“Na imekuwa haki juu Yetu kuwasaidia Waumini.”
Lengo kuu linapaswa kuwa ni mamlaka kamili ya Lebanon, ambayo haiwezi kupatikana isipokuwa kupitia suluhisho moja pekee: kusimamishwa kwa aina zote za uchokozi wa Israel dhidi ya Lebanon (katika ardhi, anga na bahari), kuondoka kwa Israel katika ardhi za Lebanon ili jeshi la Lebanon liweze kupelekwa kusini mwa Mto Litani, kuachiwa huru wafungwa, kurudi kwa wananchi katika vijiji vyao vyote na kuijenga upya nchi.
Hatuikubali kabisa kuhusisha “uwepo wa muqawama” na “kusimamishwa kwa uchokozi na kuondoka kwa Israel”.
Maoni yako