Jumanne 24 Februari 2026 - 11:15
Mapendekezo ya Sheikh Zakzaky kuhusu vikao vya Qur’ani ndani ya mwezi mtukufu wa Ramadhani

Hawza/ Kwa mnasaba wa kuwasili kwa mwezi mtukufu wa Ramadhani na kuongezeka kwa vikao vya tafsiri ya Qur’ani Tukufu katika maeneo mbalimbali ya Nigeria, kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria, Ibrahim Zakzaky, ametoa ujumbe akiwahimiza wafasiri na wanazuoni wa dini kumcha Mwenyezi Mungu na kulinda heshima ya maneno ya Wahyi. Ameonya dhidi ya kubadilisha mimbari za tafsiri kuwa majukwaa ya matusi, kejeli na mabishano yasiyo na faida.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Katika ujumbe wa video uliotolewa, alisisitiza umuhimu wa kuhifadhi utakatifu wa Qur’ani na kuwataka wafasiri waepuke matumizi ya maneno makali au tabia zinazochochea mgawanyiko katika vikao vya tafsiri.

Alieleza masikitiko yake kwamba, baadhi ya watu wamegeuza mazingira ya kiroho ya tafsiri ya Qur’ani kuwa uwanja wa makabiliano, akisema kuwa jambo hilo ni kuukosea heshima utukufu wa Qur’ani na halilingani na heshima ya mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Hatari ya kutafsiri Qur’ani bila elimu na utaalamu

Sheikh Zakzaky alibainisha kuwa, tafsiri ya Qur’ani si jambo la juu juu au rahisi. Alisema kuwa mfasiri kwa hakika yuko katika nafasi ya kubainisha makusudio ya Mwenyezi Mungu, na hili ni jukumu zito sana.

Alifafanua kwamba, ikiwa mtu atatafsiri vibaya maneno ya kiongozi wa kidunia atakuwa amekosea; je, inawezekanaje mtu kuthubutu kutafsiri maneno ya Mola wa walimwengu bila uangalifu wa kielimu na kwa kufuata matamanio binafsi?

Akinukuu hadithi ya Mtume Muhammad (saww), alikumbusha: “Yeyote atakayetafsiri Qur’ani bila elimu au kwa maoni yake binafsi, basi ajitayarishe kuwa makazi yake motoni.” Alisema hadithi hii inaonyesha uzito wa nafasi ya tafsiri na kwamba hakuna nafasi ya kulazimisha mitazamo binafsi; lengo ni kugundua makusudio ya Mwenyezi Mungu pekee.

Sharti la msingi kwa mfasiri: Uwezo na utaalamu

Alisisitiza kuwa, si kila mtu ana sifa za kuingia katika uwanja wa tafsiri. Uwezo na elimu maalumu katika taaluma za Qur’ani ni sharti la msingi kwa mfasiri.

Wale wasio na elimu ya kutosha katika masomo ya Qur’ani hawapaswi kujilazimisha kutafsiri, bali wanapaswa kujifunza au kufaidika na maelezo ya wanazuoni wenye ujuzi na uzoefu.

Aidha, alieleza kuwa; mfasiri anapaswa kurejea katika vyanzo vya kuaminika na kazi za wanazuoni wa zamani, ikiwemo tafsiri zilizosimuliwa (tafsir ma’thur) na tafsiri za kilugha, na kuwa na mawasiliano ya mara kwa mara na marejeo hayo.

Alisisitiza kuwa, umahiri katika “sayansi za tafsiri” ni jambo la lazima na lisiloepukika kwa kila anayejishughulisha na tafsiri ya Qur’ani.

Umuhimu wa kurejea kwa wanazuoni wenye sifa

Sheikh Zakzaky alieleza kuwa; kama ambavyo Waumini hurejea kwa wanazuoni wakuu katika masuala ya fiqhi, vivyo hivyo katika kuelewa maana na kina cha Qur’ani wanapaswa kurejea kwa wanazuoni wabobezi na wenye sifa, badala ya kila mtu kutoa maoni kwa mujibu wa matakwa yake binafsi.

Mwisho, aliwahimiza watu wote na wasomi kuiheshimu nafasi ya Qur’ani Tukufu, akionya kwamba, kubadilisha vikao vya tafsiri kuwa uwanja wa tuhuma na majibizano hakutazaa chochote isipokuwa kueneza mgawanyiko na kuwanyima watu baraka za kiroho za maneno ya Wahyi.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha