Jumanne 16 Juni 2026 - 00:00
Wanazuoni wa Kishia na Kisunni wa Kashmir Washirikiana Kulinda Umoja wa Kiislamu

Hawza/ Katika kipindi kinachokaribia kuingia mwezi wa Muharram al-Haram, Kamati ya Uratibu ya Kishia na Kisunni ya Majlis Muttahid Ulama Kashmir ilifanya mkutano mjini Srinagar kwa ushiriki wa wanazuoni, wasomi na shakhsia mbalimbali za kidini na kijamii.

Kwa mujibu wa ripoti ya Kitengo cha tarjama cha Shirika la Habari la Hawza, katika kuelekea kuanza kwa mwezi wa Muharram al-Haram, Kamati ya Uratibu ya Kishia na Kisunni ya Majlis Muttahid Ulama Kashmir iliandaa mkutano muhimu kwenye makao makuu ya Jumuiya ya Wakfu ya Msikiti Mkuu wa Srinagar, Mkutano huo ulihudhuriwa na wanazuoni, viongozi wa kidini, wasomi na shakhsia za kijamii kutoka madhehebu mbalimbali.

Kusisitiza Umoja wa Umma wa Kiislamu na Ushirikiano wa Madhehebu

Washiriki walijadili changamoto zinazoukabili Umma wa Kiislamu katika ngazi za ndani, kitaifa na kimataifa, na wakasisitiza ulazima wa kuimarisha umoja wa Kiislamu, kuheshimiana, kuishi kwa amani pamoja na kuendeleza mazungumzo kati ya madhehebu mbalimbali, wazungumzaji walibainisha kuwa; katika mazingira ya sasa, ushirikiano na maelewano kati ya wafuasi wa madhehebu tofauti ya Kiislamu ni muhimu zaidi kuliko wakati mwingine wowote kwa ajili ya kulinda usalama, uthabiti na mshikamano wa kijamii.

Kulinda Heshima ya Muharram na Kupambana na Uchochezi wa Migawanyiko

Waliohudhuria mkutano huo, huku wakirejelea nafasi adhimu ya mwezi wa Muharram, walisisitiza umuhimu wa kudumisha mazingira ya udugu na mshikamano katika jamii, walitangaza kwamba; hawataruhusu juhudi zozote za kuzua mivutano ya kimadhehebu au kudhoofisha umoja wa kijamii kufanikiwa.

Onyo Kuhusu Matumizi Mabaya ya Mitandao ya Kijamii

Washiriki pia walieleza wasiwasi wao kuhusu baadhi ya sintofahamu na mivutano iliyojitokeza mwaka uliopita kutokana na machapisho yaliyosambazwa katika mitandao ya kijamii, walizitaka taasisi za kidini, makhatibu, wahadhiri na wananchi wote kuwa na uwajibikaji, umakini na msimamo wa wastani wanapotumia mitandao ya kijamii au kutoa maoni hadharani.

Kuwaheshimu Ahlul-Bayt (as), Mhimili wa Umoja wa Kiislamu

Katika mkutano huo, ilisisitizwa haja ya kuhifadhi heshima na nafasi ya juu ya Masahaba watukufu wa Mtume Muhammad (saww) pamoja na Ahlul-Bayt watoharifu (as). Washiriki walieleza wazi kwamba; kauli au vitendo vyovyote vya uchochezi na vya kuleta mifarakano vinapingana na mafundisho ya Kiislamu, umoja wa Umma wa Kiislamu na urithi wa muda mrefu wa kuishi pamoja kwa uvumilivu na maelewano nchini Kashmir.

Washiriki wa mkutano huo walisisitiza tena umuhimu wa mazungumzo, ushirikiano na kuimarisha kuaminiana kati ya wafuasi wa madhehebu ya Kishia na Kisunni, pia walitoa wito wa kuendelea kwa mikutano ya mashauriano na programu za pamoja kwa lengo la kuimarisha mahusiano na kupanua mshikamano wa kijami, aidha walisisitiza kuendelea juhudi za pamoja katika kutatua matatizo ya wananchi na kuendeleza ustawi pamoja na maendeleo ya jamii.

Pendekezo la Kuunda Kamati Maalumu ya Muharram

Katika mkutano huo pia ilipendekezwa kuundwa kamati maalumu chini ya usimamizi wa Majlis Muttahid Ulama Kashmir ambayo itakuwa ikifuatilia kwa karibu maendeleo na hali ya kijamii katika kipindi cha Muharram, na kuchukua hatua zinazofaa kwa wakati iwapo kutatokea vitendo vyovyote vya uchochezi au vinavyotishia umoja wa kidini.

Mwisho wa mkutano, Hujjatul-Islam Sayyid Mujtaba Abbas Mousavi, mmoja wa wanazuoni wa Kashmir, alitoa pongezi kwa nafasi na huduma za Majlis Muttahid Ulama Kashmir pamoja na uongozi wake, hususan Dkt. Maulawi Muhammad Umar Farooq, kwa mchango wao katika kuimarisha umoja wa Kiislamu, kuiongoza jamii na kukuza maelewano kati ya madhehebu mbalimbali.

Alisisitiza umuhimu wa kuhifadhi mila na desturi za thamani za Kashmir za uvumilivu, mazungumzo na kuheshimiana, na akatoa wito wa kuendelezwa kwa mtazamo huo katika jamii.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha