Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Ayatullah A‘rafi katika ujumbe wake wa kiuchambuzi na kimkakati amesema kuwa; mfano mkubwa zaidi wa “kutafuta marekebisho” katika zama za sasa ni kumiliki mipaka ya juu ya elimu, akili bandia (AI), pamoja na kufanikisha mamlaka ya kiuchumi na kujitosheleza, ili Umma wa Kiislamu utoke chini ya mijeledi ya unyonyaji na ulaghai wa kimataifa na kubadilisha mizani ya nguvu kwa manufaa ya waliodhulumiwa. Harakati hii ya pande zote leo inapumua katika upeo wa kimataifa na wa kina wa risala ya Hussein, na imevuka mipaka ya migogoro ya kimadhehebu na tofauti ndogo ndogo ndani ya Umma.
Mhimili mwingine wa ujumbe wa Ayatullah A‘rafi ni kwamba; kina halisi cha harakati ya Hussein kimejengwa juu ya “uongozi kamili na usiofungwa na wakati wa tukio la Karbala katika mradi mkubwa wa marekebisho ya misingi ya Umma.” Kuhusu hilo amesisitiza kuwa; harakati ya Hussein haikuwa kamwe mkondo wa kutafuta madaraka, maslahi ya makundi ya kisiasa, ubaguzi wa kikabila, kimadhehebu au kifamilia, bali ilikuwa jibu la hatima kwa upotovu wa kimuundo na wa kina ambao ulikuwa ukiupotosha Umma katika kipindi cha mwanzo kabisa cha historia ya Uislamu.
Mkurugenzi wa Hawza pia amesisitiza katika sehemu ya ujumbe wake kwamba; leo katika kusimama imara, upinzani na jihadi ya Iran, Lebanon na kambi nzima ya muqawama katika eneo hili, tunashuhudia mfano halisi na mwendelezo hai wa tukio la Karbala kama marejeo ya juu ya kusimama kidete, ushujaa na kujitolea mbele ya mashine katili zaidi na uovu duniani. Huu ni uwanja ambao ndani yake aina yoyote ya kurudi nyuma kutoka katika mamlaka ya kitaifa au kukubali maridhiano na utawala haramu wa Kizayuni unaolenga kuangamiza kadhia ya Palestina na kufanya mauaji ya kimbari dhidi ya watu wetu wanaodhulumiwa, ni kuzalisha upya bay‘a kwa Yazid wa zama hizi.
Soma hapa chini ujumbe kamili wa kiuchambuzi na kimkakati wa Ayatullah A‘rafi:
Kwa Jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, Mwenye Kurehemu
Shukrani na sifa zote ni za Mola ambaye kwa mara nyingine ametujalia neema kubwa ya kuifikia siku za Ashura; fursa ya kimalaika ya kuitakasa nafsi, akili na moyo wa ulimwengu wa Kiislamu chini ya nuru, mwongozo, maana na utukufu wa harakati ya Imam Hussein (as). Kwa kuvuma upepo wa Ashura ya Hussein, kwa mara nyingine roho za watu huru duniani hujaa manukato ya harakati kubwa zaidi ya kimarekebisho katika historia ya wanadamu; harakati adhimu ambayo ndiyo dira ya mwongozo wetu katikati ya mabadiliko makubwa ya zama hizi.
Karbala haikuwa na wala si tukio la kihistoria lililofungwa ndani ya mipaka ya mwaka wa 61 Hijria, bali ni mkondo hai na wenye harakati katika kina cha mapambano yetu ya leo, na ni chemchemi inayobubujika ya nguvu ambayo Umma wa Kiislamu kwa msaada wake huvunja minyororo ya udhaifu na utegemezi ili kurejesha utukufu, heshima na nguvu zake miongoni mwa mataifa ya dunia, na kwa sauti moja na historia hutangaza:
«إِنِّی سِلْمٌ لِمَنْ سَالَمَکُمْ وَ حَرْبٌ لِمَنْ حَارَبَکُمْ إِلَی یَوْمِ الْقِیَامَةِ»
"Hakika mimi ni mwenye amani kwa anayekuwa na amani nanyi, na ni mwenye vita dhidi ya anayepigana nanyi hadi Siku ya Kiyama."
1. Mtazamo wa Kirisala kuhusu Ashura: Leo katika uhalisia wa jamii ya Kiislamu, mtazamo wa kirisala kuhusu Ashura unaonesha mshikamano usiovunjika wa vipengele viwili vya msingi: “maombolezo” na “ushujaa.”
Kipengele cha huzuni na hamasa ya kihisia ambacho hubeba damu takatifu ya Karbala ni mstari wa mbele wa kulinda dhamiri ya kibinadamu katika ulimwengu wa leo. Ni kipengele kinachofichua sura mbaya ya dhulma na ubeberu na kuzuia maumbile ya mwanadamu kuzoea hali dhalimu iliyopo na kuikubali.
Kina hiki cha kihisia hukamilishwa moja kwa moja na kipengele cha ushujaa na ujenzi wa nguvu; pale ambapo Hussein (as) katika uwanja wa leo anajitokeza kama kiongozi wa mapinduzi na mjenzi wa ustaarabu, akimpatia mwanadamu mfano bora kabisa wa kusimama kidete dhidi ya mifumo ya utawala wa mabavu na upotoshaji wa kitamaduni.
2. Amana hii ya kihistoria leo imo mabegani mwa wahadhiri, vyombo vya habari, wasanii na waandishi wa fasihi ya Ashura ili wamwasilishe Hussein (as) kwenye kizazi cha vijana na kwa fikra za umma duniani, si kama “mwathirika asiye na mtetezi na aliyejitenga,” bali kama mbunifu wa mustakabali na mchoraji wa mifumo mipya ya ustaarabu.
Damu ya mwenye kudhulumiwa na kisa cha Karbala, kwa namna ambavyo wanafikra na wanazuoni wakubwa wamekifafanua katika tafsiri zao za kiharakati na kihistoria, ndiyo nguvu ya kimkakati na ya kuendesha harakati inayovunja uhalali wa mifumo dhalimu, ni nguvu inayoweza kujenga miundo ya kiustaarabu, kibinadamu na kimaadili inayohitajika kwa ajili ya kuongoza mapambano ya kisasa na kubadilisha mizani ya nguvu.
3. Kina halisi cha harakati hii kimejengwa juu ya “marejeo kamili na ya kuvuka mipaka ya wakati ya tukio la Karbala katika mradi mkubwa wa marekebisho ya msingi ya Umma.”
Harakati ya Hussein haikuwa kamwe mkondo wa kutafuta madaraka, maslahi ya kisiasa ya makundi, ubaguzi wa kikabila, kimadhehebu au kifamilia, bali ilikuwa jibu la hatima kwa upotovu wa kimuundo na wa kina ambao ulikuwa ukipotosha njia ya Umma katika kipindi kile cha msingi na cha mwanzo kabisa cha historia ya Uislamu.
Hussein (as) alisimama dhidi ya mkondo uliopangwa na kuratibiwa ambao lengo lake lilikuwa kuondoa wahyi, kupotosha maadili ya Qur’ani, kusimamisha ufanisi wa Uislamu kama dini na mfumo wa maisha katika nyanja zote, na kuiondolea dini maudhui yake ya kirisala.
4. Kwa msingi wa ushahidi huu wa wazi wa kihistoria, nafasi ya Imam Hussein (as), uimamu wake na uhusiano wake wa moja kwa moja na chemchemi ya wahyi, vinaipa harakati hii uhalali wa kipekee, wa juu na endelevu. Nafasi hii imeifanya kufuata njia ya Hussein kuwa dharura muhimu kwa Umma, na imezipa harakati zote za kisasa za marekebisho zinazolenga kukabiliana na kupotoshwa kwa utambulisho wa Kiislamu uhalali wa hali ya juu; harakati ambayo falsafa yake ya kina imechukuliwa kutoka katika kauli hii ya milele:
«إنّی لَمْ أَخْرُجْ أَشِراً وَلا بَطِراً وَلا مُفْسِداً وَلا ظالِماً، وَإِنَّما خَرَجْتُ لِطَلَبِ الإِصْلاحِ فی أُمَّةِ جَدِّی»
"Sikutoka kwa ajili ya kiburi, majivuno, ufisadi wala dhulma; bali nimetoka kwa ajili ya kutafuta marekebisho katika Umma wa babu yangu."
5. Marekebisho haya ya kisasa leo yamebeba jukumu la kumkomboa mwanadamu kutoka katika minyororo ya upotoshaji wa fikra na uporaji wa maarifa; hasa katika zama ambazo wanadamu Mashariki na Magharibi wanakabiliana na mgogoro wa uwepo, ambapo mashine ya uyakinifu imeponda utambulisho na asili ya mtu binafsi, na mifumo ya utandawazi imemvua mwanadamu kina chake cha kimaadili na kiroho.
Hapo ndipo sauti ya Hussein (as), akiwa katikati ya mzingiro, inapopenya kuta za historia na kumwambia mwanadamu wa zama za kidijitali:
«إنْ لَمْ یَکُنْ لَکُمْ دِینٌ وَکُنْتُمْ لا تَخافُونَ المَعادَ، فَکُونُوا أَحْراراً فی دُنْیاکُمْ»
"Ikiwa hamna dini na hamuogopi Akhera, basi kuweni watu huru katika dunia yenu."
Kauli hii ni hati hai inayozungumza na asili ya pamoja ya kibinadamu na fitra ya mwanadamu. Inamuokoa mwanadamu wa leo dhidi ya kupotea katika mzunguko wa matumizi kupita kiasi, na inaziweka thamani za uadilifu na uhuru juu ya hesabu za ubinafsi na upuuzi wa kimada wa uliberali uliopindukia.
6. Muunganiko huu wa kimaumbile kati ya harakati ya Ashura na uhalisia wa kisasa una maana ya kwamba; kauli kuu za Ashura ni nguvu inayoendesha na kuchochea moja kwa moja nyanja za kimkakati za Umma.
Tunaposikia sau wa wito wa kutaka heshima ukisema:
«أَلا وَإنَّ الدَّعِیَّ ابْنَ الدَّعِیِّ قَدْ رَکَزَ بَیْنَ اثْنَتَیْنِ، بَیْنَ السِّلَّةِ وَالذِّلَّةِ، وَهَیْهاتَ مِنَّا الذِّلَّةُ»
"Tambueni kwamba mwana wa mtu dhalili amenisimamisha kati ya mambo mawili: upanga au udhalili; na ni mbali sana nasi kukubali udhalili."
Tafsiri yake ya kijiografia na kisiasa katika uwanja wa leo ni kukataa kabisa utawala wa mabavu na ukoloni wa kisasa.
Leo katika kusimama kidete, muqawama na jihadi ya Iran, Lebanon na kambi nzima ya muqawama katika eneo hili, tunaona mfano halisi na mwendelezo hai wa tukio la Karbala kama marejeo ya juu ya kusimama imara, ushujaa na kujitolea mbele ya mashine katili zaidi za uovu duniani. Huu ni uwanja ambao ndani yake aina yoyote ya kurudi nyuma kutoka katika mamlaka ya kitaifa au kukubali kufanya maridhiano na utawala haramu wa Kizayuni unaolenga kuangamiza kadhia ya Palestina na kufanya mauaji ya kimbari dhidi ya watu wetu wanaodhulumiwa, ni kuzalisha upya bay‘a kwa Yazid wa zama hizi.
7. Katika mwendelezo wa njia hii, matakwa ya mradi wa marekebisho wa Ashura katika mapambano yetu ya kielimu na ya kiustaarabu ni kuziba mapengo ya maarifa na teknolojia; kwa sababu mfano mkubwa zaidi wa “kutafuta marekebisho” katika zama za sasa ni kumiliki mipaka ya juu ya elimu, akili bandia (AI), pamoja na kufanikisha mamlaka ya kiuchumi na kujitosheleza, ili Umma wa Kiislamu utoke chini ya mijeledi ya ulaghai na shinikizo za kimataifa na kubadilisha mizani ya nguvu kwa manufaa ya waliodhulumiwa.
Harakati hii ya pande zote leo inapumua katika upeo wa kimataifa na wa kina wa risala ya Hussein, na imevuka mipaka ya migogoro ya kimadhehebu na tofauti ndogo ndogo ndani ya Umma; kwa sababu Hussein (as) wakati alipoondoka hakusimama kwa ajili ya kundi maalumu, bali alisimama kwa ajili ya kurekebisha Umma na kuokoa ubinadamu, kwa kutegemea misingi imara ya Qur’ani na Sunna.
8. Mwamsho huu wa kimaarifa leo unatuita kuhuisha “mtazamo wa kimfumo na kimuundo kuhusu dini na jamii”, ili tuweze kuzima fitna za kimadhehebu na miradi ya utenganishaji inayopangwa na vyombo vya kijasusi vya kigeni, na kufungua safu moja ya muqawama wa kiustaarabu ambayo itavuka tofauti ndogo ndogo kwa ajili ya kulinda Uislamu na kuhifadhi utambulisho wa kifitra wa mataifa.
Hapa ndipo jukumu la kihistoria la wasomi, Hawza na taasisi kubwa za ulimwengu wa Kiislamu linapounganishwa na wito wa kihistoria wa Imam Hussein (as) aliposema:
«أَمَا مِنْ مُغِیثٍ یُغِیثُنَا لِوَجْهِ اللَّهِ؟ أَمَا مِنْ ذَابٍّ یَذُبُّ عَنْ حَرَمِ رَسُولِ اللَّهِ؟»
"Je, yupo wa kutunusuru kwa ajili ya Mwenyezi Mungu? Je, yupo wa kuitetea heshima ya Mtume wa Mwenyezi Mungu?"
Wito huu wa kuomba msaada ni wito hai, wa kisasa na endelevu. Ukimya wa wasomi mbele ya kupotoshwa maadili ya dini, mauaji ya kimbari dhidi ya mataifa yaliyodhulumiwa, na kuondolewa mwamko wa vijana, ni mfano halisi wa kutafuta starehe na kuepuka wajibu kama walivyofanya waliovunja bay‘a mwaka wa 61 Hijria.
9. Kwa kuchapisha waraka huu wa Ashura na ustaarabu, tuna imani ya yakini kwamba: Umma wa Kiislamu haukabiliwi na upungufu wowote, si katika rasilimali zake za kimada wala katika hazina zake za kipekee za kibinadamu, bali ulimwengu wa Kiislamu leo uko katika kizingiti cha kudhihirisha na kuhuisha irada ile ile ya chuma ya Hussein na uoni wa kimaarifa ambao hubadilisha mizani ya nguvu na kuandika upya historia.
Ahadi ya Mwenyezi Mungu kuhusu ushindi wa waliodhulumiwa na kuporomoka kwa viti vya madhalimu na uyakinifu ni ya hakika. Tunatumaini kwamba msimu huu wa Ashura utakuwa hatua yetu thabiti kuelekea kufanikisha “uongozi wa marejeo na utangulizi wa kiustaarabu”, na kuwasilisha mfano wa kimataifa unaolingana na fitra na dhamiri ya mwanadamu.
وَالسَّلامُ عَلَی الحُسَیْنِ، وَعَلَی عَلِیِّ بْنِ الحُسَیْنِ، وَعَلَی أَوْلادِ الحُسَیْنِ، وَعَلَی أَصْحَابِ الحُسَیْنِ الأَحْرَارِ.
Amani iwe juu ya Hussein, na juu ya Ali bin al-Hussein, na juu ya watoto wa Hussein, na juu ya masahaba wa Hussein walio huru.
Alireza A‘rafi
Mkurugenzi wa Hawza nchini Iran
Maoni yako