Jumanne 23 Desemba 2025 - 17:30
Mwezi wa Rajabu ni Fursa Adhimu ya Kufanya Mabadiliko na Kuijenga Nafsi

Hawza/ Ayatullah Marwī katika hitimisho la darsa yake ya fiqhi alisema: “Tuufanye mwezi wa Rajab kuwa mwanzo wa kuzijua zaidi dua za Ahlul-Bayt (a.s); ni kwa lugha gani tunaweza kusema kwamba Sahifa Sajjadiyya imepuuzwa na kutelekezwa nasi?”

Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Habari la Hawza, Ayatullah Jawād Marwī, Katibu wa Pili wa Baraza Kuu la Hawza, katika hitimisho la darsa yake ya juu ya fiqhi siku ya Jumatatu, tarehe mosi ya mwezi wa Rajab 1447 Hijria, alielezea nafasi na umuhimu wa mwezi huu mtukufu. Maelezo kamili ni kama ifuatavyo:

Kwa jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu

Leo, kutokana na mnasaba wa kuingia mwezi wa Rajab, tutataja mambo mawili:

Kwanza kabisa, nawapongeza  wote kutokana na maadhimisho ya kuzaliwa Imam Muhammad al-Bāqir (a.s). Baadhi ya watu wanasisitiza kwamba mara kwa mara tuzungumzie angalau jambo moja au mawili. Mimi binafsi sina hamasa kubwa ya kuchukua muda wa ndugu zangu, na sababu yake ni kwamba ikiwa mtu atakuwa mtendaji wa yale anayoyasema, basi maneno yake yana athari; la sivyo hayana athari. Na mara nyingi sisi hujiona tukiwa katika kundi la pili, hivyo tunaona uwezekano wa athari kuwa mdogo, na sitaki kupoteza muda wa wengine. Hata hivyo, ninasema hili kwa kuzingatia kwamba imepokelewa kutoka kwa Amirul-Mu’minin Ali (a.s) kwamba: “Kuwaza juu ya kheri humvuta mtu kwenda kwenye kheri.”

Ikiwa tumeelewa vyema maana ya riwaya hii, huenda ikamaanisha kwamba hata kuandaa tu utangulizi wa kuwaza, na mtu akafikiri kuhusu jambo la kheri, humfikisha kwenye kheri hiyo. Kwa msingi huo, ninasema jambo hili ili kunukuu kheri kwa wengine, kwa matarajio kwamba huenda likawa sababu ya mimi mwenyewe kufikia kheri. Mwezi wa Rajab ni mwezi mtukufu sana, na unaweza kuwa chanzo cha mabadiliko ya kivitendo katika mwenendo na maisha ya mtu.

Nukta ya kwanza:

Wakati mwingine husema hivi kwamba mwezi wa Rajab una umuhimu wa kimaudhui (wenyewe) na pia una umuhimu wa kimaelekezo (njia). Kuna riwaya zilizopokewa kuhusu mwezi wa Rajab ambazo baadhi ya kauli zake hazijaja hata kuhusu mwezi wa Ramadhani. Katika Hadith Qudsi Mwenyezi Mungu anasema:

جَعَلتُ هذَا الشَّهرَ (رَجَبَ) حَبلاً بَيني وبَينَ عِبادي فَمَنِ اعتَصَمَ بِهِ وَصَلَ بِي

“Nimeufanya mwezi huu (mwezi wa Rajabu) kuwa ni kamba kati Yangu na waja Wangu; basi yeyote atakayeshikamanisha nayo, atafika Kwangu.”

(Iqba'lul A'mal, juz4, uk 174).

Ikiwa mja anataka kufikia daraja ya kuungana (na Mwenyezi Mungu), basi anapaswa kuutilia maanani mwezi wa Rajab. Watu wakubwa (wanazuoni wakubwa) kwa kawaida huashiria kiini cha mambo na fikra zao muhimu katika wasia wao. Angalieni wasia wa marehemu Sayyid Ali Qadhi na wengineo; katika wasia wao wanawahimiza walengwa wao kuuhusu mwezi wa Rajab, na kueleza jinsi ya kuingia katika mwezi wa Rajab. Hili linaonesha wazi umuhimu wa mwezi huu.

Tunahitaji sana kujijenga upya kiroho na kimaadili. Wakati mwingine kutokana na riwaya tunaelewa kwamba kadiri elimu, umri na cheo chetu vinavyoongezeka, ndivyo tunavyokuwa zaidi katika hatari ya kuharibika; lakini sisi katika maisha yetu hutenda kinyume chake.

Mwanzoni mwa masomo ya kidini, tulikuwa na hali gani ya moyo, nia gani, fikra na malengo gani? Mtu anapozuru vyumba vya wanafunzi wachanga wa hawza, hufurahia; vitabu vimetandazwa, na sambamba na hilo wanatafuta masuala ya kiroho. Lakini ni nini hutokea kwamba kadiri vyeo vinavyopanda, kana kwamba tunakuwa watupu zaidi katika mambo ya kiroho? Maasum anasema:


یشیب ابن آدم و یشبّ فیه خصلتان: الحرص وطول الامل

 “Mwanadamu huzeeka, lakini ndani yake sifa mbili hubaki changa: tamaa na matarajio marefu.”

(Ashiha'b Filhikam Wal-a'da'b, uk 182)

Kadiri umri unavyoongezeka, sifa mbili ndani ya nafsi ya mwanadamu huongezeka nguvu na kuwaka moto: tamaa na matumaini marefu, ambayo ndiyo chimbuko la matatizo yote. Ni lazima katika fursa hii ya mwezi wa Rajab tutafute mabadiliko.

Tujitengenezee mabadiliko binafsi katika mwezi wa Rajab; tuandae mazingira ya kusimama usiku kwa ajili ya kufanya ibada (tahajjud). Mimi mwenyewe sina chochote mkononi, na sijui hata kama kusema maneno haya kuna faida au la. Lakini je, katika usiku huu mrefu, haiwezekani mtu aamke robo tatu ya saa kabla ya adhana ya alfajiri, akajaza upya hali yake ya ndani? Zamani kabla yetu, walikuwa wakisema kwamba wakati baadhi ya wanazuoni wa maadili huko Najaf walipozungumza kuhusu Swala ya Usiku, wanafunzi waliambiana wao kwa wao: “Ni nani Swala yake ya Usiku imepita hata huyu mwanazuoni anazungumzia umuhimu wa Swala ya Usiku?” Maana yake ni kwamba kuswali Swala ya Usiku kulikuwa miongoni mwa mambo ya lazima kwa mwanafunzi wa elimu ya dini, na hakuhitaji kukumbushwa.

Nukta ya pili:

Tuufanye mwezi wa Rajab kuwa mwanzo wa kuzijua zaidi dua za Ahlul-Bayt (a.s); ni kwa lugha gani tena tuseme kwamba Sahifa Sajjadiyya imekuwa dhalili na imeachwa miongoni mwetu?

Marehemu Agha Jamal Golpaygani, mwanafunzi hodari wa marehemu Naeeni, ambaye wakati mwingine katika masuala ya kiroho alikuwa akimsaidia hata mwalimu wake marehemu Naeeni, alipofikisha umri wa miaka tisini, mwili wake wote ulikuwa umejaa majeraha (bed sores), ambavyo ni miongoni mwa vidonda vigumu zaidi. Habari hiyo ilienea Najaf, na wanazuoni walikuwa wakisema: “Twende tukamwone, tujifunze kutoka katika hali yake ya utulivu.”

Walipomwona, waliona ana utulivu wa pekee. Walimuuliza: “Pamoja na taabu na mateso yote haya, utulivu huu unatoka wapi?” Alikuwa na Sahifa Sajjadiyya pembeni mwake, na akasema mara tatu: “Unatoka hapa.”

Inasemekana kwamba pembeni mwa masomo yake ya kielimu, siku zote alikuwa na Sahifa Sajjadiyya; akisoma kiasi cha masomo ya kielimu, na wakati mwingine akisoma dua kutoka katika Sahifa.

Sasa je, Sahifa Sajjadiyya ipo katika nyumba ya mwanafunzi wa elimu ya dini? Je, tuna ujuzi nayo?

Ikiwa tutaufanya mwezi wa Rajab kuwa njia na chombo kwa ajili ya hili, basi miongoni mwa mambo yatakayokuwa sababu ya kukamilika kwetu ni kwamba katika mwezi wa Rajab tujitahidi kujikita katika jambo hili.

Kuna mambo mengine pia, na tukikaribia masiku meupe, ikiwa tutapata umri na tawfiq, tutayataja. Mwenyezi Mungu atupe sote tawfiq ya kunufaika na fadhila za mwezi huu, na tuombeane dua.

Na rehema na amani zimshukie Mtume Muhammad na Aali zake watoharifu.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha