Jumamosi 27 Desemba 2025 - 17:00
Ibada tano muhimu zinazohimizwa kufanywa ndani ya Mwezi wa Rajabu

Hawza/ Mwanazuoni mashuhuri nchini Tanzania, Maulana Sheikh Hemedi Jalala Mwakindenge, Sheikh Mkuu wa Jumuiya ya Shia Tanzania (TIC) na Mkurugenzi wa Hawza ya Imam Swaadiq (a.s), amesisitiza umuhimu wa Waumini kuhuisha ibada mbalimbali ndani ya Mwezi Mtukufu wa Rajabu, akibainisha kuwa ni mwezi wa maandalizi ya kiroho na kujisogeza zaidi kwa Mwenyezi Mungu.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Maulana Sheikh Hemedi Jalala Mwakindenge aliyasema hayo katika hutuba ya Swala ya Ijumaa iliyoswaliwa katika Msikiti uliopo Makao Makuu ya Jumuiya ya Shia Tanzania (TIC), Kigogo Post, Jijini Dar es Salaam.

Swala na nafasi yake katika kutimizwa ndani ya wakati maalumu

Sheikh Jalala alianza hotuba yake kwa kusoma kauli ya Mwenyezi Mungu isemayo:

{ إِنَّ ٱلصَّلَوٰةَ كَانَتۡ عَلَى ٱلۡمُؤۡمِنِینَ كِتَـٰبࣰا مَّوۡقُوتࣰا }

(Hakika Sala kwa Waumini ni faradhi iliyo wekewa nyakati maalumu.)
[Surah An-Nisāʾ: 103]

Baada ya kusoma aya hiyo tukufu, alieleza kuwa; mara nyingi tunaposoma aya hii akili zetu zinakimbilia kuwa swala za faradhi— ambazo ni Swala ya Subhi, Dhuhuri, Alasiri, Magharibi na Isha— ndizo zenye nyakati maalumu zilizoamriwa kisheria. Lakini hata hivyo, zipo ibada nyingine zilizopendekezwa kufanywa katika nyakati maalumu, hususan ndani ya miezi mitukufu kama Mwezi wa Rajabu.

Ibada zinazohimizwa kufanywa ndani ya Mwezi wa Rajabu

Katika maelezo yake, Maulana Sheikh Hemedi Jalala Mwakindenge alisisitiza kuwa Mwezi wa Rajabu ni miongoni mwa miezi mitukufu ya Kiislamu yenye fursa kubwa ya kujisafisha nafsi, kuongeza ibada na kujiandaa kwa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani. Akazitaja ibada muhimu kama ifuatazo:

1. Kusoma Dua maalumu ya Mwezi wa Rajabu

Sheikh aliitaja dua mashuhuri isemayo: «....يَا مَنْ أَرْجُوهُ لِكُلِّ خَيْر» na kubainisha kuwa; dua hiyo ni miongoni mwa dua muhimu zitakiwazo kusomwa ndani ya Mwezi wa Rajabu, dua hiyo Imam Ja‘far al-Swaadiq (a.s) alimfundisha Muhammad ibn Dhakwān, na akawahimiza Waumini kuisoma kwa ikhlasi na unyenyekevu.

2. Dhikri maalumu za Mwezi wa Rajabu

Maulana Sheikh Jalala alieleza kuwa; ndani ya Mwezi wa Rajabu kuna dhikri maalumu zilizopokewa katika riwaya, ambazo ni sunnah kuzisoma, na dhikri hizo zina mchango mkubwa katika kuimarisha uhusiano kati ya mja na Mola wake pamoja na kuutakasa moyo.

3. Swala maalumu za Mwezi wa Rajabu

Aidha, alifafanua kuwa; kuna swala maalumu zinazopendekezwa kufanywa ndani ya mwezi huu, miongoni mwa swala hizo ni kuswali rakaa 60 kwa mpangilio maalumu. Alibainisha kuwa swala hizo huswaliwa kwa rakaa mbili kila usiku, na baada ya kila swala, husomwa dhikri maalumu kama ilivyopokelewa katika vyanzo vya Kiislamu.

4. Kusoma Dua ya Imam wa Zama (a.f)

Miongoni mwa ibada muhimu alizozisisitiza ni kusoma Dua ya Imam wa Zama (a.j), akieleza kuwa; dua hiyo husaidia kuimarisha uhusiano kati ya Waumini na Imam wao na kuhuisha hisia ya uwajibikaji wa kidini na kijamii.

5. Kufunga swaumu ndani ya Mwezi wa Rajabu

Pia aliwahimiza waumini kufunga swaumu ndani ya Mwezi wa Rajabu, akibainisha kuwa; kufunga katika mwezi huu ni sunnah yenye thawabu kubwa na ni njia bora ya kujiandaa kimwili na kiroho kwa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

Wito kwa Waumini

Maulana Sheikh Hemedi Jalala Mwakindenge alihitimisha hotuba yake kwa kuwataka Waumini kuutumia Mwezi wa Rajabu kama fursa ya dhahabu ya kuongeza ibada, kujirekebisha kimaadili, na kujiandaa kikamilifu kwa Miezi Mitukufu inayofuata, hususan Sha‘bani na Ramadhani.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha