Jumatatu 5 Januari 2026 - 07:33
Bibi Zaynab (sa): Shujaa alie okoa maisha ya Imam Sajjad (as) dhidi ya Yazidi

Hawza/ Bibi Zaynab (sa) alikuwa mwanamke mwenye akili, ujasiri na subira ya kipekee; kwa ufahamu kamili wa misukosuko, aliandamana na Imam Hussein (as), na kwa hotuba zake pamoja na uongozi wake wakati akiwa mateka, aliuhuisha ujumbe wa Ashura. Kuhusu kufariki kwake, yamesimuliwa maoni mawili: kufa kifo cha kawaida au kuuwawa kishahidi.

Kwa mujibu wa taarifa ya Shirika la Habari la Hawza, mojawapo ya maswali yanayoulizwa kuhusiana na Bibi Zaynab (sa) ni namna ya kufariki kwake, jambo ambalo wanahistoria na watafiti wamelijibu.

Yasemekana kuwa: kwa mujibu wa baadhi ya maandiko, bibi huyo mtukufu aliugua na akafariki kwa njia ya kawaida; na uwezekano huu unaonekana kuwa wa karibu zaidi na uhalisia, kwa kuwa alikumbana na mateso na misiba mingi sana, na kutokana na hayo akaumwa.

Kwa mujibu wa baadhi ya uwezekano mwingine, Bibi Zaynab Kubra alipewa sumu na watu wa Yazid na akafariki kishahidi; na uwezekano huu nao si wa mbali, kwa kuwa bibi Zaynab alishuhudia matukio yote ya Karbala, na uwepo wake ulikuwa ukumbusho wa misiba ya Karbala na maafa ya utawala wa Yazid, jambo ambalo Yazid hakuweza kulivumilia. Hata hivyo, maadui hawatoi nyaraka zinazoacha ushahidi wazi wanapotekeleza vitendo hivyo; hufanya kwa siri na kwa kificho.

Pia kuna tofauti za maoni kuhusu tarehe na siku ya kufariki kwake. Maarufu ni kwamba alifariki tarehe 15 Rajab mwaka 62 Hijria, siku ya Jumapili.

Hapa chini tunapitia kwa kifupi baadhi ya vipindi vya historia yenye misukosuko ya maisha ya bibi huyo mtukufu, kuanzia kuzaliwa kwake hadi kufariki, kutokana na mnasaba huu:

Kuzaliwa, ndoa na watoto

Bibi Zaynab Kubra (sa) alizaliwa siku ya tano ya mwezi Jamadi al-Awwal mwaka wa tano au wa sita Hijria katika mji wa Madina Munawwara. Jina lake tukufu ni Zaynab, na kunia zake ni Ummu al-Hasan na Ummu Kulthum. Lakabu zake ni pamoja na: As-Siddiqat as-Sughra, Ismat as-Sughra, Waliyatullah al-Udhma, Namus al-Kubra, Sharikat al-Hussein (as), na Alimah Ghayr Mu‘allamah, Fadhilah, Kamila, na mengineyo.

Baba yake mtukufu ni kiongozi wa kwanza wa Mashia, Amirul-Mu’minin Ali bin Abi Talib (as), na mama yake mtukufu ni Bibi Fatima Zahra (sa). Mume wake mtukufu alikuwa Abdullah bin Ja‘far bin Abi Talib. Katika kitabu I‘lam al-Wara, imetajwa kuwa bibi huyo mtukufu alikuwa na watoto watatu kwa majina ya Ali, Awn na Ja‘far, na binti mmoja kwa jina la Ummu Kulthum.

Akili na busara ya kipekee

Mwandishi wa kitabu Asawir min Dhahab anaandika kuhusu kumbukumbu na busara ya bibi huyo mtukufu akisema: katika kuthibitisha ukubwa wa akili na busara yake, inatosha kusema kuwa hotuba ndefu na tukufu aliyotoa Bibi Siddiqat Kubra Fatima Zahra (sa) akitetea haki ya Amirul-Mu’minin (as) na kuhusu kupokonywa Fadak mbele ya Masahaba wa Mtume (saww), imenukuliwa na Bibi Zaynab (s).

Na Ibn Abbas, pamoja na hadhi yake ya juu na cheo chake kikubwa katika hadithi na elimu, amenukuu kutoka kwake na humtaja kwa jina la Aqilah. Kama anavyoandika Abul-Faraj Isfahani katika Maqatil: Ibn Abbas amenukuu hotuba ya Bibi Fatima (sa) kutoka kwa Zaynab (sa) na kusema: “Haddathatni Aqilatuna Zaynab bint Ali (as)…” Tutilie maanani kwamba Bibi Zaynab (as), licha ya kuwa alikuwa msichana mdogo (yaani mwenye umri wa miaka saba au chini ya hapo), aliihifadhi hotuba hii ya ajabu na fasaha yenye maarifa ya Kiislamu, falsafa ya hukumu na masuala mengi, kwa kusikia mara moja tu, na akawa miongoni mwa wapokezi wa hotuba hiyo tukufu na fasaha.

Mapenzi maalumu ya Zaynab kwa Imam Hussein (as)

Allama Jazaairi anaandika katika kitabu Al-Khasa’is az-Zaynabiyyah: Bibi Zaynab (sa) alipokuwa mchanga na katika beseni la mtoto, kila alipokuwa hampati ndugu yake Hussein (as), alikuwa analia na kutulia kwa shida; na macho yake yalipomuona Hussein (as), alifurahi na kutabasamu. Alipokua, wakati wa kuswali, kabla ya kuanza swala, kwanza alimtazama Hussein (as), kisha akaswali.

Kuwa pamoja na Hussein kama sharti la ndoa ya Zaynab (sa) na Abdullah

Imesemekana kuwa: Amirul-Mu’minin (as), alipomwozesha Zaynab (sa) kwa mpwa wake Abdullah bin Ja‘far, aliweka sharti katika ndoa kwamba Zaynab akitaka kusafiri pamoja na ndugu yake Imam Hussein (as), asizuiwe wala kukatazwa. Na pale Abdullah bin Ja‘far alipotaka kumzuia Imam Hussein (as) kwenda Iraq, lakini Imam hakukubali, Abdullah akakata tamaa na akawaamuru wanawe wawili, Awn na Muhammad, waandamane na Imam kwenda Iraq na wapigane na kujitolea mhanga mbele yake.

Ujasiri unaofanana na wa Hussein (as)

Kuhusu bibi huyo wa kipekee, mara nyingi huzungumziwa zaidi ushiriki wake Karbala, kuandamana na ndugu yake mtukufu, pamoja na kusimamia mateka wa Karbala na kufikisha ujumbe wa Ashura. Ujasiri wa Hussein (as) ulikuwepo pia kwa dada yake Zaynab (sa); au Zaynab (sa), katika nafasi ya ujasiri—bila kuzingatia suala la uimamu—hakupungukiwa kwa chochote ikilinganishwa na Hussein (as). Nguvu ya moyo wake, kwa baraka ya kuunganishwa kwake na Chanzo cha Juu kabisa, inashangaza akili. Sheikh Shushtari anasema: kama Hussein (as) alikuwa na uwanja mmoja wa mapambano Karbala, basi Zaynab mtukufu (sa) alikuwa na viwanja viwili vya mapambano: cha kwanza ni baraza la Ibn Ziyad, na cha pili ni baraza la Yazid muovu. Hata hivyo, tofauti katika mwonekano ni kwamba mapambano ya Hussein (as) yalikuwa akiwa amevaa vazi lililorithiwa kutoka kwa Mtume (saww), akiwa na kilemba cha Mtume kichwani, joho lake begani, mkuki pamoja naye na upanga mkononi, amepanda kipando cha Mtume (saww), akaingia vitani kwa heshima na ujasiri hadi akauawa kishahidi.

Zaynab na kuacha starehe za dunia

Katika nyumba ya mume wake, alikuwa na kila aina ya neema na starehe kwa kiwango cha juu: watumwa, vijakazi na vyombo vyote vya faraja; kwa ufupi, Zaynab aliishi katika nyumba isiyo na upungufu wowote. Ghafla akaona Hussein (as) anataka kuondoka; akaacha starehe na faraja zote, akajitosa katika bahari ya matatizo na mashaka. Kama asingelijua yaliyo mbele, isingekuwa jambo kubwa; lakini tangu usiku wa tarehe 28 Rajab, alipondoka Madina pamoja na ndugu yake kwa hofu na tahadhari kuelekea Makka, alikuwa tayari amejiandaa kwa misiba aliyosimuliwa na babu yake Mtume wa Mwenyezi Mungu (saww) pamoja na baba na mama yake. Kwa elimu na yakini kwamba anaelekea katika mateso makali, je, inawezekanaje kwa Zaynab—binti wa Sultan wa kweli na wa dhahiri, na mke wa Abdullah—aende katika safari itakayoishia utumwani, kutangatanga jangwani na kuvumilia tabu za safari?

Zaynab hatengani na Hussein (as)

Bibi Zaynab Kubra (sa) alikuwa Makka tangu tarehe 3 Sha‘ban mwaka 60 Hijria. Kwa kuwa askari wa Yazid walitaka kumuua Imam Hussein (as) kwa siri huko Makka ndani ya Haram Tukufu ya Mwenyezi Mungu, Imam aliondoka Makka kuelekea Iraq siku ya Tarwiyah, yaani tarehe 8 Dhul-Hijjah. Zaynab (sa) pia alikuwa katika msafara huo. Ibn Abbas alisema: “Ewe Hussein! Ikiwa wewe mwenyewe umelazimika kwenda, basi usiwachukue wanawake.” Zaynab (sa) aliposikia maneno haya, alitoa kichwa chake nje ya howdhah na kusema: “Ewe Ibn Abbas! Unataka kunitenganisha na ndugu yangu Hussein? Mimi na kutengana na Hussein Haiwezekani kamwe.”

Utumwa: fahari ya Zaynab na siri ya kudumu kwa mapinduzi ya Ashura

Baada ya tukio la Karbala, Bibi Zaynab (sa) aliishi takriban mwaka mmoja na miezi sita. Katika msafara wa mateka, pamoja na waliosalia kwenye msafara wa Karbala, alipelekwa Kufa kisha Sham. Ingawa uongozi wa waliosalia ulikuwa mikononi mwa Imam Sajjad (a), Zaynab Kubra (sa) pia alibeba jukumu la usimamizi.

Hotuba ya kishujaa ya Zaynab (sa) huko Kufa ilisababisha mabadiliko makubwa ya fikra za umma. Aliposimama mbele ya makelele ya ulevi wa ushindi ya Ubaydullah bin Ziyad, alipokuwa akijivunia ushindi wake na kusema: “Umeonaje alivyofanya Mungu kwa watu wa nyumbani kwako?”, Zaynab (sa) kwa ujasiri usioelezeka alisema: “Sijaona chochote isipokuwa uzuri. Ushahidi wa kifo ulikuwa umeandikiwa. Walienda wenyewe kwenye hatma yao. Hivi karibuni Mwenyezi Mungu atawaleta wao na wewe ili ihukumiwe kati yenu mbele Yake.”

Pale Ibn Ziyad alipoamuru auawe Imam Sajjad (as), Zaynab (sa) kwa ujasiri kamili alimkumbatia mpwa wake na kusema: “Ukitaka kumuua, niue pamoja naye.” Kufuatia msimamo wa Zaynab (sa), Ibn Ziyad alijuta na akaacha kumuua Imam.

Msafara wa walio huru ulipelekwa Damascus. Huko Sham pia, Zaynab (sa) aliweza kubadilisha fikra za umma. Yazid alikuwa ameandaa kikao cha kusherehekea ushindi; mbele ya waliosalia kwenye tukio la Karbala, aliweka kichwa kilichokatwa cha Hussein (as) ndani ya beseni na kukipiga kwa fimbo. Zaynab Kubra (sa), kwa hotuba yake, aliuvunja kiburi cha Yazid na kumfanya ajute aliyoyafanya. Hatimaye Yazid alilazimika kuurudisha msafara Madina kwa heshima.

Huko Madina pia, Zaynab (sa), mjumbe wa mashahidi, hakunyamaza. Kwa sauti yake aliwachochea watu wa Madina dhidi ya utawala wa Yazid. Mtawala wa Madina akajaribu kumfukuza Bibi Zaynab (sa). Kwa mujibu wa baadhi ya maandiko, alisafiri kwenda Sham na akafariki huko. Wengine wamesema kuwa alihamia Misri na akafariki tarehe 15 Rajab mwaka 62 Hijria.

Rejea:

1. Muntakhab at-Tawarikh, uk. 67
2. Zaynab al-Kubra min al-Mahd ila al-Lahd, uk. 592
3. Luhuf, uk. 218; Muqarram, Maqtal al-Hussein, uk. 324; Irshad, Juzuu ya 2, uk. 144
4. Irshad, uk. 116–117; Bihar al-Anwar, Juzuu ya 45, uk. 117.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha